Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Jumanne Shauri, ametoa uamuzi juu ya mgogoro wa ardhi unaoendelea katika eneo la Pugu Bombani, Dar es Salaam na kuwapa ushindi wafanyabiashara ndogo ndogo.

Mkurugenzi Shauri ameliambia JAMHURI kuwa mgogoro huo tayari wameumaliza na eneo hilo limerudi kwa wafanyabiashara hao, hivyo taratibu za kuwapatia mikataba rasmi waendelee na biashara bila ya kubughudhiwa zinakamilishwa.

Shauri alitoa kauli hiyo Alhamisi wiki iliyopita kutokana na tatizo la mgogoro huo uliokuwa unawahusisha wafanyabiashara zaidi ya 180 wa Kijiji cha Pugu Kajiungeni Bombani.

Hata kabla ya Shauri kufikia uamuzi huo wiki iliyopita, wao walikuwa wamekwisha kuamua kuendelea na biashara zao baada ya kupigwa danadana na mamlaka husika katika kumaliza mgogoro wao na familia ya Kambi Nyamigala iliyohusika kuvunja vibanda vyao vya biashara.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Peter Majura, amesema kero yao kubwa ni mgogoro wa eneo wanalofanyia biashara kati yao na Hamza Kambi Nyamigala anayedaiwa kuwa ni mmiliki halali wa eneo hilo.

Majura amesema eneo hilo kabla ya kuwa wamiliki na kufanya biashara lilikuwa ni la Kampuni ya Amadoli ambao walilinunua kutoka kwa Shomari Mwenye mwaka 1991 kwa lengo la kumwaga mbolea ya kuku iliyokuwa inazalishwa na kampuni hiyo kipindi cha nyuma.

Amesema jirani wa Amadoli aitwaye Matt Lalani alimpokea na kumkaribisha eneo hilo kama mwenyeji wake aendelee na ujenzi wa eneo hilo. 

Uongozi wa serikali ya mtaa ulikaa na kuona matumizi ya Kampuni ya Amadoli yalikuwa si muhimu kuliko mahitaji ya wananchi, uongozi wa kijiji wakiwamo wafanyabiashara, uongozi wa CCM na serikali ya mtaa uliamua kumfuata mmiliki wa Amadoli awakatie vipande vya eneo hilo waligawe kwa  maendeleo ya jamii.

Baada ya kukubaliwa ombi lao, eneo hilo lilikuwa limegawiwa kwa ajili ya kujenga ofisi ya serikali ya mtaa, kata, kiwanja cha mpira, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wafanyabiashara ndogo ndogo wa eneo hilo.

Amadoli aliridhia mwaka 2001 eneo hilo litumike kama ilivyoombwa na serikali ya mtaa na wananchi wa Pugu Bombani. Baada ya hapo walifanya ujenzi wa kudumu na kufanya biashara bila kuwa na shida.

Ilipofika mwaka 2016 Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa na baadhi ya wajumbe wakaanza kukata maeneo katika eneo hilo na kuuzia watu. Tarehe 5/9/2019 mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa aliwaita wafanyabiashara katika Ukumbi wa Vasco, uliopo Pugu kwa lengo la kuwaeleza nia ya kukutana nao tarehe 7/9/2016 katika ukumbi huo huo.

Wafanyabiashara walikataa ombi hilo wakamwandikia barua mwenyekiti kumwomba mkutano ufanyike katika viwanja vya eneo lao Pugu kona.

Terehe 7/7/2017 mwenyekiti alipiga simu kwa Mweka Hazina wa wafanyabiashara hao, Pili Salum, kumtaarifu kwamba mkutano haupo, ameuvunja, hivyo achukue jukumu la  kuwatawanya watu waliokuwepo eneo hilo.

Salum amesema baada ya kuwapatia wananchi taarifa hiyo walikasirika na kuamua kuandamana hadi katika Ofisi za Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa kufahamu kwanini aliwaita halafu akavunja mkutano ghafla, lakini aliikimbia ofisi yake.

“Tukiwa hapo diwani wetu alikuja kujua kwanini tumekwenda katika Ofisi za Serikali ya Mtaa tukamweleza mkasa wote na aliahidi kufuatilia tatizo letu na wananchi wakatawanyika, ikawa salama kwa mwenyekiti huyo,” amesema Majura.

Tarehe 23/10/2016 kulikuwa na kampeni ya Mkuu wa Mkoa ya Dar Mpya, iliyoendeshwa na Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, aliyefika katika eneo hilo akamwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala afuatilie suala la wafanyabiashara hao.

