Kituo cha Mafunzo ya Ujasiriamali Tanzania kilichopo jijini Dar es Salaam, kimeingia katika kashfa ya kuwatapeli wajasiriamali walioshiriki katika semina  za ufugaji kwa kuwapa ahadi hewa.

Taarifa zilizoifikia JAMHURI zinasema awali kituo hicho kilikuwa kikitoa semina za ufugaji kwa wajasiriamali jijini Dar es Salaam na kuahidi kuwawezesha kwa kuwapa vifaranga vya kuku, mbuzi, ng’ombe na samaki, kwa lengo la kuwawezesha kujikwamua kupitia ufugaji.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari, kulikuwa na viwango tofauti vya malipo kadiri ya uwezo wa wajasiriamali hao. Kwa mfano, mjasiriamali aliyelipa Sh 20,000 alitakiwa kupewa vifaranga 100 vya kuku, aliyelipa Sh 50,000 aliahidiwa kupewa mbuzi wawili (jike na dume), aliyetoa Sh 150,000 alitakiwa kupewa  ng’ombe na aliyetoa Sh 250,000 alitakiwa kupewa vifaranga vya samaki.

Inaelezwa kwamba washiriki wa semina walikuwa wakipewa vyeti maalum vya ushiriki. Baada ya semina masharti yalikuwa kwamba mshiriki alitakiwa kuandaa mazingira kadiri ya ufugaji anaotaka kufanya.

“Kama unafunga mbuzi au ng’ombe ulitakiwa kuandaa zizi, kama ni kuku unaandaa banda la kuku na kama ni samaki unakuwa na bwawa, baada ya hapo kuna wataalamu waliotakiwa kuja kukagua na baada ya hapo unapewa ulichotakiwa kupewa kadiri ya malipo.

“Cha ajabu ni kwamba hao wakaguzi walikuja wakayaona mazingira yetu na wakaidhinisha kuwa tunatakiwa kupewa hiyo mifugo kwa kuona mabanda yetu, mpaka leo hakuna kinachoendelea, na hii ilikuwa mwaka 2011, mpaka mabanda yameanza kuliwa na mchwa, halafu wakaguzi hawa tulikuwa tunawalipa shilingi 15,000 akija kukagua banda lako,” kimesema chanzo chetu cha habari.

Taarifa zaidi zinasema kuwa baadhi ya wajasiriamali wamekuwa wakijaribu kuwasiliana na mkuu wa kituo hicho ambaye ni mwanamke, lakini wanadai kuwa amekuwa akiwajibu kwa ukarimu wa hali ya juu kwa kuwataka wavute subira.

“Huyu mama amekuwa akitujibu kwa ukarimu sana ila ana visingizio vingi mara vifaranga vilikufa, mara tuvumilie kidogo, hivi kweli tutavumilia mpaka lini? Hebu fikiria tangu 2011 mpaka sasa, hii siyo haki kabisa,” kimesema chanzo cha habari.

Pia inasemekana kwamba mama huyo amekuwa akiwaambia kuwa mradi huo ni wa wanajeshi wastaafu. Mwandishi wa gazeti hili aliwasiliana na mwanamke anayesemekana ni mmiliki wa kituo hicho ili kujua ukweli juu ya shutuma hizo. Mama huyo hakuonesha ushirikiano katika suala hili zaidi ya kutoa vitisho vya hapa na pale.

Yafuatayo ndiyo majibu ya mama huyo kwa mwandishi wa habari hizi kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno (SMS):

“Andika ulivyotumwa tena ktk magazeti yote waliokutuma wakwambie wamekuja matapeli wenzio wengi wakijifanya waandishi na waliokutuma nawajua usicheze na mimi utapata matatizo makubwa andika sina muda wa kukutana  na ww na umetumia  no ya zanteli pia ninalo jina lako nimechukua rb yako.

“Kwa kukusaidia hiyo kazi nimefanya nchi nzima andika tena koma kutumia simu yangu hao jamaa wakiishiwa wanajifanya waandishi andika nawajua wamefilisika mawazo sina ninachoogopa wala sihitaj ushirikiano ila no zako zote nimechukua rb Kanjanja.

“Hao waliokutuma waliwahi kuniletea majambazi yakawataja nawe ni mmoja wao?Andika mi si wa kuchezea.

“Najua ww ni jambazi au matapeli mjini mmoja anakaa maramba mawili mingine tabata juz ulipiga ukimtaka chenge buld  up ur career acha ubabaishaji km wamekufata waambie waite press au studio deal imekuwa dirisha leo siogopi chochote nawajua wote.”

Habari zaidi kuhusu sakata hilo itaendelea toleo lijalo


1505 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!