Hivi karibuni Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja, amefanya mahojiano na kipindi cha MIZANI cha Televisheni ya Taifa (TBC1). Katika kipindi hicho anazungumza masuala mengi kuhusu upatikanaji wa huduma ya majisafi na majitaka jijini Dar es Salaam pamoja na maeneo mengine ambayo DAWASA inatoa huduma. 

Hapa chini fuatilia maelezo yake neno kwa neno katika mahojiano hayo ya TBC1. Endelea…

Kwa mwaka 2020 tumejipanga na tunakwenda kumkabidhi mwenye duka thamani ya duka lake. Tumeweza kufikia asilimia 85 ya malengo ya Ilani ya Uchaguzi 2015-2020. Tuna miradi kadhaa ambayo tutafikia lengo la asilimia 90.

Wananchi wa Dar na Pwani wanapata maji kwa asilimia 88, hadi Desemba mwaka jana, DAWASA tumepunguza magonjwa ya mlipuko jijini Dar es Salaam.

Rais wa Awamu ya Kwanza Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ndiye aliyezindua mtambo wa maji wa Ruvu mwaka 1972. 

Aidha, ndiye aliyezindua mtambo wa Ruvu Chini na Ruvu Juu mwaka 1976. Miaka ya karibuni tumeboresha. Mwaka 2020 tunaanza kujenga mtambo mpya kuzalisha maji lita za ujazo milioni 750,

kutoka Rufiji hadi Kisarawe ambapo kutakuwa na tanki kubwa. 

Mei mwaka huu tutampata mhandisi mshauri. Kuna vitu viwili ambavyo tumeomba kwa mhandisi mshauri wa mradi. Mtambo huo unajengwa na fedha za ndani za DAWASA. Wazo la mpango wa Rufiji, mwaka 2030 Dar es Salaam itakuwa na watu milioni kumi na mahitaji ya maji yatakuwa zaidi ya lita bilioni moja kwa siku. 

Majitaka

Katika kuhakikisha kwamba tunashughulikia majitaka, DAWASA inajenga mabwawa ya majitaka Buguruni na Airwing, lengo likiwa ni kuboresha huduma hiyo.

Tumenunua magari ya kubeba majitaka na tunaanza kuwaratibu hao wenye malori ya majitaka. Buguruni tutajenga mtambo wa majitaka. Kurasini pia tunajenga kwa fedha za Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Mbezi Beach, mradi unafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).

Viwanda

DAWASA imejikita zaidi katika Mkoa wa Pwani; Mkuranga, Chalinze Mboga Kiwanda cha Sayona, tunapeleka huduma Tan Choice na tumejikita kwenye kushamirisha Tanzania ya viwanda.

Miradi

Kuna mradi unaoendelea kutoka Kisarawe mpaka Banana, mwingine unaendelea kutoka Mkuranga hadi Vikindu, Mwanambaya. Kuna mradi unaendelea kutoka Mlandizi, Chalinze mpaka Mboga lakini pia mradi huu utapeleka maji Ubena Zomozi, na njia panda ya kwenda Morogoro Vijijini.

Pia kumekuwa na mradi ambao umekuwa ukisumbua sana, mradi wa Kimbiji – Kigamboni nao umekwisha kuanza, sasa wananchi wote wa pembezoni mtaona tunavyowaingiza kwenye hiyo miradi. 

Kuna mradi mwingine wenye thamani ya Sh bilioni 77, huu tumepata mkopo wa gharama nafuu kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya maeneo ya Mivumoni, Madale, Goba, Bunju mpaka Bagamoyo nao umekwisha kuanza. Kwa hiyo maeneo yote ya pembezoni tayari yameingizwa katika miradi hiyo inayoendelea kutekelezwa. 

Ukiondoa mradi huu wa Benki ya Dunia, miradi mingine itakamilika kabla ya Juni mwaka 2020. Kwa hiyo wananchi wa Gongolamboto, watuvumilie tu na kazi imekwisha kuanza, ni suala la muda tu.

Miundombinu kwenye Jiji la Dar es Salaam

Tumefanya awareness kubwa na tunawatumia sana wenyeviti wa Serikali za Mitaa, kwa hiyo tumeanza kuelewana, zamani ilikuwa ni tabu kutaka kupitisha mabomba mpaka mtu alikuwa anaomba fidia alipwe kwanza, wengine wanazuia, lakini sasa hivi hiyo changamoto haipo tena. 

Kwa mfano, hivi karibuni tumepeleka maji katika kiwanda cha nyama cha Tan Choice kule Kibaha, ni kiwanda kikubwa sana ambacho kitakuwa kinachinja ng’ombe 1,000 kwa siku na kuchinja mbuzi 4,000 kwa siku. 

Kwa hiyo, pale sisi kama nchi tutapata fedha nyingi sana kwa maana ya kodi, lakini pia kitatoa ajira nyingi, lakini wananchi walikuwa wamezuia bomba lisilazwe kwa urefu wa kilometa mbili wakitaka fidia, tukawashirikisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo na mkuu wa wilaya, tatizo hilo limeondoka.

