TEC, Bakwata, CCT wafichua mkwamo

 

Rais wa TEC, Askofu Gervas Nyaisonga

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) wamefichua mambo manane yanayoifanya nchi ishindwe kuwahakikishia wananchi uchumi imara na maendeleo endelevu.

Mbali na kufichua aina hizo nane za udhaifu katika uchumi wa taifa, taasisi hizo zimebainisha fursa nane kuu, changamoto tano na aina nyingine nane kuhusu uwezo uliomo ndani ya uchumi wa nchi.

Lakini pia, wamechanganua baadhi ya taasisi nyeti za kitaifa ikiwamo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakisema: “Benki Kuu ya Tanzania ilikuwa huru zaidi katika utendaji wake kupitia sheria mpya ya mwaka 2006 ingawa bado kuna changamoto ya kuingiliwa na maamuzi ya kisiasa. Serikali inateua watendaji wa Benki Kuu na kupanga mishahara na mafao yao ya uzeeni, hii inasababisha benki hii kutokuwa na uhuru wa kujitegemea.

“Mchakato wa kuwapata watumishi wa Benki Kuu ya Tanzania unapaswa kuzingatia ujuzi na ubobezi. Wanaoomba nafasi hizo ni vema wakafanyiwa usaili ili kupata wasimamizi na watumishi makini wa taasisi hii muhimu. Taratibu zinapaswa kusimamiwa vizuri kuhakikisha Benki Kuu inaweza kupambana na athari za changamoto mbalimbali za masoko ya fedha,” wameeleza viongozi hao wa dini kupitia kitabu walichokizizundua wiki iliyopita kinachofahamika kama Uchumi wa Soko Jamii.

Na kwa hiyo, wanashauri Benki Kuu ya Tanzania iwe huru na iondokane na ushawishi wa kisiasa huku Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, akilieleza JAMHURI kwa ufupi kuwa: “Serikali haiwezi kubishana na viongozi wa dini. Mawazo yao tunayaheshimu. Pale panapostahili kuchukua hatua, serikali itachukua hatua kwa masilahi ya taifa na wananchi wote kwa ujumla kama ambavyo imekuwa ikifanya siku zote.”

Viongozi hao, wamekuja na dhana ya UWEZO ambao wameutafsiri kuwa ni mambo yaliyopo nchini ambayo yanaipa nchi nguvu ya kufanya mambo vizuri na kwa ufanisi, lakini UDHAIFU ni mambo yanayoifanya nchi ishindwe kufanya shughuli zake vizuri.

Pia wamesema kuna FURSA ambazo ni mambo ambayo nchi inayo au inaweza kuyapata nje na ingeweza kuyatumia kwa manufaa yake, wakati CHANGAMOTO kwa mujibu wa tafsiri yao, ni yale mambo yanayoweza kuleta matatizo ama kurudisha nyuma shughuli za kimaendeleo nchini.

Wamebainisha hayo katika kitabu chao kilichozinduliwa hivi karibuni kuhusu “Uchumi wa Soko Jamii kwa Tanzania” kuelekea maendeleo shirikishi na endelevu.

Sheikh Mkuu wa Tanzania,
Mufti Abubakar Zubeir

Aina ya kwanza ya udhaifu

Aina nane za udhaifu walizozitaja ni pamoja na teknolojia na viwanda, wakisema kumekuwa na elimu ndogo ya teknolojia, uwekezaji mdogo wa teknolojia kwenye viwanda vidogo na vya kati, pamoja na utegemezi mkubwa kwenye njia za asili za kilimo.

Wanafafanua zaidi kwa kueleza, ukuaji wa uchumi unasaidiwa na maendeleo ya teknolojia na matumizi ya mbinu na njia za kisayansi na kwamba nchi inapowekeza vya kutosha kwenye maendeleo ya teknolojia inaweza kuendelea kwa kasi kwa sababu matumizi ya teknolojia sahihi husaidia kuongeza uzalishaji katika taifa hata kama rasilimali ni chache.

“Tanzania hutumia asilimia moja ya pato lake la taifa kwa shughuli zinazohusu sayansi, teknolojia na uvumbuzi. Matokeo ya uwekezaji huu ni madogo kwa sababu serikali haiwekezi vya kutosha kwenye kufanya utafiti. Kwa vile kuna uwekezaji mdogo kwenye sekta hii, kumekuwa pia na mchango mdogo wa kifedha kutoka kwenye sekta binafsi kwa ajili ya kuwekeza.

