Hayati Kanali Tumaniel Ndetichia Mlay

KANALI TUMANIEL NDETICHIA MLAY

(1942 – 2018)

 

Nilipata mshituko mkubwa na kushikwa na majonzi pale niliposikia katika simu yangu ya kiganja, Kanali Lameck Meena akisema, “Jambo Sir, umesikia habari za kifo cha Kanali Mlay Sir?” Nilimjibu kwa mshangao, “We Meena ati nini? Nani kafariki?” Ndipo Kanali Meena akarejea kuniarifu kuwa Kanali Mlay amefariki dunia usiku, nyumbani kwake Moshi. Hii ilikuwa asubuhi ya Jumatano tarehe 17 Januari hii ya mwaka huu. Nikaendelea kudadisi Ester mkewe anasemaje? Nikajibiwa haongei na simu, analia tu!

 

Kifo cha Kanali Mlay kilinishtua sana. Ni mwezi Desemba tarehe 02, 2017 tulikutana pale Bunyokwa – Segerea nyumbani kwa Mkuu wa JKT Meja Jenerali Michael Isamuhyo kwenye msiba wa Mrs. Loyce Isamuhyo, mke wa CNS. Tuliongea na akaahidi kuja kunitembelea nyumbani kwangu, Uwanja wa Taifa kunijulia hali katika ugonjwa wangu.

Leo, Januari katikati huyu Kanali anafariki! Loo, kweli kazi ya Mungu haina makosa. Kila mmoja wetu amepangiwa siku yake kwenda mbele ya haki. Bwana Mungu asifiwe – Amina.

Mimi nilimjua Kamanda Mlay tangu Novemba 1964 katika Kambi mama la JKT Mgulani. Wakati mimi naingia JKT kama mwalimu, Mlay na wenzake walikuwa ndiyo kwanza wameajiriwa kama viongozi (leaders) katika JKT.

 

Kanali Mlay nimjuavyo alijiunga na JKT pamoja na vijana wenzake wapatao 170. Walijitolea kulitumikia Taifa pale Mgulani. Vijana hawa walikuwa kundi la III kujiunga na JKT tangu lianzishwe tarehe 10.07.1963. Basi hawa walikuwa kundi C katika mikupuo ya kuingia JKT waliitwa “C” Coy. Wengine ninaowakumbuka ni kama Kanali Edmund Mjengwa, Kanali Christopher Daniel Khamsini, Luteni Kanali Francis Sanga, Meja Christopher Charles Mzena, Kapteni Juma Muhombolage, Kapteni Ngitiri Kapango. Wengine nimeshawasahau.

Vijana wa Coy C walijiunga na JKT hapa Mgulani tarehe 17 Januari 1964. Wakafunzwa uaskari na wengine uongozi hata kufikia vyeo nilivyovitaja hapo juu.

Cha maana kwa kundi hili ni kwamba hata kabla hawajaondolewa ushamba wa ukuruta pale Mgulani, siku ya 4 tu ya kuwa kwao kambini ndipo yalitokea yale maasi ya askari wa KAR kule Colito Barracks (Lugalo) tarehe 20 Januari 1964.

Vijana hawa hawakuelewa nini kilitokea na wakashikwa na mfadhaiko wasijue hatima yao katika Jeshi. Kumbe Waingereza wana usemi kuwa yale maasisi ya askari KAR, kwao sasa yalikuwa “a blessing in disguise! Kushitukia hamadi – Rais Nyerere anatangaza – kila kijana wa nchi hii sasa anatakiwa kujiunga na JKT ndio mlango pekee wa ajira! Wao kumbe wamo ndani ya JKT. Haraka haraka wakafunzwa uaskari, na baadhi yao wakafunzwa uongozi na hatimaye wakaajiriwa kama viongozi ndani ya JKT. Hawa wamekuwa mhimili mkubwa wa JKT mpaka kustaafu kwao.

Kanali Mlay na baadhi ya wenzake wakawa wa kwanza kuajiriwa ndani ya JKT mwaka ule 1964 na ajira zao zilianza tarehe 01.10.1964 kwa cheo cha Cadet Guide. Kuanzia siku ile Kanali Mlay amelitumikia JKT kwa uhodari na uaminifu mkubwa sana.

