Wiki iliyopita katika toleo hili la Uamuzi wa Busara tulisoma jinsi Mwalimu Julius Nyerere alivyofanya uamuzi muhimu 

wa kujiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu wa nchi kwa lengo la kuwapa moyo wananchi. Zaidi alijiuzulu nafasi hiyo ya uongozi ili wananchi wapate kujiamini na wayakubali mabadiliko yaliyokuwa yakitokea. Hata hivyo nchi za nje hazikutambua kwa kina sababu ya uamuzi huo wa Mwalimu Nyerere. Kujua zaidi endelea kusoma tulipoishia…

Kwa hiyo tarehe 22 Januari, 1962 Mwalimu Julius K. Nyerere alitangaza kujiuzulu kwake. Alieleza kwamba siku hiyo alikuwa akiacha kazi yake ya Waziri Mkuu wa Tanganyika. Kabla hajafanya hivyo yeye mwenyewe alikuwa amewateua mawaziri wapya na Rashid Kawawa akiwa mkuu wao.

Kawawa alikubali kuwa waziri mkuu na mawaziri ambao Mwalimu Nyerere aliamini kwamba wangeweza kutimiza wajibu wao wa kuongoza nchi hii. Mwalimu Nyerere aliendelea kueleza kwamba yeye binafsi hangekuwa katika serikali hiyo lakini angeendelea kuiunga mkono akiwa mbunge na Rais wa TANU.

Mwalimu Nyerere aliamua hivyo na kuungwa mkono na wenzake baada ya majadiliano marefu yaliyoendelea kwa siku nyingi, kwa sababu ya imani yake kwamba hiyo ndiyo ilikuwa njia bora zaidi ya kufikia lengo letu jipya la kujenga nchi ambayo watu wote wanashiriki kwa uthabiti katika vita ya kuondoa umaskini, ujinga na magonjwa.

Kufikia lengo hili ilikuwa ni lazima kuwa na serikali nzuri iliyochaguliwa na kuungwa mkono na watu. Hili lilikuwa limekwisha kupatikana na lingeendelea kuwapo.

Ilikuwa pia lazima kuwa na chama cha siasa kilicho imara ambacho kingefanya kazi katika kila kijiji, kikiwa kama barabara yenye njia mbili ya nyakati zote, ambayo ingewezesha madhumuni, mipango na matatizo ya serikali kusafiri mpaka kuwafikia watu. Wakati huo huo mawazo, matakwa na shida za watu kusafiri moja kwa moja mpaka kwa serikali. Hii ilikuwa ni kazi ya TANU mpya.

Mwalimu Nyerere aliamini kwamba madhumuni hayo mawili ya Tanganyika yangeweza kufanikiwa kwa kutekelezwa na serikali yenye mawaziri wenye uwezo ambao alikuwa na imani nao.

Yeye binafsi akatumia wakati wake wote katika kazi za TANU. Kutokana na njia hizi ushirikiano kati ya serikali na chama ungeweza kuimarishwa na madhumuni na matakwa yao yangeweza kutekelezwa kwa ufasaha na haraka zaidi.

Mwalimu Nyerere alizidi kueleza kwamba uamuzi huo ungewashangaza wengi. Lakini hiyo ingetokea kwa ajili ya tabia. Ni tabia vilevile ambayo ingewafanya wengi kuelewa vibaya umuhimu wa hatua hiyo.

Inafahamika kwamba si kawaida kwa waziri mkuu kuacha kazi yake kama kiongozi wa serikali na kwenda kukiongoza chama ambacho kinaiunga mkono serikali mpya.

Lakini Mwalimu Nyerere alisema kuwa hatuamini kwamba ni lazima kufuata mifano ya nchi, alisema kuwa hatuamini kwamba ni lazima kufuata mifano ya nchi nyingine, tunaamini kwamba lazima tutafute mtindo wetu wa demokrasia na kwamba hatua aliyokuwa ameichukua siku hiyo ndiyo ilikuwa njia bora kwetu kuendelea kwa wakati huo.

Kwa hiyo, ilikuwa ni kwa imani kubwa katika serikali mpya na watu wa Tanganyika ambayo ilimfanya Mwalimu Nyerere aamue kushika kazi ya kushiriki katika kuijenga TANU mpya, TANU ambayo ingelilingana na hali ya Tanganyika huru.

Mwalimu Nyerere alimtaka kila raia wa Tanganyika kushiriki katika vita ya kujenga maisha bora. Pia aliwataka watu wote kutoka nchi za nje waliokuwa wakishiriki katika kazi hiyo kutokana na kazi zao katika utumishi wa serikali na mahali pengine, kuendelea na kazi zao katika utumishi wa serikali na mahali pengine, kuendelea na utumishi wao kama zamani chini ya serikali mpya.

Alizidi kuwaomba marafiki zetu walioko ng’ambo kuelewa mabadiliko hayo na kutojaribu kufikiria madhumuni mengine ambayo hayakuwamo. Mabadiliko hayo yalikuwa na maana moja tu. Nia ya kujenga nchi ya kidemokrasia ambayo watu wote wangeweza kushiriki kikweli kweli katika kujenga nchi yao. Alimalizia kwa kusema kwamba tulikuwa tunaendelea mbele kama hapo awali katika umoja wetu na kwa furaha nyingi kwa nafasi tuliyokuwa nayo mbele yetu, “UHURU NA KAZI,” ikiwa ngao yetu.

By Jamhuri