Baadhi ya visima vya maji safi katika Kitongoji cha Buseresere wilayani Chato, mkoani Geita vimebainika kuwa na mchanganyiko wa maji na dizeli.

Kutokana na hali hiyo, wananchi hao wanaelekeza lawama zao kwa mmiliki wa Kituo cha Mafuta cha Buseresere, Samwel Magazi. Kituo hicho cha mafuta kipo katika Mtaa wa Kabaherere, Kitongoji cha Buseresere, Kata ya Buseresere.

Wananchi hao wamechukua hatua kadhaa, mojawapo ya hivi karibuni ni kumwomba Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Luhumbi, kuingilia kati sakata hilo baada ya taasisi zinazohusika kushindwa kulipatia ufumbuzi huku wakidai kuwa kuna mchezo mchafu uliolenga kuwanyima haki wananchi.

Katika madai yao wananchi wanaamini haki haikutendeka kutokana na kutopatiwa majibu ya uchunguzi kwa muda mrefu, kutoridhishwa kwao na mwenendo wa uchunguzi kwa kuwa mmiliki wa visima hivyo ndiye aliyegharimia posho na uchunguzi, huku kukiwa na madai kwamba baadhi ya maofisa wa serikali waliofika hapo kulipwa posho kwa ajili ya kazi hiyo na hata mashine iliyotumika haikuwa na kiwango bora kutokana na kushindwa kutoa vipimo halisi.

Wananchi hao waliwaeleza waandishi wa habari hivi karibuni kwamba visima walivyochimba vilitoa maji yenye mchanganyiko wa mafuta ya dizeli.

Wananchi hao walidai kuwa walikuwa wakiyatumia maji hayo kupikia, kuoga, kufua, kuosha vyombo vya ndani pamoja na matumizi mengine ya kibinadamu kama kumwagilia bustani na kwa sasa baadhi ya familia zimesitisha matumizi ya maji hayo huku wengine
wakiendelea kuyatumia kwa maelezo kuwa hawana uwezo wa kununua maji tofauti na hayo ya kisima.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI ikiwemo kuzungumza na wananchi hao umebaini kuwa visima hivyo vilikuwa na mafuta ya dizeli lakini wananchi awali hawakujua chanzo cha mafuta hayo.
Baadhi ya wananchi waliokumbwa na mkasa huo ni pamoja na familia ya Sudi Mussa ambaye amesema kisima chake kina maji yaliyochanganyika na mafuta na kuongeza kuwa, hata wataalamu kutoka wilayani Chato walikwisha kutembelea na kubaini mafuta katika visima hivyo.
Kwa upande wao wananchi wamedai kuathirika kiafya, ikiwamo kupata vidonda vya koo. Miongoni mwa familia zilizopata madhara ni pamoja na familia ya mama aliyejulikana kwa jina la Maimuna. Familia ya Adrian Mutasingwa na Sudi Musa, pia ni miongoni mwa zilizoathirika baada ya kutumia maji hayo yanayosadikika kuwa na mafuta ya dizeli. Sehemu ya wanafamilia wanaeleza kuwa walianza kuhisi baridi sana mwilini nyakati za usiku inayoambatana na homa, muwasho wa ngozi, na harufu mbaya. Awali waliamini kuwa hali hiyo ni matokeo ya matumizi ya maji hayo.
Hata hivyo JAMHURI limeelezwa kuwa wakazi wa kijiji hicho wanategemea maji ya visima lakini  mwaka huu walibaini tatizo hilo na kumfuata mmiliki wa kituo husika cha mafuta ili afanye jitihada za kukagua visima vyake vya mafuta kwa kuwa wanaamini mafuta hayo yanatiririka kutoka kwake.
Uchunguzi zaidi wa gazeti hili umebaini kuwa kituo hicho cha mafuta kiko umbali wa takriban mita 100 kutoka kwenye makazi ya wananchi hao wanaolalamika na kwamba awali kulikuwa na taarifa kuwa mmiliki wa visima hivyo, Samwel Magazi, amekuwa akiwaomba wakutane ili wazungumze namna ya kupata suluhisho.
Mmiliki wa visima hivyo vya mafuta, Magazi, katika mazungumzo yake na JAMHURI kuhusu sakata hilo hivi karibuni amekiri kupokea malalamiko na kufafanua kuwa moja ya hatua alizochukua ni kumtafuta Bwana Afya wa Wilaya ya Chato ili kufanya uchunguzi.
Katika utetezi wake Magazi amesema baada ya madai hayo Ofisa Afya wa Wilaya ya Chato baada ya kupima maji hayo alijiridhisha kwamba yamekuwa na mchanganyiko wa mafuta. Hata hivyo amesema ofisa huyo alikanusha mafuta hayo kutoka katika kituo husika.

