Moja ya mijadala iliyotawala kwenye mitandao ya kijamii wiki iliyopita ni hatua ya Rais Dk. John Magufuli kuwaalika Ikulu baadhi ya viongozi wa upinzani na kufanya nao mazungumzo. 

Ukiacha mazungumzo hayo, mvuto pia ulikuwa katika picha za video zilizosambazwa na Ikulu zikionyesha Magufuli akisalimiana au kuagana na viongozi hao kwa mtindo wa kutoshikana mikono, wakipigisha miguu tu.

Kabla ya hapo tuliona picha za Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akisalimiana na viongozi wengine bila kupeana mikono. Viongozi hawa walifanya hivi kama moja ya mambo ambayo watu wanapaswa kuyafanya ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Wengi walijadili matukio haya kama mambo ya ajabu, lakini ukweli ni kuwa viongozi hawa wameonyesha mfano mzuri ambao unapaswa kuigwa na watu wengine.

Ipo tabia imejengeka miongoni mwa Watanzania kuwa katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko kazi kubwa inapaswa kufanywa na serikali. Ni kweli, lakini huo si ukweli kamili. Wakati serikali ikifanya yale yanayopaswa kufanywa nayo, wananchi nao wanapaswa kukumbuka kuwa wana wajibu katika mapambano dhidi ya maambukizi hayo.

Katika suala la corona mathalani, wakati serikali ikiandaa vifaa na wataalamu kwa ajili ya kukabili maambukizi iwapo yatajitokeza, ni kwa kiasi gani wananchi wa kawaida wanafanya yale ambayo yanapawa kufanywa nao kama njia ya kudhibiti maambukizi hayo?

Mathalani, tangu Waziri wa Afya atangaze njia za kujikinga dhidi ya maambukizi ya corona ambazo zinahusisha kutoshikana mikono na tukawaona viongozi wetu wakuu wakiongoza katika hilo, wananchi kwa upande wao wamefanya nini kutekeleza hilo?

Mpaka leo hii bado watu wanaona suala la kusalimiana kwa kupigisha miguu kuwa kama kitendo cha ajabu. Hakuna ambaye anaonekana kukitekeleza zaidi ya kufanywa kama utani na baadhi ya watu.

Tunadhani kwamba kwa kuwa utamaduni wa kusalimiana kwa kushikana mikono ni jambo ambalo limeshamiri sana katika jamii zetu, kipindi hiki kingetumiwa na watu kufanya ‘mazoezi’ ya kusalimiana bila kushikana mikono, ili iwapo itatokea kuwa tunalazimika kufanya hivyo kwa sababu corona imeingia, basi tusipate tabu kuzoea.

Hii ni moja ya mambo ambayo wananchi wa kawaida wanapaswa kuyafanya kama mchango wao katika kukabiliana na kusambaa kwa kasi kwa virusi vya corona, lakini wengi hatuonekani kulitilia suala hili maanani, ndiyo maana hivi leo akionekana mtu amevaa kiziba pua na mdomo akikatiza mitaani watu wanamshangaa badala ya kumuiga.

1277 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!