Tarehe 25/10/2016 kiliitishwa kikao na mkurugenzi akiwataka watu wa pande zote kuwepo ila wafanyabiashara ndio pekee waliohudhuria na walalamikiwa hawakuhudhuria. Mkutano ulifanyika katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala ukahusisha wataalamu mbalimbali wa ardhi wa manispaa.

Baada ya kikao hicho, mkurugenzi aliwataka wataalamu wa ardhi na pande zinazopingana wakutane katika ofisi za kata kusikiliza tatizo hilo kwa kina. Upande wa pili haukuhudhuria pia.

Baada ya kikao hicho walikaa kikao kingine wafanyabiashara, mmiliki wa Kampuni ya Amadoli, wazee 15 wa eneo lile na  Mtendaji wa Serikali ya Mtaa,  ndipo ilipogundulika kuwa eneo lile ni la  Kampuni ya Amadoli.

Walikubaliana, na maofisa ardhi walivigawa viwanja hivyo kama ifuatavyo: Kiwanja Na. 50 Ofisi ya Serikali ya Mtaa, Kiwanja Na. 51 Ofisi ya Mtendaji Kata, Kiwanja Na. 49 Ofisi ya CCM, Na. 48 na 47  eneo la  wafanyabiashara na Na. 46 uwanja wa mpira.

Pili Salum amesema tarehe 4/1/2017 nyakati za usiku walishtukia magari ya Polisi na matingatinga wakivamia eneo hilo wakabomoa vibanda vyote na kuteketeza bidhaa zao.

Tarehe 5/1/2017 walikwenda kwa Kamanda Simon Sirro kutoa kilio chao kwamba walivunjiwa bila taarifa. Alichukua maelezo yao na kuahidi kuyashughulikia, lakini hadi leo hawajajibiwa.

Waliandika barua kwenda kwa Mkuu wa Mkoa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, mwanzo wakagonga mwamba, ila baadaye Mwenyekiti Peter Majura, Mweka Hazina, Pili Salum na shangazi wa walalamikiwa, Kesi Kambi Nyamigala, walionana na Lukuvi aliyeagiza Kamishna wa Ardhi kwenda kuchunguza, lakini hakuna kilichotokea.

Waliunda timu ya watu wawili kwenda Dodoma kumuona Mwita Waitara, wakati huo akiwa mbunge wa Jimbo la Ukonga kwa tiketi ya Chadema. Walifika Dodoma, ila Waitara aliwaambia hawezi kuwapeleka kwa Waziri Lukuvi.

“Kwa kweli tuliumia sana kwa kauli hiyo na siwezi kuisahau, kwani alitusaliti wananchi wake kipindi kile tulikuwa na shida na tulifunga safari kwa ajili yake, lakini ametukimbia na kutujibu hawezi, tuliumia sana,” amesema Salum. Walirudi Dar es Salaam kwa lengo la kwenda kumuona Kamishina wa Ardhi wizarani.

Baada ya kuzungushwa walifunga safari tena kwenda Dodoma wakiwa na Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Peter Majura, Bilungo wa  CCM, Nasoro na Pili Salum kwenda kumuona Waziri wa TAMISEMI, Seleman Jaffo. Jaffo aliwaambia wawasiliane na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ila naye wawe wanamkumbushakumbusha.

Walikwenda Ofisi ya Waziri Mkuu wakakutana na Magesa wa Magesa aliyewaambia mezani kwake kuna  nyaraka za kina  Kambi Nyamigala waliokuwa wanagombea eneo.

Magesa aliwaomba watoe nyaraka zao na baada ya kujiridhisha aliamua kupiga simu kwa shangazi wa kina Kambi Nyamigala kujiridhisha kwamba wale watu si wamiliki halali wa eneo lile na akawapatia ahadi ya kuunda Tume Maalumu na kwenda eneo la tukio kuona hali halisi. Hawakupata msaada.

Baadaye wakaenda kumwona mzee Mtulya, Katibu wa Wazee Mkoa wa Dar es Salaam akawapeleka moja kwa moja kwa Makonda kuonana naye. Makonda alimwita RAS wa mkoa na kumwagiza atatue suala lao ndani ya wiki moja.

Salum amesema kuwa baada ya hapo ilikuwa nenda – rudi, wakawa hawapewi majibu, mwisho wakasubiri ziara ya Waziri Lukuvi huko Gongo la Mboto tarehe 17/10/2018. Walipotoa maelezo Lukuvi alimwamuru Afsa Ardhi wa Manispaa ya Iala ajibu hoja yao, aliyesema walivunjiwa kikamosa na kwamba wale wanaogombana nao si eneo lao, wameghushi hati.

