“Niliona  ni vyema nikuze kipaji changu kuliko kitumike na watu wengine kwa kuajiriwa, kwani nina ubunifu mkubwa kuliko ndiyo maana niliona ni bora nianzishe kampuni yangu.” Hayo ni maneno ya Denis Vedasto, mkazi wa Kitunda, Dar es Salaam ambaye ni mjasiriamali anayejishughulisha na utengenezaji wa vitanda vya hospitali, ambavyo vingine hutumiwa wakati wa kinamama kujifungua.

Anaeleza alivyoanza kujiendeleza na kufikia hatua ya kushiriki Maonyesho ya 36 ya Sabasaba mwaka huu 2012 alikopata bahati ya kukutana uso kwa uso na Rais Jakaya Kikwete, alipotembelea banda la Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO). Vedasto alikuwa amepewa fursa ya kuonyesha bidhaa zake kama mmoja wa wajasiriamali walioko Dar es Salaam.

 

“Nilijisikia furaha sana kutembelewa na Rais Kikwete na kushikana naye mikono, na yeye alifurahishwa sana na ubunifu wangu hasa baada ya kumwelezea jinsi nilivyoanza na kufikia hapo. “Vitanda hivi ni vya aina nyingi. Kwa mfano hivi wanavyotumia kina mama kujifungulia vinaitwa ‘Delivery Beds’. Hivi vina sehemu mbili. Sehemu ya kwanza inampa fursa mama kujifungua, na baada ya kujifungua inavutwa sehemu ya pili kufikisha urefu wa futi sita aweze kupata nafasi ya kupumzika. Kitanda kina nafasi ya kuongeza urefu mama anyooshe miguu yake tayari kwa ruhusa ya kwenda nyumbani,” anasema Vedasto.

 

Anasema aina nyingine ya kitanda ni ya kuwalazia wagonjwa. Vitanda hivi havihitaji kuwa na mito kwani tayari wamevitengeneza kwa staili ambayo mgonjwa akitaka kulala anainua sehemu ya juu inakuwa kama mto kwa ukubwa anaoutaka. “Sifa kubwa ya kitanda hiki ni pale mgonjwa anapotaka kula, hakuna haja ya kumshikilia kwani ‘unakiseti’ mithili ya kochi, mgonjwa anakaa kwa kuegemea kutegemeana na mgonjwa anavyotaka.

 

“Nilijifunza utaalamu huu katika Chuo cha Taifa cha Mafunzo ya Ufundi Stadi Kagera (NVTC). Kwa sasa kinaitwa VETA ambako nilimaliza mafunzo mwaka 1993. Niliajiriwa na Bokoba Engineering Works na baadaye nikafanya kazi SIDO Dar es Salaam kwa muda. “Baada ya kukaa katika ajira kwa kipindi ndipo nilipoamua mwaka 2008 kuanzisha kampuni yangu na kuweka ubunifu wangu kwenye kampuni kuliko kuwatumikia watu wengine. Na katika hili nilipata msaada mkubwa kutoka kwa Shirika Linalohudumia Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO)”

 

Vedasto anabainisha kwamba SIDO ndiyo waliomsaidia kufikia hatua ya kushiriki Maonyesho ya 36 ya Sabasaba mwaka huu. Anawashukuru kuwa wamemwezesha kwa kumpa ushauri, banda na fursa ya kushiriki maonyesho haya ambayo ni nafasi adhimu. Ukiacha vitanda vya kina mama kujifungulia na vya wagonjwa wodini, Vedasto anatengeneza madirisha, milango ya vyuma, viti na madawati, meza za ofisini.

 

“Kwa ujumla tunatengeneza samani za chuma (steel furniture). Yeyote anayehitaji atuone sisi tupo pale Buguruni Kisiwani ‘A’ CCM – ndipo ilipo karakana (workshop) yetu,” anasema Vedasto. Tangu ameshiriki maonyesho haya, anasema ameshapata angalau mikataba miwili ya kazi na anapata simu nyingi zenye kutia matumaini, hali inayomfariji kuwa maneno ya Rais Kikwete kwake kuwa mwelekeo wake unatia moyo na atafika mbali ameanza kuona matunda yake.

 

Anawasihi sana Watanzania waweze kuwa na tabia ya kupenda vifaa vinavyozalishwa hapa nchini, kuliko vinavyotoka nje ya nchi kwani bidhaa zake ni bora zaidi na ni vya garama nafuu.  Anasema kuwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini zikinunuliwa kwa wingi zitakuza viwanda vya ndani, zitazalisha ajira za kutosha na hatimaye kukuza uchumi wa taifa kwa ujumla.

 

“DEVE GENERAL SUPPLIES ni jina la kampuni yangu na ninapatikana kwa simu 0787036302, 0715036302,  Buguruni karibu na ACB Bank”. Pamoja naye anasema anao vijana wapatao sita anaofanya nao kazi, hali inayompa fursa ya kutafuta masoko na kumaliza kazi kwa wakati. Mjasiriamali huyu anajipanga kushiriki tena maonyesho ya Sabasaba yajayo, ila anaiomba Serikali kuwaangalia vijana wabunifu kama yeye na kuwawezesha kimtaji, hali itakayokuza pato lao na uchumi wa Taifa, kwani wakipata fedha wigo wa kulipa kodi utaongezeka na Taifa litaneemeka.

 

By Jamhuri