TUZO YA MO IBRAHIM KUKOSA MSHINDI

 

Nimesikitishwa na habari za Tuzo ya Mo Ibrahim kukosa mshindi mwaka huu, zilizotangazwa hivi karibuni na Kamati ya tuzo hiyo ambayo ni zawadi yenye thamani kubwa dunaini. Tuzo hiyo ilianzishwa mwaka 2006 na bilionea wa nchini Sudan, Mo Ibrahim, kwa ajili ya marais wastaafu wa nchi za barani Afrika.

 

Rais mstaafu anayestahili kupewa tuzo hiyo ni aliyewezesha nchi yake kuwa mfano mzuri wa kuigwa kwa utawala wa kidemokrasia, uhuru binafsi, kuheshimu haki za binadamu, uthabiti wa kisiasa na maendeleo ya kiuchumi.

Tuzo ya Mo Ibrahim ilipangwa kutolewa kila mwaka, ambapo mshindi hukabidhiwa kitita cha dola za Kimarekani milioni tano kwa mwaka katika kipindi cha miaka 10 mfululizo, na dola 200,000 kwa kila mwaka kwa maisha yake yote duniani.


Mwaka jana (2011), Kamati ya Tuzo ya Mo Ibrahim ikiongozwa na Mtanzania, Dk. Salim Ahmed Salim, ilikutana jijini London, Uingereza na kumtangaza Rais mstaafu PedroVerona Rodrigues Pires wa Cape Verde, kuwa mshindi wa tuzo hiyo kwa mwaka huo.

 

Marais wengine wastaafu waliowahi kuibuka washindi na kutunukiwa tuzo hiyo ni Joaquim Chissano wa Msumbiji (mwaka 2007) na Rais Festus Mogae wa Botswana (mwaka 2008).


Hata hivyo, Tuzo ya Mo Ibrahim haikutolewa mwaka 2009 na 2010 kutokana na kilichoelezwa na Kamati ya tuzo hiyo kuwa ni kukosekana kwa washindi (marais waliotimiza vigezo vya utawala bora barani Afrika).


Kama hiyo haitoshi, kwa mara nyingine tena, tuzo hiyo imekosa mshindi mwaka huu. Hakuna aliyekidhi vigezo vya kuitwaa miongoni mwa marais wastaafu walioshindanishwa mwaka huu. Hizi ni dalili mbaya katika mustakabali wa uongozi katika Bara la Afrika.

 

Hicho ni kipimo kinachothibitisha moja kwa moja kwamba dhana ya uongozi bora inatoweka kwa kasi ya kutisha katika mataifa yanayounda Bara la Afrika. Dhana ya uongozi bora wa kisheria na unaoheshimu haki za binadamu barani Afrika inaelekea kumezwa na utawala wa kimabavu, kidikteta, kidhalimu na usiojali wananchi!


Viongozi wengi wa mataifa ya barani Afrika wamegeuka vinara wa kutanguliza maslahi yao binafsi na kuweka kando misingi thabiti ya uongozi bora wa kidemokrasia, unaoheshimu haki za binadamu na unaoshughulikia ipasavyo maendeleo ya kiuchumi na kijamii.


Katika mazingira ya aina hiyo, kuna hatari ya Tuzo ya Mo Ibrahim kuendelea kukosa mshindi katika miaka ijayo, hali ambayo itakwaza dhamira nzuri ya bilionea huyo wa nchini Sudan, inayolenga kuhamasisha uongozi bora katika nchi za barani Afrika, kwa lengo kuu la kuboresha maisha ya jamii husika.


Fikra ya Hekima inafikiri kuwa kuna haja ya marais wa sasa wa mataifa yanayounda Bara la Afrika kutafakari kwa makini kasoro ya tuzo hiyo kukosa mshindi mara tatu (mwaka 2009, 2010 na 2012), kubaini waliowatangulia waliteleza wapi na wao sasa wanapaswa kufanya nini ili kukidhi vigezo vya kutwaa tuzo hiyo baada ya kustaafu.


Ninasema hivyo kwa sababu itakuwa aibu kubwa kwa Bara la Afrika kuendelea kukosa marais wastaafu wenye sifa za kutwaa Tuzo ya Mo Ibrahim. Hofu ni kwamba taswira hiyo inaweza kutoa mwanya kwa mataifa ya mabara mengine kulikandamiza na kulinyima bara hili fursa muhimu kwa kisingizio cha ukosefu wa uongozi bora.


Uongozi bora utawezesha wakazi wa Bara la Afrika kuishi maisha bora yaliyopambwa na demokrasia ya kweli, uhuru wa mawazo na kuabudu, ukuaji wa uchumi, na kikubwa zaidi kunufaika na rasilimali zilizopo ipasavyo na kwa usawa.

 

Uchunguzi umebaini kuwa kutoweka kwa uongozi bora barani Afrika ni matokeo ya viongozi wa sasa kujenga kasumba ya kuigeuzia kisogo misingi ya uongozi bora iliyowekwa na viongozi waliowatangulia, wakiwamo Kwame Nkrumah wa Ghana, Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Nelson Mandela wa Afrika Kusini.


Nadhani umefika wakati viongozi wa sasa wa mataifa ya barani Afrika kuheshimu dhamana walizopewa kwa kuhakikisha wanazingatia misingi ya uongozi bora wenye manufaa kwa wananchi waliowapatia ridhaa ya kuongoza.

 

Viongozi wetu watambue kwamba uongozi wa kibabe, kidikteta na kidhalimu hautaishia kuwakosesha Tuzo ya Mo Ibrahim pekee, bali utawaweka katika hatari ya kuadhibiwa na nguvu ya umma, lakini pia wataonekana wakosefu hata mbele za Mwenyezi Mungu.

 

Fikra ya Hekima inatarajia kwamba marais wa sasa wa nchi mbalimbali za barani Afrika watagutuka na kujifunza kutokana na dosari ya Tuzo ya Mo Ibrahim kukosa washindi mara tatu. Itapendeza kuona na kusikia wanaepuka vitendo vilivyosababisha watangulizi wao kukosa sifa za kutunukiwa tuzo hiyo.


Bara la Afrika limejaaliwa na Mwenyezi Mungu utajiri wa rasilimali lukuki, zinazopaswa kutumiwa vizuri na viongozi wetu ziweze kutuendeleza sote katika nyanya mbalimbali zikiwamo za kielimu, kiuchumi na kijamii kwa jumla kulifanya bara hili kuwa mahali pazuri pa kuishi duniani.


Waafrika wengi tungependa kama si kutamani kuona viongozi wetu wanauenzi utukufu huo wa Mungu, kwa kuonesha uongozi bora unaojali maslahi ya wengi badala ya kujikita katika kujitafutia maslahi binafsi kiasi cha kukosa sifa za kutwaa Tuzo ya Mo Ibrahim iliyoasisiwa kwa ajili yao.


 

By Jamhuri