“Ni kweli yale ni mafuta, tulithibitisha pamoja na ofisa afya wa wilaya lakini matenki yangu ya mafuta hayavuji,” amesema Magazi na kuongeza kuwa makubaliano kati yake na bwana afya ilikuwa ni kuwakutanisha na wananchi waliokuwa wakilalamika ili kuweza kubaini hayo mafuta yanatoka kwa nani,” amesema Magazi.
Magazi alikiri kuwa mwaka 2018 alipata malalamiko hayo na akatumia fedha zake kuwalipa watu kuchimba kisima kimoja kati ya vilivyodaiwa kuwa na mafuta. Walichimba kwa kuongeza kina kwenda chini ili wagundue chanzo cha mafuta hayo.
Akithibitisha kutafutwa na mmiliki wa kituo cha mafuta ili kufanya makubaliano, Sudi Musa, amekiri kutafutwa na Magazi na kumpa kazi ya kusafisha kisima cha Adrian Mutasingwa ambacho kilikuwa na mafuta pia, lakini amesema baada ya kuchimba, mafuta yalikuwa mengi ndani ya kisima hicho na Magazi aliahidi kufanya utafiti zaidi.
“Ni kweli niliwahi kutafutwa na Magazi na kunipa kazi ya kusafisha kisima cha Mutasingwa ambacho kilikuwa na mafuta pia. Lakini baada ya kuchimba, mafuta yalionekana kuwa ni mengi ndani ya kisima hicho na Magazi aliahidi kufanya utafiti zaidi,” amesema Sudi.
Hata hivyo JAMHURI limeelezwa kuwa pamoja na kutokea kwa tatizo hilo, Magazi hakutoa taarifa ya kusambaa kwa mafuta hayo kwa wananchi kama ambavyo Mamlaka ya Udhibiti wa Mafuta  na Maji (EWURA) inavyomtaka kufanya kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta (The Petroleum Act) namba 21 ya mwaka 2015, kifungu cha 217 (1-9) kinachoweka masharti kwa mmiliki wa leseni ya mafuta, na mmiliki endapo mafuta yakivuja achukue hatua za haraka ili kutatua tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa EWURA ndani ya saa 24.

JAMHURI lilimtafuta Meneja wa EWURA Kanda ya Mwanza, Mhina Mathew, kujibu maswali kadhaa kuhusu sakata hilo, ikiwa ni pamoja na taasisi yake kudaiwa kushindwa kutenda haki katika kufanya uchunguzi wa sakata hilo.

“Madai hayo si ya kweli. Tulifanya uchunguzi na ripoti tulishaituma kwa viongozi wa serikali, waende kwa mkurugenzi au kwa mkuu wa wilaya…. tulibaini kuwa matenki hayo hayana shida na kwamba pamoja na hayo tulipata shaka kuhusu tenki namba mbili ambalo tulilifunga,” amesema.

Tangazo la Serikali Namba 380 la Machi 3, 2018, kifungu cha 31(1-3) kimeweka masharti ya kumlazimisha mmiliki wa biashara ya mafuta kuhakikisha anafanya tathmini ya athari ya mazingira kabla hajaanza biashara hiyo au kujenga, na kuhakikisha anafuata sheria ya mazingira kama anavyotakiwa kufanya katika sheria nyingine za nchi.
Aidha, kwa mujibu wa tangazo la Serikali (GN) la Machi 3, 2018, kifungu cha 45 (1-5) kinatoa maelekezo kwa wauzaji wa mafuta na watumiaji na wahifadhi hatua za kufuata endapo mafuta yatavuja au kumwagika.
Kifungu hicho kinaweka faini ya Sh milioni 100 kwa mtu aliyetiririsha mafuta au adhabu ya kufungwa kifungo kisichopungua miaka 10 endapo hatachukua hatua za makusudi zilizowekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni hizo ili kuondoa madhara yatokanayo na mafuta hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel, hakuweza kupatikana baada ya simu ya mkononi kuita muda mrefu bila majibu.

1294 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!