Akasema eneo lina viwanja vine, kati ya hivyo viwili vimeshafutwa na viwili bado vinafanyiwa kazi na baada ya hapo Waziri Lukuvi aliahidi kwamba baada ya mwaka mpya angekwenda tena eneo hilo ambapo hakupata nafasi ya kwenda tena.

Diwani wa kata hiyo, Boniventure Mphuru, amesema: “Nilipofika eneo hilo niliwaomba wananchi nikae nao kikao pande zote pamoja na wazee wa eneo husika na nilipowaita walikuja wote isipokuwa upande wa walalamikiwa, familia ya Kambi Nyamigala wanaodai eneo hilo ni lao, mwakilishi kutoka Kampuni ya Amadoli, Petro Stella, alifika; baada ya kikao nikapata picha kwamba eneo ni la Kampuni ya Amadoli.”

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Pugu Bombani, Gido Bernard, amesema limewekwa zuio na kesi ipo mahakamani inayomhusu Hamza Kambi na Kamishna wa Ardhi.

Haji Kambi, mmoja wa wanafamilia ya Kambi Nyamigala amesema eneo lile ni la marehemu baba yao aitwae Salim Kambi Nyamigala, alilinunua shamba hilo mwaka 1946 likiwa na minazi 57 ikiwemo mikorosho, mifenesi na michungwa.

Amesema wakati baba yao mzazi ananunua eneo hilo walikuwa wanaishi Kariakoo, kule shamba walikuwa wameweka vibarua tu.

Amesema tatizo lilikuja baada ya kufariki dunia baba yao mwaka 1988, ambapo kaka yao mkubwa Hamza Kambi, alikuwa amekwenda Ulaya, hakuwepo kwenye msiba wa baba yao kipindi hicho.

Mwaka 1991 wakati kaka yao yupo Ulaya, shangazi zao; Ravia Kambi, Kesi Kambi, Mwatanga Kambi na Ndela Kambi walichukua jukumu la kukata kipande cha eneo la shamba hilo na kumuuzia, Mart Lalani, kwa ajili ya kujenga kituo cha mafuta.

Nyamigala amesema baada ya mauzo hayo shangazi zao waliwataka wachukue kiasi cha pesa baada ya mauzo kama sehemu ya urithi kwa wajukuu ndipo kaka yao mkubwa akapiga simu kutoka Ulaya na kuongea na mmoja wa shangazi zao na Abasi Kambi – kaka yao mdogo, kwamba wasikubali kuchukua pesa yoyote kutoka katika mauzo ya eneo hilo.

Amesema baada ya mauzo walikwenda kwa shangazi yao anayeishi Kariakoo na kuweka kikao cha familia kwa ajili ya ukweli wa eneo hilo.

Nyamigala ameongeza kuwa baada ya sakata hilo shangazi yao wa Kariakoo aliitisha kikao cha familia akawaambia shangazi zao wengine kwamba: “Kula pesa za eneo hilo ni kula moto,” mwishowe alikataa kuchukua pesa zile.

Amesema baada ya mgogoro huo, shangazi zao wakazidi kuwadhulumu hata eneo la nyumba ya Magomeni iliyokuwa ikimilikiwa na shangazi yao Ndela, ndugu wa baba yao mzazi – baba mmoja, mama mmoja na alikuwa hajaacha mtoto kurithi, hivyo wao wakauza eneo hilo na pesa wakala.

Wakati hayo yote yalipokuwa yakiendelea, walishindwa kufungua mirathi na kufanya chochote, kwa sababu kaka yao mkubwa Hamza hakuwapo.

Nyamigala amesema eneo hilo lilibaki muda wote likiwa linakaliwa na mke wa baba yao mdogo, ambapo alipewa eneo hilo aishi kwa muda na shangazi na kaka yao Abasi Kambi kwa sharti  kwamba aishi kwa muda katika eneo hilo, akipata uwezo ahame na kuliacha wazi.

Amesema mama huyo aliishi katika eneo hilo na kuanza kufanya biashara ndogondogo, baadaye aliondoka na kuwaacha baadhi ya wafanyabiashara wakifanya biashara eneo hilo.

Ameongeza kuwa ilipofika mwaka 2000 baada ya mama huyo kuondoka, walionekana wafanyabiashara wengi katika eneo hilo, ndipo serikali ya mtaa ikawaamuru waliokuwa wanafanya biashara katika eneo hilo wajaze mikataba, wakaijaza.

