BandariBaada ya gazeti la JAMHURI kuchapisha habari za uchunguzi wiki iliyopita kuonyesha udanganyifu unaofanywa na baadhi ya maafisa wa Bandari ya Dar es Salaam, hali inayoipotezea mapato Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), wiki moja tu, hali imebadilika.

Bandari ya Dar es Salaam sasa imejaza mzigo wa makontena na magari kwenye yadi zake, hali inayotafsiriwa kuwa mapato ya TPA sasa yatapanda kutokana na kukusanya tozo mbalimbali katika mizigo hiyo.

Habari za uhakika kutoka Bandari na kwa wamiliki wa Bandari Kavu (ICD) nchini, zinaonyesha kuwa baada ya JAMHURI wiki iliyopita kuchapisha taarifa zinazoonyesha mchanganuo wa mapato jinsi yanavyopotea, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko alikata mara moja ‘mrija’ unaopoteza mapato.

“Tunawashukuru sana JAMHURI. Habari ile ilipotoka, watu wakafunguka macho. Kila mtu alikuwa anashangaa. Tena nyie wakati mliandika zinapotea Sh bilioni 200 kwa mwezi, uhalisia ni zaidi. Zinaweza kuwa hadi Sh bilioni 500. DG Kakoko aliagiza mara moja kusitisha mzigo usitolewe Bandari ya Dar es Salaam kwenda kwenye ICD kabla Bandari haijajaa,” kilisema chanzo chetu.

Gazeti la JAMHURI liliripoti kuwa baadhi ya watendaji wa Bandari ya Dar es Salaam wasio waadilifu wamekuwa ‘wakiuza mizigo’ isishushwe katika Bandari ya Dar es Salaam ipelekwe kwenye ICDs ambazo ni za watu binafsi wanaodaiwa kuwapatia fungu la kumi.

Jumapili gazeti la The Guardian on Sunday, limechapisha habari ikionyesha kuwa baadhi ya wamiliki wa ICDs wanajipanga kufunga biashara na wengine hali zao ni mbaya. JAMHURI linazo taarifa kuwa kampuni nyingi za uwakala wa meli na Bandari Kavu nchini zinapumulia mashine.

Baadhi ya ICD zilizotajwa ni Farion Trading Limited, ambayo ina uwezo wa kuhifadhi magari 2,250, lakini hadi mwishoni mwa wiki ilikuwa na magari 120. ICD ya Chikasa iliyopo Mbagala Dar es Salaam ina uwezo wa kuhifadhi magari 1,800, lakini hadi Jumapili walikuwa na magari 113, huku wakiwa hawajapokea mzigo mpya kwa wiki kadhaa.

Bandari ya Silver, inayomilikiwa na Mbunge wa Kibaha Mjini, Sylvester Koka, mmiliki huyo ameliambia JAMHURI kuwa tayari wamepunguza wafanyakazi zaidi ya asilimia 50 kutokana na biashara kushuka kwa kiwango cha kutisha.

“Tumepunguza wafanyakazi bado hatujafunga, tumepunguza wafanyakazi zaidi ya asilimia 50. Ungeongea na mejena anaitwa Ally angeweza kukupatia data vizuri zaidi,” amesema Koka. Ameongeza kuwa biashara ikiwa nzuri watu watarudi kazini. “Hiyo ni hasara kubwa kwa sababu tumeishawekeza alafu unapopunguza wafanyakazi ina maana unapoteza fedha,” amesema Koka kwa masikitiko.

Baadhi ya wamiliki wa ICD wameliambia JAMHURI kuwa TPA haiwatendei haki kwani waliingia mkataba na wamewekeza fedha nyingi kujenga miundombinu, lakini sasa ghafla wanajikuta hawana cha kufanyia majengo. “Wengine tuna mikopo benki. Wasipotupa mzigo tunailipaje?” anahoji mmoja wa wamiliki wa ICD.

Janeth Ruzangi, Meneja Mawasiliano wa TPA, ameliambia JAMHURI kuwa wenye ICD hawapaswi kulalamika kwani kinachofanyika sasa ni utekelezaji wa makubaliano ya kimkataba walioingia na Bandari.

“Mkataba wetu na hao wanaopokea magari, wanaitwa port extension. Na katika ule mkataba walikubaliana kwamba kwanza tutajaza bandarini, alafu tutafanya in rotation bases (kwa mzunguko), kwamba meli hii itapeleka huku kama Bandari imejaza, tutapeleka huku, yaani kwa kikao kabisaaaa, wanakubaliana.

“Sasa what happens now (kinachotokea sasa) ni kwamba, nafasi tunayo ndani ya Bandari, kwa hiyo meli inapokuja priority (kipaumbele) ya kwanza ni Bandari, eheee, kwa hiyo siyo kwamba wananyimwa, warejee tu mkataba wao unasemaje,” amesema Ruzangi.

Amesema kinachoendelea sasa ikiwa zitafika meli tatu kwa wakati mmoja wanaweza kupata mzigo, ila ikija meli moja ni lazima ijaze bandari kwanza. Ruzangi ameongeza: “Tumejipanga, tunasema wateja wapitishe mizigo yao Bandari ya Dar es Salaam. Kama umeishalipia mizigo yako ukamaliza na documentation zote na umelipia, unaweza kuchukua mzigo within 48 hrs… kwa sasa tunaruhusu direct delivery (mzigo unatoka melini kwenda kwa mteja.”

Amewataka wateja kuitumia Bandari ya Dar es Salaam akisema ina ulinzi wa kutosha na kwa sasa inafanya kazi saa 24, hivyo wateja wajisikie huru kuitumia na yeyote anayekutana na urasimu afikishe malalamiko yake kunakohusika yatatatuliwa ndani ya muda mfupi.

Baadhi ya maafisa wa Bandari waliozungumza na JAMHURI, walishangilia hatua hiyo iliyochukuliwa na Mkurugenzi Mkuu Kakoko, wakamshauri awawajibishe viongozi waliokuwa wanapeleka mzigo nje ya Bandari, badala ya kutekeleza mkataba unavyosema kuwa ICD zitapewa mzigo pale tu, Bandari inapokuwa imejaa.

Bandari kwa sasa ina uweza wa kuhifadhi kontena 8,500 na kutokana na kushuka kwa mzigo ambapo kwa wiki yanaingia makontena kama 600 tu, mzigo huo wote sasa unakaa bandarini. Kabla ya Kakoko kupiga marufuku, ilikuwa asilimia 75 ya makontena hayo 600 inapelekwa kwenye ICD hali iliyoshusha mapato ya Bandari kwa kiasi kikubwa.

Zipo taarifa pia kuwa hata baadhi ya meli zimehamishiwa kwa washindani wa TPA kwa njia ya ‘kuuza’ mzigo wahusika wakapewa fungu la kumi na nyingine zimehamishwa baada ya kuweka sera kuwa kila mzigo lazima uende kwenye ICD hali inayoongeza gharama ya kufanya biashara na wateja hawaipendi.

By Jamhuri