 

Nilimkuta pale Mgulani akiwa mkufunzi wa maaskari – “recruit instructor”.

Kitu kimoja ninakikumbuka mpaka leo ni namna alivyonikosoa mimi nikiwa mgeni kabisa katika JKT Cadet Guide Mlay na mwenzake Cadet Guide Makame Rashid (alipata kuwa Meja Jenerali na Mkuu wa JKT 1989 – 2006) wakanijia ofisini na kunielimisha juu ya hali ya majeshi. Kwanza hawa wawili walinifundisha namna ya kupokea saluti za maamkio. Kamanda Mlay ni kiongozi straight forward ni mkweli na hapendi watu nyoronyoro.

Pili, walinieleza kuwa pale Mgulani hapakuwa shuleni, mahali walimu wanapoita watoto kwa majina yao, Juma, John, Selemani, Ana na kadhalika. Pale ni jeshini nisiwaite kwa majina yao kama vile Makame, Mawazo, Mlay, Mzena, bali wao pale ni viongozi napaswa kuwaita (identify them) kwa vyeo vyao kama vile niwaite Leader Mlay au Cadet Guide Makame. Hili kwangu lilikuwa funzo muhimu sana.Vijana hawa wawili walionesha upendo na heshima kwa ualimu wangu basi walipenda nitumbikie katika ujeshi niende nao pamoja. Nalo nimelikumbuka mara kwa mara – Jeshi siyo shule ni taasisi ya watu wazima na kuna mila na desturi zao lazima zifuatwe.

Kamanda Mlay amekuwa “Instructor” wa likruti Mgulani kwa miaka mingi. Ni kazi aliyoipenda aliijua na aliithamini. Wengi wakimwita kamanda makelele au “a shouter”, lakini alijitokeza kuwa kiongozi hodari katika gwaride na ufundishaji wa silaha (weapon trainer).

“Operation Umoja” wakila kiapo Uwanja wa Taifa 1966

akiwa mmoja wa Makanda Kombania (Coy Commander) ni

aliyesimama mbele ya Coy yake

 

Kanali Mlay amekuwa instructor, siyo Mgulani tu, bali kule Mafinga kama Coy Kamanda, Ruvu na Makutupora. Alipanda vyeo katika JKT hadi kuwa Assistant Master. Ulipofika mwaka 1975 JKT ilipoungana na JWTZ, Rais na Amri Jeshi Mkuu aliwatunuku maafisa wote wa JKT Kamisheni katika JWTZ. Mlay hapo akapewa Na. P2710 na kuwa na cheo cha Kapteni kuanzia Julai Mosi mwaka ule 1975.

Kuanzia hapo Mlay akashika madaraka mbalimbali hata akafikia ukamanda kikosi kule Buhemba mara tu alipotoka vitani Uganda. Na akawa Kamanda kikosi wa Mafinga hadi kustaafu kwake akiwa na cheo cha Ukanali mnamo Juni 30, 1995.

 

Kanali Mlay alikuwa hodari na shupavu katika kazi. Mwaka 1979 nilimkuta akiwa kule Uganda Kaskazini kabisa mpakani na Sudan mahali panaitwa Moyo. Kule alikuwa Det Kamanda.

Kanali Mlay alimuoa Bibi Ester na walibahatika kupata watoto saba; kati yao wakike wakiwa wanne.

Mimi nimeandika haya ili wale aliokaa nao katika Kambi za JKT na wakimwita “afande mkali” wapate taarifa hii nzito na ya kusikitisha ya msiba wa Kamanda wao.

Imani yangu, wengi tutamwombea kwa Mungu, roho yake aipumzishe kwa amani huko mbinguni.

Kanali Mlay alizikwa Jumatatu tarehe 24 Januari kijijini kwake kwa heshima zote za kijeshi. Baadhi ya maafisa wastaafu wenzake wa JKT alikuwa nao Coy C 1964 walipata fursa ya kwenda kumzika kule Moshi.

Ni askari, ni afisa, ni baba wa familia na ni mtu mwenye haiba kubwa katika JKT na amelitumikia Taifa hili kwa uaminifu mkubwa sana. Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina lake libarikiwe. Ayubu 1:21

 

“Requiescat in Pace”

Please follow and like us:
Pin Share