“Tulipoona watu wananufaika na eneo letu, tukaamua na sisi kudai tunufaike na eneo letu kama wenye eneo, ndipo ukaanza mgogoro na wafanyabiashara,” amesema Nyamigala.

Nyamigala ameongeza kuwa baada ya kuona wamekataa kuwapatia haki yao, waliamuru wafanyabiashara waondoke eneo hilo sanjari na kufungua mirathi mwaka 2002.

Ameongeza kuwa kipindi hicho kaka yao mkubwa, Hamza Kambi, alikuwa amerudi kutoka Ulaya, na alipofika walimweka kuwa  msimamizi wa mirathi, hivyo walifanikiwa kufungua  mirathi katika Mahakama ya Mwanzo Temeke.

Amesema mahakama hiyo ilitaka vielelezo vya mali za mirathi ya marehemu, kwa bahati mbaya hati ya eneo la Pugu Kona haikuwepo, bali kwa muda huo ilikuwepo hati ya nyumba na ‘godown’, vyote vipo Temeke.

Amesema kwa kipindi hicho mahakama ilipoona wameshindwa kutoa hati za shamba hilo, waliorodhesha  mali mbili tu na hakimu aliwaomba waende serikali ya mtaa kufuata uthibitisho kama kuna uthibitisho, ambapo kwa kipindi hicho walikosa.

Kwa mshanago, anasema mwaka 2007 wakati wanafanya ukarabati wa nyumba yao, siku moja walisikia harufu mbaya imeenea kwenye nyumba hiyo na walipofuatilia inatoka wapi wakaamua kufumua dali la nyumba kujua kinachojili.

“Tulipofika juu ya dari, ghafla tulikuta mzoga wa paka aliyeukufa, pembeni  tulikuta vitu mbalimbali likiwemo sanduku la mbao, kiti cha kizamani na kitanda, baada ya kufungua sanduku au boksi hilo la mbao tulikuta vitu mbalimbali vikiwemo risiti za ‘godown’, pesa za zamani pamoja na hati ya shamba la Pugu lililonunuliwa mwaka 1946. 

“Baada ya hapo tulitafuta mwanasheria ambaye alitushauri kwamba twende mahakamani tukaingize hilo eneo katika hati ya mirathi, kwa kuwa tayari hati ya eneo hilo ilikuwa imepatikana na bado kisheria haijafika miaka 12,” amesema Kambi.

Kambi amesema waliandika barua kwenda kwa Mkurugenzi, Afisa Ardhi Temeke na Afisa Ardhi Ilala yenye kumbukumbu namba 8420002, iliyoandikwa maneno kwamba hati inatakiwa kubadilika kutoka kwa Salim Kambi kwenda kwa majina ya watoto ambao ndio warithi, baaada ya baba yao kufariki dunia. Ilifanyika hivyo, wakafanikiwa.

Amesema waliambiwa kwenda serikali ya mtaa na kata, wakafanya hivyo, wakaambatanisha hati ya kifo cha baba yao na uthibitisho wa hati ya shamba la Pugu Kona.   

Kambi aliendelea kusema kuwa baada ya hapo walipata kibali cha kuendelea kufuatilia hati ya shamba hilo mpaka wakapata hati ya eneo lao.

Amesema kuwa walipopata hati wakaanza kuandika barua ya kutaka kuendeleza eneo lao, ndipo walipopata kibali cha kuendeleza eneo lao kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala.

Amesema baada ya hapo walimwandikia Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa kwamba wanataka vibanda viondoke waendeleze eneo lao.

Amesema wakati walipokuwa kwenye mchakato wa kuendeleza eneo hilo Mkuu wa Mkoa, Makonda, alitembelea eneo hilo na wananchi waliinuka na kumwambia kero ya eneo hilo, baada ya hapo mkuu huyo wa mkoa alimwinua Afsa Ardhi aliyesema eneo hilo ni la Salim Kambi Nyamigala na kubadilishwa kuwa la Abasi Kambi Nyamigala kama msimamizi wa mirathi baada ya baba yake kufariki dunia.

 Amesema mwenyekiti wa serikali ya mtaa naye baada ya kusimamishwa alithibitisha hivyo, isipokuwa mkurugenzi ndiye alisema yeye ni mgeni atafuatilia.

Amesema baada ya muda mkuu wa mkoa aliwaomba akutane nao katika ofisi yake wakiwa na vielelezo vyao, walipofika katika ofisi hiyo hawakukutana na mkuu wa mkoa, badala yake walikutana na Katibu Tawala wa Mkoa.