Kwa hiyo, jambo hilo kwetu si kubwa kutokana na ukweli kwamba wananchi wamehamasika kuiunga mkono serikali, kwa hiyo vitu kama vile vya maendeleo, mkikaa mezani na wakaelewa changamoto zinakwisha.

Maeneo mapya ya Mkuranga, Kisarawe  

Niishukuru sana serikali, hasa Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli pamoja na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, imeanza kupanua eneo la DAWASA. Kwa sasa tunafanya kazi Mkuranga, Mwanambaya mpaka Vikindu, lakini pia tumepewa eneo la Wilaya ya Kisarawe. 

Kisarawe ni mji mkongwe, lakini haujawahi kupata maji. Kisarawe na Jiji la Nairobi zina umri mmoja lakini Nairobi sasa hivi maji yanapatikana kwa asilimia zaidi ya 80, wakati upatikanaji wa maji Kisarawe ulikuwa chini ya asilimia 30. 

Tumefanikiwa na tayari tumepeleka mradi wa maji wa Sh bilioni 10, na mradi umekamilika, tumetoa maji Kibamba mpaka Kisarawe na sasa hivi ninavyoongea wananchi wanapata maji. Nitumie fursa hii kumshukuru sana Mbunge wa Kisarawe, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jaffo. 

Yeye amekuja na kampeni nyingine ya kuunganisha maji nyumba kwa nyumba na ametoa target kwa wenyeviti wa Serikali za Mitaa kwamba atatoa bonus kama nyumba zote zitapata maji, kwa hiyo Kisarawe nyumba zote kabla ya mwezi Mei zitakuwa zimepata maji kwa sababu ya motivation ya mbunge. 

Mpango wa Mheshimiwa Rais Dk. Magufuli ni kuhakikisha serikali inamtua mama ndoo kichwani, sisi DAWASA tunamuunga mkono rais kwa nguvu kubwa sana. Moja ni kwamba tumeondoa utaratibu wa wateja kulipia pesa kwanza, halafu ndiyo wapate huduma ya maji kwa maana ya maunganisho ya kwanza. 

Hiyo sisi tumeifuta kwa Dar es Salaam na Pwani, mwananchi anakuja ofisini anajaza fomu anapigiwa hesabu na ile gharama ya maunganisho anailipa katika kipindi cha mwaka mmoja, sasa kwa sababu Kisarawe ni eneo la mfano na ni mradi wa kwanza ambao umetekelezwa na DAWASA kwa fedha zake za ndani na ni mradi ambao umechukua dhana ya Mheshimiwa Rais Dk. Magufuli kwamba tujitegemee, kwa hiyo kwa Kisarawe tumetoa bonus kwamba kwa wananchi wa Kisarawe wataunganishiwa maji kwa mkopo wa miaka miwili, hii ni sawa na bure. 

Tunataka sasa wananchi wajitokeze kuunganishiwa maji, hatutaki mwananchi yeyote kwenda kuomba maji kwa jirani, tunatamani kuona kila mwananchi wa Kisarawe anakuwa na maji nyumbani kwake. Hiyo ndiyo maana halisi ya kumtua mama ndoo kichwani.

Tumeunda mikoa mipya, sasa hivi DAWASA ina mikoa 14 rasmi, tumeunda Mkoa wa Kigamboni, hiyo maana yake ni kwamba tunataka wananchi wote Kigamboni, Mjimpya, Mjimwema mpaka Kongowe wapate huduma ya maji. Pale tayari kuna visima vinane vimekamilika, kwa hiyo tuna ofisi pale ambayo inahusika na kuunganisha wateja wa maji, ofisi iko pale Gezaulole. 

Mradi ambao umeshaanza ni mradi wa Sh bilioni 10, ambao kimsingi unakwenda kuunganisha visima vyote vinane ambavyo vina uwezo wa kutoa maji lita za ujazo milioni 40 kwa siku. Kwa hiyo tunaamini kwamba wananchi wote wa Kigamboni watapata maji na mradi huo unakamilika Desemba mwaka huu. Tumeusaini hivi karibuni pale kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni mbele ya Mbunge wa Kigamboni.

Kama nilivyotangulia kusema, tumeanzisha mkoa mpya wa Mkuranga, mkoa huu utahudumia wananchi wa Mkuranga hadi Vikindu, kwa hiyo ni corridor yote kuanzia Mkuranga, Mwanambaya hadi Vikindu. 

Mkuranga mradi unaendelea na umefikia asilimia 97 ya distribution (usambazaji), uko asilimia 35 kwa maana ya kujenga tanki pamoja na vile visima vitatu vya Mpera. Kwa hiyo kwa ratiba tuliyonayo huu mradi utakamilika kwa asilimia 100 Mei, mwaka huu. 

Baada ya kukamilika hapa pia tutaanza mkakati wa kusambaza maji house to house (nyumba kwa nyumba) kwa wananchi, ambako pia tutatoa promotion kwa wananchi. 