“Hali ya utafiti nchini bado iko nyuma, hivyo matokeo ya tafiti mbalimbali zinazofanywa hayawezi kukusanywa na hivyo hayawezi kutumika kwa maendeleo ya viwanda. Ukilinganisha na nchi zingine, Tanzania inashika nafasi ya chini kwenye matumizi ya teknolojia na kuingia kwenye mfumo wa kidijitali ukiilinganisha na nchi kama Uganda, Kenya na Nigeria,” wanaeleza viongozi hao katika kitabu hicho.

Kwa ujumla, wanaeleza kuwa hakuna matumizi ya kutosha ya teknolojia mpya na za kisasa kutokana na gharama kubwa za uendeshaji, lakini, vilevile hakuna uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa kutumia teknolojia hizi.

Kutokana na udhaifu huo, wameshauri: “Endapo Tanzania inataka kufanikiwa kwenye mpango wake wa uchumi wa viwanda, inahitaji kubadili mtazamo wake na kuwekeza katika teknolojia.”

Maeneo mengine ya udhaifu

Udhaifu mwingine wameubainisha katika suala la umaskini, kwamba idadi ya maskini ni kubwa na tofauti kati ya wenye nacho na wasionacho inaongezeka. Eneo jingine ni kuhusu sekta binafsi na biashara.

“Sekta binafsi na biashara ni dhaifu kwa upande wa wazawa na kampuni za wazawa ni chache katika biashara za kimataifa,” inaelezwa katika kitabu hicho.

Eneo jingine dhaifu lililotajwa ni soko la ajira ambapo wasio na ajira ni wengi pamoja na wasomi wa vyuo vikuu wasio na ujuzi wa kutosha kulingana na soko la ajira. Mbali na hilo la soko la ajira, eneo jingine dhaifu ni elimu wakisema thamani ya elimu ni ya chini, hali inayoambatana na mambo kadhaa, kama vitendea kazi duni sambamba na ufundishaji duni.

Eneo la afya pia ni moja ya eneo lenye udhaifu, kwamba kumekuwa na mfumo dhaifu wa utoaji huduma, kwa mfano, ukosefu wa wataalamu wenye ujuzi na weledi, na bima ya afya ipo chini sana, haijawafikia wengi. Nishati na maliasili nayo yametajwa kuunda jumla ya maeneo manane yenye udhaifu nchini.

Katika nishati na maliasili imeelezwa kuwa upatikanaji wa umeme usio wa uhakika na matumizi mabaya ya maliasili ni tatizo.

“Tanzania ina utajiri mkubwa wa rasilimali endelevu. Rasilimali hizo ni pamoja na maji, makaa ya mawe, upepo, jua na mabaki ya takataka za mimea. Kati ya hizi, maji ni chanzo kikubwa cha uzalishaji wa umeme. Hata hivyo, mabadiliko ya hali ya hewa na matatizo katika mifumo ya usambazaji imesababisha kuwa vigumu kutegemea nishati ya umeme itokanayo na nguvu za maji pekee.

“Tanzania ingeweza kutumia njia mbadala za kuzalisha nishati ya umeme ambazo zina uwezo mkubwa wa kuzalisha nishati hiyo, mfano, umeme utokanao na makaa ya mawe, upepo, nishati ya jua pamoja na mabaki ya takataka za mimea,” imeelezwa. 

Kwa sasa nchini, asilimia 90 ya vyanzo vya nishati zitumikazo majumbani zinatokana na sekta ya misitu, mfano kuni na mkaa, ikikadiriwa kuwa Watanzania milioni moja wanajihusisha na biashara ya mkaa, na sekta ya misitu nchini inachangia takriban nusu ya vifaa vya ujenzi nchini, hivyo, umuhimu wake ni mkubwa.

Eneo la nane la udhaifu ni hali ya uchumi, wanasema katika hali ya uchumi kumekuwa na ukosefu wa dira na itikadi ya kiuchumi, pamoja na utekelezaji hafifu wa mbinu bora za zamani.

 

Katibu wa TEC, Dk. Charles Kitima

Fursa nane katika uchumi

Licha ya kuainisha maeneo hayo manane ya udhaifu, viongozi hao kupitia kitabu hicho wameainisha maeneo manane ambayo ni fursa. Kwanza ni soko na biashara. Hapa wanaeleza kuwa makubaliano kati ya nchi na nchi na ushirikiano wa kikanda kama vile, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Shirikisho la Biashara Afrika, Mpango wa Makubaliano ya Kibiashara na Marekani (AGOA) kuhusu mazao ya kilimo na madini.

