Katika mabishano kuhusu ni wapi panafaa kuwa makao makuu ya Wilaya ya Bukoba Vijijini, zipo hoja mbalimbali. Lakini ipo moja iliyo kuu ya kwa nini wananchi wa Bukoba Vijijini wanapendelea makao makuu ya wilaya yao yawe katika eneo la Ikimba. 

Kwa ufupi ni kwamba eneo hilo liliitwa Ikimba kutokana na ziwa lililoko ndani ya eneo hilo linaloitwa Ziwa Ikimba, ambalo ni tunu iliyowekwa na Mwenyezi Mungu.

Bila shaka hakuna mtu yeyote aliyehangaika kufanya kampeni ya ziwa hilo kuwa mahali lilipo. Ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu tu. Kinachofuatia ni ubishi wa pengine, kutaka kupingana na mipango ya Mungu. Kama ambavyo nimeishaelezea eneo kwenye maandishi yaliyotangulia haya, eneo hilo limejitenga na kuonyesha jinsi Mungu alivyofanya makusudio yake na kuyaonyesha wazi.

Amelitenga eneo hilo na maeneo mengine kwa kulizungushia bonde maarufu lijulikanalo kama bonde la Mto Ngono.

Yaani Mungu ametenga moja kwa moja na kuifanya sehemu hiyo iwe wilaya inayojitoshe leza, tunaweza kuiita wilaya ya Ikimba. 

Hicho ni kitu ambacho hakikupaswa kuwahangaisha viongozi wa kisiasa kwa kutafuta mahali pengine ambako makao makuu ya wilaya hiyo ingetakiwa kuwa. Moja kwa moja hiyo ilipaswa kuwa wilaya ya Ikimba. Huo ni mpango ambao tayari Mungu alikwisha kuweka mkono wake.

Lakini kutokana na idadi ya wananchi kuwa ndogo wakati tunapata uhuru, ilionekana eneo hilo liunganishwe na maeneo mengine na kutengeneza eneo kubwa linalofaa kuwa Wilaya ya Bukoba Vijijini. Hii ni kwa sababu kigezo cha eneo kuwa wilaya si tu kuwa kubwa kijiografia, bali pia idadi ya watu waliopo katika eneo hilo. Ndiyo maana kuna maeneo makubwa sana ambayo hayajawa wilaya hadi leo, kwa sababu hayana idadi ya kutosha ya watu.

Kwa hiyo, kufikia mahali tulipo kwa wakati huu, baada ya zaidi ya miaka 50 ya Uhuru, eneo la Ikimba limekua sana kiasi cha kuhitaji kuwa wilaya inayojitegemea. Kama nilivyosema awali, mazingira ya eneo hilo yamejitengeneza yenyewe bila ya mtu yeyote kuonekana amefanya figisu. Mtu anayeelekea eneo hilo anajiona kuwa ameingia katika eneo fofauti na sehemu nyingine ya Bukoba Vijijini, baada ya kuvuka bonde hilo katika daraja la Kalebe akitokea Bukoba Mjini.

Yapo pia maeneo mengine ambayo nayo  yanaweza kupitika kuingia eneo la Ikimba lakini vilevile yakionyesha kwamba mtu anaingia kwenye eneo tofauti na maeneo yaliyosalia. Upande wa mashariki na kaskazini limezungukwa na bonde la Mto Ngono, wakati upande wa magharibi likiwa na uwazi unaopakana na Wilaya ya Karagwe wakati kusini kuna mwinuko mkubwa unaotengeneza sehemu ya Muleba Kaskazini au Kihanja.

Ni jambo la kushangaza kuona watu wa sehemu za mbali kama Bumai, Rubafu katika Tarafa ya Bugabo wanachanganywa na watu wa Izimbya, Kibirizi, Kamuli na Rukoma sehemu ambazo ni kama ziko mikoa miwili tofauti.

Hicho ni kitu kinacholifanya eneo hilo la Ikimba kuwa gumu kuunganishwa na sehemu nyingine kutengeneza wilaya moja.

