Zimepita wiki kadhaa sasa tangu ziwepo taarifa za mafuriko makubwa kuvikumba baadhi ya vijiji katika Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi. Ukiacha watu 14 ambao waliripotiwa kufariki dunia, watu wengine zaidi ya 15,000 waliathiriwa na mafuriko hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, amenukuliwa akieleza kuwa maelfu ya wakazi wa vijiji hivyo wameachwa bila makazi huku vyakula vyao majumbani vikisombwa na maji na mashamba yakiharibiwa, hivyo kuwafanya wasiwe na uhakika wa chakula kwa muda mrefu ujao.

Kwa kuwa vitu vyote vya watu hawa vimesombwa au kuharibiwa na maji ya mafuriko, ni dhahiri kuwa wanalazimika kuishi kwa kusaidiwa na watu na taasisi nyingine katika kipindi hiki cha mpito kwao. Misaada kutoka kwa watu wengine ndiyo itawawezesha kuvuka kipindi hiki kigumu.

Lakini cha kusikitisha ni kuwa tangu taarifa hizo zitolewe hatujasikia jinsi ambavyo wananchi hao wamepatiwa misaada. Inakuwa kama wameachwa yatima, wakilazimika kujihudumia wenyewe katika mazingira magumu sana.

Upo uwezekano kuwa watu na taasisi nyingi zimeogopa kuwasaidia watu hao kwa kufuata kauli ya serikali hivi karibuni kuwa haitajihusisha kuwasaidia watu walioathiriwa na mafuriko kama watakuwa wamejenga makazi yao katika maeneo ya mabondeni.

Kama ni hivyo, itakuwa vema Watanzania wakaliangalia suala hili upya kwa sababu wananchi hawa wa Kilwa hawakujenga mabondeni. Wameishi katika vijiji hivyo kwa miaka mingi bila athari zozote. 

Mafuriko yaliyowakumba mwaka huu yanatokana na mvua kuongezeka kwa kiasi kikubwa. Hivyo si sahihi kuwachukulia kuwa wameyafuata mafuriko hayo kwa kujenga mabondeni.

Kinachoshangaza ni kuwa kwa muda mrefu sana Watanzania tumekuwa na moyo wa kusaidiana katika taabu na raha, hasa katika majanga ya aina hii. Kamwe hatukuwahi kutupana katika kipindi kigumu kama hiki kinachowakabili wenzetu wa Kilwa.

Kwa hakika bado hatujachelewa kuwasaidia watu hawa. Ni wakati muafaka sasa kwa watu wengine na taasisi kuangalia namna ya kuwasaidia Watanzania wenzetu ambao wameathirika kutokana na majanga ya asili.

Tukumbuke kuwa wananchi wa Kilwa hawakujitakia majanga haya. Kwa kiasi kikubwa kilichowakumba kilikuwa juu ya uwezo wao kukidhibiti.

Kwa upande mwingine, kwa kusisitiza kile kilichosemwa na serikali kuhusu kuishi mabondeni, tungependa kuwasihi Watanzania wenzetu ambao wamejenga na wanaishi katika maeneo ya mabondeni kuondoka haraka wakati huu ambapo sehemu kadhaa za nchi zinatarajiwa kuanza kupokea mvua za masika.

9437 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!