Tumefungua mkoa mpya wa Ukonga kwa ajili ya watu wa Ukonga, Pugu, hili eneo lote halikuwahi kupata maji tangu Tanzania iumbwe, hili eneo tunaliita Dar es Salaam Kusini, hili ni eneo ambalo lilikuwa linakumbwa sana na ugonjwa wa kipindupindu. 

Huko walikuwa na visima vifupi ambavyo maji hayakuwa yanatibiwa, hayakuwa maji salama. Kwa hiyo tumefungua mkoa pale Ukonga. 

Lakini pia tumefungua mkoa Kisarawe kwa ajili ya wananchi wa Kisarawe na wananchi wa maeneo ya jirani, tumeanzisha mikoa hiyo ili iweze kusaidia kutoa huduma, lakini tuko mbioni kufungua mkoa mwingine Chalinze.

Makusanyo na gawio

Ninawashukuru sana wananchi wa Dar es Salaam na Pwani kwa mwaka 2019, maana tumeweza kukusanya takriban Sh bilioni 140, ambazo ni sawa na Sh bilioni 11.6 kila mwezi. Tumefikia malengo ya makusanyo kwa zaidi ya asilimia 90. 

Mimi nimekuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA kwa miaka miwili sasa, kabla ya hapo nilikuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO, kwa kweli efficiency (ufanisi)ni kubwa. Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipowashukuru wananchi wa Jiji la Dar es Salaam. Makusanyo hayo yalitusaidia kutoa gawio la Sh bilioni 1.4 kwa Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli. 

Kwa kweli niwaombe sana wananchi wote wanaotumia huduma yetu ya maji mwaka huu wasituache.

Ajira na upotevu wa maji

Tumechangia sana kuleta ajira kwa vijana kupitia miradi tunayoitekeleza, mwaka 2018 wakati DAWASA na DAWASCO zinaungana, jumla zilikuwa na wafanyakazi 1,100 lakini sasa hivi unazungumzia DAWASA yenye wafanyakazi 2,089 wenye ajira mbalimbali. 

Kwa sababu tunatekeleza miradi mingi kwa kupitia fedha zetu za ndani kupitia force account, tuna vibarua zaidi ya 700, Mkuranga tumetoa ajira kwa vijana kama 300 na hapa katikati ya mji (Dar es Salaam) kama 400 hivi. Japokuwa kuna changamoto za hapa na pale lakini vijana wanashukuru. 

Suala la upotevu wa maji, kuna changamoto ya upotevu wa maji, ni changamoto ambayo kwa mamlaka kubwa kama DAWASA au Mamlaka ya Maji ya Jiji la Nairobi au Uganda National Water (Mamlaka ya Maji Uganda) wanapitia changamoto kama hizi, ni kwamba mtandao ni mkubwa hivyo lazima itokee leakage (uvujaji), kwa hiyo upotevu unasumbua. 

Katika mwaka wa fedha wa 2018/2019, Mheshimiwa Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa alisoma bungeni kwamba upotevu wa maji ni asilimia 44, lakini mpaka juzi Januari hii na Desemba mwaka jana tumeripoti upotevu wa maji kwa asilimia 37, kwa hiyo unazidi kupungua. 

Changamoto kubwa nyingine ni ile ya teknolojia, tunatumia teknolojia ya zamani sana, sababu maji yanatembea maeneo mengi, sasa inabidi utumie simu ufanye patrol ambayo ni mambo ya kizamani.

Sasa tumeamua kuchukua teknolojia na tumetumia uwezo wa ndani, tumewaomba wenzetu wa Chuo cha DIT, wao wana teknolojia ambazo tutazifunga na zitakuwa zina-control (zinadhibiti) kwa signal ili tuone eneo ambalo maji yanapotea.

Siri ya mafanikio

 Kwanza, ninaishukuru serikali chini ya Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli, alitoa maelekezo kwamba DAWASA na DAWASCO zikiungana zinakuwa na nguvu ya pamoja, lakini pia Waziri wa Maji pamoja na Katibu Mkuu wakalisimamia vizuri. 

Mwaka 2018 zikaungana, na moja ya mafanikio makubwa ni kuwa na timu moja hata matumizi ya pesa, mkipata pesa mnatumia pamoja. 

Tumetengeneza timu ya pamoja; pili, jambo hili limeongeza mapato yetu. Makusanyo yameongezeka na mapato 2018/2019 yamepanda na katika hilo tumekuja na utaratibu wa kutumia mapato yetu ya ndani kusukuma hili gurudumu. 

Tumekuwa na uwezo wa kujiendesha na kufanya miradi ya kimkakati, umekuwa mkubwa, kwa hiyo maana yake ni kwamba tumeweza kuwafikia wananchi wengi. Mpango wetu wa baadaye ni kuhakikisha tunakamilisha miradi yote ambayo imeanza, kuna mradi kama ule wa Mkuranga, Kimbiji na Kigamboni ikamilike ili tuepukane na kadhia ya upungufu wa maji. 

Mwaka ujao wa 2021 tutawekeza nguvu zetu nyingi katika kujenga mtambo pale kwenye mradi wa bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere.

By Jamhuri