Mwanzoni wakati tunapata uhuru eneo lote liliunganishwa katika Wilaya ya Bukoba Vijijini. Kama nilivyoeleza, hiyo ilitokana na upungufu wa wakazi wa eneo husika. Lakini kwa sasa kutokana na ongezeko la wakazi wa eneo la Ikimba halihitaji tena wakazi wa maeneo mengine kwani idadi ya watu waliopo inajirosheleza kuifanya kuwa wilaya inayojitegemea.

Kitu kingine kinacholifanya eneo hilo lisihitaji tena kuunganishwa na maeneo mengine ni ukweli wa kwamba wakazi wengi wa eneo hilo wamehamia tokea maeneo mengine yaliyotajwa na kupafanya makazi yao ya kudumu hapo.

Watu wametokea maeneo ya Bukoba Mjini, Bugabo, Kiziba, Maruku, Muleba Kaskazini na hata mikoa ya nje kama vile Mwanza, Shinyanga na kwingineko na kuweka makazi yao katika eneo la Ikimba. Idadi hiyo ya wahamihaji ni kubwa kuliko idadi ya wakazi wa asili kwa zaidi ya mara tatu. Hilo ni jambo linalofanya eneo hilo lijitegemee kiwilaya.

Ni kwamba kilichokuwa kivutio kikubwa kwa wahamiaji hao ni urafiki kwa wakulima ambapo mazao mengi yanazalishwa kwa urahisi, hususan ndizi, ambalo ndilo zao maarufu mkoani Kagera. Sote tunajua kuwa chakula cha asili cha Mkoa wa Kagera ni ndizi.

Ndizi limekuwa zao la chakula na biashara kutokana na wananchi wengi Tanzania kupendelea kula ndizi hata ambao si wenyeji wa Bukoba. Mfano ndizi zinazoliwa Tanzania nzima ni tani nyingi kwa siku, ila zinajulikana kama  ndizi za Bukoba ingawa kiuhalisia zinatokea mkoani Mbeya na mikoa mingine!

Suala la ndizi za Bukoba kutokea mkoani Mbeya ni jambo mojawapo linalowafanya wananchi wa Ikimba kuomba wilaya yao. Si kwamba Mbeya kuna ndizi zaidi ya Bukoba, isipokuwa miundombinu inakuwa hafifu sana kiasi cha kuzifanya ndizi zinazolimwa Bukoba hususan maeneo ya Ikimba, zikose kufikishwa sokoni kwa haraka.

Wakati ndizi zinazolimwa Kyela, Mwakaleli, Ipinda na kwingineko zinasafirishwa kwa haraka kupitia barabara za lami kufikishwa Dar es Salaam na mikoa mingine, hali inakuwa tofauti kwa ndizi zinazolimwa Izimbya, Rubale, Katoro na maeneo mengine ya Bukoba Vijijini, achilia mbali Ikimba, kuweza kufikishwa sokoni Bukoba Mjini. Bado hujafikiria jinsi ya kuzisafirisha kuzifikisha Dar es Salaam na mikoa mingine!

Kuna wakati, hasa katika msimu wa mvua, kwa zaidi ya wiki mbili magari yanashindwa kufika eneo linaloitwa Izimbya kutokana na barabara kujaa maji na tope! Ambapo gari lililojaza mikungu ya ndizi likikwama kwa siku mbili tu bidhaa yote iliyomo inageuka takataka, yaani ndizi zilizoiva, ambazo hazifai tena kuliwa, labda kwa wanaotengeneza pombe ya kienyeji!

Lakini ikumbukwe kwamba ndizi zinazosafirishwa kupelekwa sokoni karibu zote ni za chakula, si za kutengeneza pombe.

Huo ni mfano mmojawapo wa kwa nini sehemu ya Ikimba inaomba itengewe wilaya yake inayojitegemea badala kuendelea kuitwa kwa pamoja Bukoba Vijijini.

Uwepo wa wilaya hiyo unaweza kuzifanya ndizi za Bukoba kufikishwa hata Ulaya kama wafanyavyo Waganda na Tanzania kuhesabika kama nchi inayozalisha ndizi kimataifa. Jambo la muhimu ni miundombinu.

[email protected]

0654031701 / 

0784989512

By Jamhuri