Fursa nyingine ya pili ni kubadilishana teknolojia baina ya mataifa. Tatu, mawasiliano, kwamba gharama katika mawasiliano ni ndogo ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika. Nne, huduma za afya, kwamba kuna wadau wa afya kwa ajili ya kuboresha huduma za afya. Tano, mitaji. Hapa wanaeleza kuwa uboreshwaji wa soko la mitaji mfano huduma za kutuma na kupokea fedha kupitia mitandao ya simu kama M-PESA inavyotumika barani Afrika.

Sita, baadhi ya nchi kukosa bandari. Saba. Hali ya ushindani, kwamba ongezeko la bidhaa za Tanzania hasa mazao ya kilimo inayotokana na ongezeko la watu kikanda. Na fursa ya nane wameibainisha kuwa ni “mifano ya kuigwa” kwamba uwepo wa mifano inayoweza kuigwa inayohusu uchumi jamii inayoweza kutekelezwa nchini Tanzania.

Maeneo manane ya uwezo

Eneo la kwanza wanalotaja ni ukuaji imara wa uchumi. Pili, idadi kubwa ya vijana, yaani nguvu kazi ya kutosha. Tatu, upatikanaji wa ardhi yenye rutuba na maliasili nyingi za aina mbalimbali. Nne, nchi ipo pazuri kijiografia, chukulia mfano wa bandari, bahari na maziwa. Tano, umoja wa kitaifa, amani na maelewano, lugha moja, mshikamano wa kweli. Sita, miundombinu imeboreshwa na mtandao wa mawasiliano umesambazwa kote nchini. Saba, elimu kwa wote na ongezeko la vyuo vya elimu ya juu na nane, ni kuhusu afya kwamba, ongezeko la hospitali za kisasa kama vile Hospitali ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Changamoto

Wamebainisha pia changamoto tano ambazo ni pamoja na masoko huria na biashara, jicho lao likimulika uwezo wa kampuni kubwa za kimataifa dhidi ya biashara za wazawa. Pili, ni kuhusu teknolojia ambapo kumekuwapo na ushindani mdogo kwenye ulimwengu unaobadilika haraka kiteknolojia.

Tatu, mazingira. Katika mazingira wanasema changamoto iliyopo ni hali ya hewa isiyoridhisha na mabadiliko ya tabia nchi yanayotokea. Nne, ni kuhusu hali ya ushindani wa kibiashara na hasa suala la mazingira mazuri kwenye nchi nyingine. Tano, ni hali ya kisiasa isiyo tulivu katika nchi zinazopatakana na Tanzania.

Kulinda mali binafsi

Katika kitabu hicho, wameeleza kile walichokiita ‘hali halisi’ kuhusu umiliki wa mali binafsi, kwamba ni jambo muhimu linalochochea wananchi kushiriki katika uzalishaji mali na kupata kipato.

“Kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya chini katika kulinda mali binafsi kwa kuwa bado mali za wawekezaji binafsi zinataifishwa. Wadau wa sekta binfasi hawana nguvu ya kusema lolote juu ya hili. Usajili wa mali binafsi ni wa gharama kubwa na huchukua muda mrefu ukilinganishwa na nchi nyingine,” wameeleza.

Lakini katika kupata suluhisho la hali hiyo vilevile wameshauri: “Ili mfumo wa uchumi soko jamii uweze kufanya kazi vizuri ni muhimu kuwepo na ulinzi wa haki miliki ya ubunifu na mali. Haki ya kumiliki mali ni lazima iheshimiwe kisheria na mfumo wa mahakama ulio huru na wa haki. Usajili wa haki miliki ni vema ukarahisishwa. Lazima kuwepo na makubaliano ya wazi juu ya hakimiliki ili kulinda watu binafsi katika soko.”

Hata hivyo, pamoja na maoni hayo, ofisa mmoja mwandamizi wa serikali ameliambia gazeti hili kuwa, kwanza, serikali haiwezi kutaifisha mali bila mchakato wa Mahakama. Pili, mali binafsi huwa zinalindwa tayari kisheria, akitolea mfano, Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999. Zaidi ya hapo, amesema hata kwenye suala la hakimiliki kuna Sheria ya Hakimiliki na Hakishirikishi ya Mwaka 1999.

11580 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!