Kinga ni bora kuliko tiba. Mara nyingi magonjwa mengi yanahatarisha afya zetu kwa kutoziweka maanani dalili zake. Bila shaka makala hii leo itakusaidia katika kuzitambua dalili zinazoashiria shambulio la moyo na kuwahi kuwaona wahudumu wa afya.

Uchovu usio wa kawaida

Uchovu usio wa kawaida ni moja ya dalili kuu zinazoashiria kuwa mtu yupo hatarini kupata shambulio la moyo. Dalili hii mara nyingi hutokea zaidi kwa wanawake kuliko wanaume.

Japo ni kawaida kupata uchovu kutokana na shughuli mbalimbali tunazozifanya kila siku ambazo aidha zinatumia nguvu kubwa za mwili, au pia zinatumia akili nyingi, lakini ni muhimu kuutilia maanani uchovu ambao mara nyingi chanzo chake hakijulikani na unaodumu kwa muda mrefu na hata kusababisha kushindwa kufanya shughuli ndogo ndogo hata za nyumbani.

Kukosa pumzi na kupata matatizo kwenye mfumo wa upumuaji mara kwa mara

Wakati mwingine, mtu anaweza kupata hali isiyo ya kawaida ambapo anaweza akajikuta anapata wakati mgumu sana kupumua na hasa wakati wa kuvuta hewa.

Hali hii mara nyingi huwa inatokea kuanzia miezi 6 kabla hadi wakati ambao mtu anapatwa na tatizo hili la shambulio la moyo.

Matatizo yanayojitokeza kwenye upumuaji, sambamba na kuashiria matatizo ya moyo, pia yanaweza kuashiria matatizo mengine makubwa kama vile pumu, na hata magonjwa ya mapafu. Tafadhali uonapo dalili hizi ni vyema kuwaona wahudumu wa afya.

Mapigo ya moyo kutoenda sawa

Hii ni dalili ya wazi ambayo wengi wameizoea, kiafya moyo unatakiwa kuwa na mapigo takribani 70 kwa dakika kwa mtu ambaye kiafya hana tatizo lolote, aidha hali hii huwa inatokea mara chache kwa muda na kutoweka kutokana na sababu chache kama vile woga na hasira.

Kwa wakati ambao mtu anakuwa kwenye hali ya woga au hasira, ni rahisi sana mapigo yake ya moyo kwenda mbio, lakini hata hivyo hali hii hutoweka mara tu hasira na woga vinapokoma. Kuyumba kwa mapigo ya moyo pia ni kawaida kuwapata watu wenye shinikizo la damu, au hata wenye uzito mkubwa uliopitiliza.

Lakini ikitokea hali hii hutokea mara kwa mara hata kwa wakati ambao mtu hayupo kwenye hali ya hasira au woga na hana shinikizo la damu, ni vyema kupata msaada wa daktari haraka kwa kuwa hii ni  dalili ya wazi kabisa kuonesha kuwa mtu yupo hatarini zaidi kupatwa na shambulio la moyo.

Maumivu ya kifua 

Wengi hupitia hali hizi za maumivu ya kifua kwa nyakati tofauti na sababu tofauti kutokana na sababu mbalimbali za kibaiolojia.

Mara nyingi kwa wanaume, dalili hii huashiria hatari ya kupatwa na shamulio la moyo ambapo mwanaume aonapo tu dalili hizi hatakiwi kufumbia macho. Aidha, inaripotiwa ni wanawake watatu tu kati ya wanawake 10 wanaopatwa na maumivu ya kifua wanapata tatizo la shambulio la moyo.

Hivyo, wanaume wapo hatarini zaidi kuliko wanawake kupatwa na shambulio la moyo kupitia dalili hii ya maumivu ya kifua.

15989 Total Views 4 Views Today
||||| 4 I Like It! |||||
Sambaza!