Wiki iliyopita Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango, aliwasilisha kwa wabunge mapendekezo ya serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na kiwango cha ukomo wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2020/21.

Katika wasilisho lake, Dk. Mpango alieleza kuwa kwa mwaka ujao wa fedha serikali inapanga kukusanya na kutumia Sh trilioni 34.879, ikiwa ni ongezeko la kama Sh trilioni 1.7 kutoka bajeti ya mwaka huu ya Sh trilioni 33.1.

Kwa kiasi kikubwa bajeti hiyo ya mwaka ujao itapata fedha kutokana na makusanyo ya kodi, yanayokadiriwa kufikia Sh trilioni 20.325 huku misaada na mikopo ikiipatia serikali Sh trilioni 7.939.

Kutokana na kuyumba kwa hali ya uchumi duniani kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuibuka kwa virusi vya corona, kuna uwezekano mkubwa kiasi ambacho serikali inakitarajia kama misaada na mikopo kikapungua.

Hilo linamaanisha kuwa kwa kiasi kikubwa makusanyo ya ndani yanatarajiwa kuendelea kuhimili utekelezaji wa bajeti kwa kiasi kikubwa.

Kwa maana hiyo, tunadhani serikali inapaswa kuchukua hatua ambazo zitaiwezesha kuongeza makusanyo kutoka vyanzo vya ndani na hilo lina faida kadhaa kubwa.

Kwanza, ongezeko la makusanyo ya ndani litamaanisha ongezeko la shughuli za kiuchumi ndani ya nchi, na hili litawezesha kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi mkubwa wa taifa. Pili, ongezeko la shughuli za kiuchumi ndani ya nchi kutaongeza kiasi cha taifa kugharamia miradi mikubwa. Tatu, kukua huko kwa shughuli za uchumi kutaongeza ajira kwa Watanzania. Nne na kubwa zaidi, kukua kwa shughuli za uchumi ndani ya nchi kutaihakikishia nchi uwezo wa kuhudumia bajeti yake bila kutegemea mapato kutoka nje ya nchi au kutegemea kwa kiasi kidogo sana.

Ndiyo maana tungependa kuihimiza serikali kuhakikisha kuwa inaweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi kuimarika. Kukua kwa sekta binafsi ndiko ambako kutaongeza shughuli za kiuchumi nchini.

Kwa upande mwingine, kwa kuwa asilimia kubwa ya Watanzania hutegemea kilimo, inafaa serikali kuiangalia sekta hiyo kwa karibu na kuhakikisha inapatiwa kila kinachohitajika ili ikue.

Kukua kwa sekta ya kilimo, pamoja na kutoa ajira kwa watu wengi lakini pia kutaongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kupunguza urari wa biashara uliopo hivi sasa kutokana na kuagiza zaidi kuliko kuuza nje zaidi.

Nia ya serikali kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu, pia uboreshaji wa  mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji, ikitekelezwa kwa vitendo, tutafanikiwa kugharamia bajeti ijayo bila matatizo makubwa.

By Jamhuri