Baada ya hapo wakiwa na mwanasheria wao, waliambiwa waache nyaraka zao zifanyiwe kazi. Zilikaa hapo kwa muda wa mwezi mmoja na baada ya hapo walikwenda kuuliza na kuambiwa jalada lao liko masijala ya siri.

 “Tulifuatilia barua hiyo kwenye masijala ya siri tukapewa barua hiyo na tulipoifungua ndani tukakuta imeandikwa kwamba hakuna uthibitisho kwamba Kampuni ya Amadoli ni mmiliki, lakini upande wa Kambi Nyamigala wao wametoa vielelezo,” amesema Nyamigala.

Kambi ameongeza kuwa baada ya taarifa hiyo wakaamua kuandika barua na kwenda kuweka bango kwamba wafanyabiashara wabomoe vibanda vyao waache eneo hilo wazi.

Siku mbili tangu kubomolewa kwa vibanda, Mkuu wa Wilaya ya Ilala aliwaita ofisini kwake na kuwauliza kwanini walivunja vibanda vya wafanyabiashara Pugu Kona, wakamweleza sababu, na baada ya hapo kukawa hakuna majibu, wakafuatilia manispaa ambapo nako kulikuwa hakuna majibu.

Amesema waliamua kufuatilia tena kwa mkuu wa mkoa, na majibu ya mkuu wa mkoa ni kwamba wao walikuwa hawana ardhi na ardhi ni ya manispaa. Walipokwenda manispaa kukawa na danadana za hapa na pale, baadaye manispaa iliwapigia simu na barua ya wito ya kuwataka waende huko.

Amesema barua hiyo iliandikwa kwamba walitakiwa wafike katika ofisi hiyo ya manispaa, ambayo ilikuwa imeunda timu maalumu kwa ajili ya kupata suluhu ya mgogoro huo wakampatia mwanasheria wao. Ilikuwa tarehe 17/5/2017, Arnautoglo badala ya Pugu.

Kambi ameongeza kuwa kamati ile iliwahoji na kutaka watoe vielelezo vyote muhimu. Walifanya hivyo, wakaambiwa kwamba watapewa majibu na watayapata katika ofisi ya mkuu wa mkoa.

“Cha kusikitisha zaidi, tulipofika posta kuangalia barua tukakuta barua inayotutaarifu kufuta viwanja viwili vya eneo letu na alitupatia siku 15 bila ya kutupatia muda wa kujieleza,” amesema Kambi.

Amesema mpaka sasa wameamua kumshitaki Kamishina wa Ardhi kwa kutowatendea haki, hivyo kesi ipo Mahakama Kuu na vielelezo vyote wanavyo na hawezi kuvitoa kwa mtu mwingine yeyote bila idhini ya mwanasheria wao, kwani wanaendelea na kesi.

Mtendaji wa Kata wa Pugu Kajiungeni Kona, Justin Nyangwe, amesema kwamba kuhusu suala hilo yeye si msemaji, badala yake atafutwe Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala.

Mart Lalani, amesema anavyolifahamu suala hilo, mwanzoni eneo hilo lilikuwa ni la Kampuni ya Amadoli na vijana hao haliwahusu, kwani wafanyabiashara walipewa kufanya biashara kutoka kwa mmiliki huyo.

Mmiliki wa Kampuni ya Amadoli, Petro Stella, amesema kuwa yeye eneo hilo analijua ni mali ya Kampuni yao ya Amadoli na hawezi kuzungumza kwenye simu, yupo Arusha.

 Mwenyekiti wa CCM Pugu Bombani, Bilungo Jackson, amesema mwenye eneo hilo ni Kampuni ya Amadoli, alinunua eneo hilo kwa lengo la kuweka mbolea zake za kuku.

Aidha, aliongeza kwamba wakati kampuni hiyo inaendelea na umwagaji wa mbolea kwenye eneo hilo kulikuwa na vibaka wanavamia watu ndipo wananchi walipoamua kupeleka maombi kwa kampuni hiyo wafanye shughuli za maendeleo.

Amesema wajanja wachache walitumia mwanya huo kwenda kutengeneza hati kwa kushirikiana na manispaa, wakatengeneza hata feki ili waonekane ni wamiliki wa eneo hilo.

Amesema kuwa eneo hilo yeye analifahamu sana tangu miaka mingi wakati bado lipo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, lilikuwa linaitwa Kajiungeni na mabomba yalikuwa bado hayajajengwa, ndiyo maana hakukuwa na Mtaa wa Bombani kama ilivyoandikwa katika hati yao. “Bomba limekuja sasa hivi,” alibainisha.

5814 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons