Dar es Salaam ikiweza, Tanzania imeweza

Wiki iliyopita itabaki katika kumbukumbu miongoni mwa Watanzania wengi wa kizazi hiki kutokana na tishio la ugonjwa wa COVID-19 unaotokana na virusi vya corona kusababisha matamko na maelekezo kadhaa kutoka serikalini.

Kwa mara ya kwanza katika miaka ya karibuni Tanzania ililazimika kuungana na mataifa mengine duniani katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu kwa kusitisha kwa siku 30 masomo katika shule na vyuo vyote nchini na kutoa tahadhari kubwa.

Huenda hii ni tahadhari ya kwanza kutolewa na uongozi wa juu serikalini tangu mwaka 1999 pale Serikali ya Awamu ya Tatu ilipotangaza ukimwi kuwa ni janga la taifa, ingawa ni ukweli kuwa hofu iliyopo kwa sasa ni zaidi ya mwaka 1999.

Hofu ya safari hii inaweza kufananishwa na ile ya mwaka 1977/78 wakati ugonjwa wa kipindupindu ulipoingia na kusambaa nchini kwa kasi ya ajabu, kasi ambayo iwapo itakuwa sawa na corona, hali itakuwa mbaya sana.

Kuepuka misongamano ni miongoni mwa tahadhari muhimu katika kuzuia maambukizi ya corona na ndiyo maana serikali ikaamuru kufungwa shule na vyuo nchini, ikishauri wananchi kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima kwa sasa.

Kwa kuwa Dar es Salaam ndio mji wenye idadi kubwa ya watu nchini, kuna umuhimu wa kipekee kwa jiji hilo kuongoza mapambano ya kuzuia kusambaa kwa corona Tanzania, kwa kuchukua tahadhari kubwa zaidi.

Hadi mwishoni mwa wiki, maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kama ndani ya vyombo vya usafiri wa umma (daladala na mwendokasi), Kariakoo, Kivukoni na masoko mengine ya Dar es Salaam shughuli ziliendelea kama kawaida.

Bila shaka ni mapema kwa Dar es Salaam kufanya kile wenzetu wanachokiita ‘total lockdown’, lakini ni wakati muafaka wa kupunguza hata kwa lazima msongamano hasa kwenye usafiri wa umma kama Wizara ya Uchukuzi ilivyoelekeza.

Serikali inaweza kwa kipindi hiki kuruhusu ‘Coaster’ zinazoegeshwa zikisubiri kukodiwa sasa kusafirisha abiria ndani ya jiji; Coaster hizo na daladala ziruhusiwe kufika katikati ya jiji kupitia Barabara ya Morogoro na kupunguza msongamano BRT.

Lakini pia kwa abiria wenye uwezo kwa namna fulani nao waruhusiwe kutumia Bajaj kuingia maeneo ya katikati ya jiji. Hawa watapunguza watu wanaolazimika kurundikana kwenye daladala na mwendokasi.

Hatua hizi kama zitafanyika ndani ya siku 21 katika Jiji la Dar es Salaam huku tahadhari za kawaida zikiendelea mikoani, hali inaweza kudhibitiwa, hivyo watoto na wanafunzi wa vyuo nchini kurejea masomoni katika tarehe iliyopangwa.