nmb-4Hotuba za mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, zenye mwelekeo wa kuileta Tanzania mpya, zimeonekana kuwakuna wengi.

Dk. Magufuli, hotuba zake zimekuwa zikiwagusa wananchi kutokana na kugusa kero zinazowakabili moja kwa moja.

Kwa wale wanaotaka mabadiliko, amekuwa akiwaambia kuwa mabadiliko bora anayoyaahidi watayapata kupitia CCM, na si nje ya chama hicho anachosema kina hazina kubwa ya uongozi.

Amedhamiria kufuta ile dhana ya kiongozi anayechaguliwa au kuteuliwa kujiona “ameuala”, badala yake amesema mawaziri wake watafanya kazi usiku na mchana ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Katika mikutano yake mingi, amesikika akisema: “Itakuwa ni Serikali ya utendaji, Serikali ya utumishi yaani kutumikia watu, kutumikia umma wote wa Watanzania. Mawaziri wangu watakuwa wachache, watafanya kazi saa 24.”

Dk. Magufuli ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ujenzi, amesema: “Katika hili sitanii, nataka kujenga Tanzania ya Viwanda. Sasa huwezi kutimiza hayo kama unakuwa na mawaziri wanaolala.”

Anasema kwamba atafuata taratibu zote za uteuzi kwa mujibu wa mwongozo wa Serikali, lakini kabla ya mteuliwa kutangazwa hadharani, atazungumza naye.

“Kama wewe unaweza kazi. Ajibu: ‘ndiyo’, ndipo namtangaza.”

Anasema kwamba anafanya hayo yote akipania kuunda Serikali ambayo italeta mabadiliko kwa Watanzania na kama wapigakura wanataka kushuhudia hilo, basi wamchague Oktoba 25.

Anasema akichaguliwa atakuwa na timu ambayo, kila Mtanzania ataona kweli Serikali inanijali.

Anaeleza kukerwa kwake na habari za kijiji, kata, wilaya au mkoa kuwa na shida ya maji.

“Mimi nasema maji yote haya? Huyo waziri wa maji sijui, eeh… hiii… maana kama haleti maji naye anakwenda na maji, nichagueni muone,” anasema.

Kumekuwa na dhana ya viongozi wa umma wanapoteuliwa na kufanya kazi serikalini kujiona wamepata ulaji na matokeo yake wanakuwa miungu watu.

Dk. Magufuli anasema: “Kama waziri ni wa kwenda field, basi atakwenda field (eneo la kazi).”

Dk. Magufuli amesema sifa za watu atakaowajumuisha katika Baraza la Mawaziri ni kuchapa kazi na kutoa majibu yasiyo ya visingizio katika kuhalalisha ucheleweshaji wa huduma kwa wananchi.

“Ninaposema hata viwanda vitajengwa, yakija madai ofisini kwangu eti ofisa fulani amekalia faili na kuchelewesha kazi atawajibika ofisa huyo na waziri wake. Kufanya mabadiliko sitaona kazi. Hakuna ulaji wala rushwa hapa. Hapa ni kazi tu,” anasema.

Anasema waziri atayeteuliwa katika Baraza lake ni kujali muda katika kushughulikia kero za wananchi na ikitokea ameshindwa ni vema akawasiliana naye ili amsaidie.

“Hata ninyi wagombea ubunge, njoo gonga Ikulu hata kama ni saa 8 usiku. Sitaki kusikia visingizio,” amewahakikishia.

Anasema kwamba sifa nyingine ya waziri au naibu waziri wake ni kukubali kuchapa kazi bila kuchoka kwa saa 24 kwa sababu hatua iliyofikia sasa na kasi ya maendeleo hahitaji mtendaji goigoi.

“Napenda mtu anayesikiliza watu, anayesikiliza matatizo ya watu. Uwaziri kwangu ni utendaji, mtu kama Katibu Mkuu wizarani au Naibu wake ni kumsaidia tu. Hapo ndipo nataka tufike, Serikali ya Magufuli eeh, kazi tu.

“Nikiona mtu anaacha ofisi na ikagundulika amekwenda kwenye shughuli zake binafsi, hiii… tungoje muda tu,” anasema Dk. Magufuli, maarufu kwa jina la Tingatinga.

Jaji Joseph Warioba, akimnadi Dk. Magufuli maeneo mbalimbali mkoani Mara, alisema: “Suala la uadilifu. Nani amesikia Wizara ya Ujenzi kuna kashfa? (wananchi wanajibu, hakuna) Umesikia lini Magufuli amekwenda nje? (wananchi wanajibu, ‘hakuna’). Mchagueni huyo awafanyie kazi.”

Jaji Warioba anasema kwamba Dk. Magufuli atafunga njia zote za upotevu wa fedha za umma ili fedha zitakazookolewa zielekezwe kwenye huduma za jamii kama kuhakikisha kuwa zahanati, vituo vya afya na hospitali vinakuwa na dawa na vifaa tiba vya kutosha.

Dk. Magufuli ameahidi kuboresha maslahi ya watumishi wa umma, hasa akiwaangazia walimu, madaktari na wauguzi.

“Sitaki wauze dawa na kuzikuta pharmacy na hospitali hakuna dawa,” anasema Dk. Magufuli na kuongeza: “Hilo litawezekana kama tutaboresha maslahi ya wafanyakazi.

“Nataka kuwa Rais wa wote. Niwatumikie wote. Uwe CUF wewe ni wangu,  ACT – Wazalendo, Chadema, NCCR – Mageuzi wote nitakuwa mtumishi wenu. Wale wa Peoples Power wanichague Magufuli nilete maajabu,” anasema.

Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli anasema mambo mengi yamekwama serikalini kutokana na viongozi kushindwa kuchukua uamuzi mgumu na kwa wakati; jambo ambalo hataki kuona mawaziri wake wakilifanya.

Anasema: “Nchi haiwezi kusonga mbele kwa sababu kuna viongozi wamepewa madaraka, lakini wamekuwa na kigugumizi kuchukua maamuzi magumu na kwa wakati  jambo aliloahidi kulivalia njuga iwapo Watanzania watampa ridhaa ya kuwa Rais.”

Katika hilo, anasema akichaguliwa kuwa rais atakomesha tabia ya kuhamisha watendaji wabovu walioharibu sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Ameahidi kuwa Serikali yake itakachofanywa kwa watumishi waliovurunda ni kuwafukuza kazi na kuwapa nafasi hizo watendaji waadilifu ambao alisema wapo wengi, tena wenye elimu nzuri.

Mchuano wa urais unahusisha wagombea wanane, lakini mchuano wa kweli unaonekana kuwa kati ya Dk. Magufuli, na mgombea anayewakilisha Ukawa, Edward Lowassa.

1451 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!