Dodoma walizwa

Kampuni uuzaji viwanja, nyumba

yafanya yake

*
Mamia waambulia patupu, waangua

vilio

*
Ilitambulishwa bungeni kwa

mbwembwe nyingi

DODOMA

NA MWANDISHI WETU

Baadhi ya watumishi wa umma na watu
binafsi jijini Dodoma wanalalamika
kutapeliwa na kampuni ya uendelezaji ardhi,
ya Umoja wa VICOBA Tanzania (VIGUTA).
Miongoni mwa ‘wanaolia’ ni watumishi wa
serikali, hasa waliohamia Dodoma miezi ya
karibuni, wafanyabiashara na watu wengine
maarufu.
Tayari vilio vimeanza kuwapata baadhi ya
watu waliojitokeza kununua viwanja na
nyumba kupitia umoja huo. Wengi waliamini
kuwa watafanikiwa, wakiwamo wabunge
ambao walifanyiwa utambulisho rasmi
bungeni na kuamini watafaidika.
Wamesema wameingia makubaliano ya
kuendeleza ardhi kwa kujengewa nyumba
kwa miezi minne, lakini sasa ni mwaka
mmoja hakuna kinachoendelea.
Baadhi ya walionunua viwanja katika eneo
la Vikonje, Dodoma wamesema walipewa
mkataba wa makubaliano ya mauzo baina
yao na VIGUTA wakiahidiwa kupatiwa hati
baada ya hatua zinazotakiwa kufanyika,
lakini hawaoni dalili.
Wananchi waliozungumza na JAMHURI

kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini,
wamesema waliingia makubaliano hayo
Aprili na Juni, mwaka jana, na walipaswa
wakabidhiwe nyumba zao kati ya Agosti na
Oktoba mwaka huo, lakini hadi sasa hakuna
utekelezaji wa makubaliano hayo.
Miongoni mwa masharti ya VIGUTA kwa
mnunuzi ni malipo kwa ajili ya ujenzi wa
nyumba, ikiwamo asilimia 10 ya gharama za
ujenzi ukianza kufanyika.
Wamesema baada ya kuona wanaendelea
kulipa bila ujenzi kuanza ndipo walipoingiwa
hofu na kuanza kuhoji.
Mmoja wa wateja amesema aliingia
mkataba wa kuuziwa viwanja viwili na
kujengewa nyumba mbili za Sh milioni 12
kila moja.
“Baada ya kulipa hiyo asilimia 10 niliendelea
kulipa marejesho kama tulivyokubaliana
katika mkataba, ambapo nilitakiwa ndani ya
miaka 10 niwe nimemaliza kulipa pesa yote,
nikalipa miezi minne bila kuona chochote,
hapo nikashituka,

” amesema.

Ameliambia JAMHURI kuwa alianza
kufuatilia Kampuni ya VIGUTA bila kupata
majibu ya uhakika, ndipo aliamua kuandika
barua (nakala tunayo), akitaka arejeshewe
fedha zake, lakini hata hivyo barua hiyo

haikujibiwa.
“Nimeshachukua hatua kadhaa bila majibu
yoyote, hata ukipiga simu haipokewi, barua
niliyoandika Januari, mwaka huu sijajibiwa
hadi leo, pamoja na kwamba waliomba
kama watakwenda kinyume tumalizane nje
ya mahakama, lakini naona hawapo tayari
kwa lolote,

” amesema mwananchi huyo.
Mlalamikaji mwingine amesema alifuata
hatua kama alivyofanya mwenzake bila
mafanikio, ndipo alipokwenda kwa Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge,
ambaye aliahidi kufuatilia.
Hata hivyo, mkuu wa mkoa baadaye
alisema aliwaita viongozi wa VIGUTA, lakini
wakakaidi mwito wake. Amesema baada ya
VIGUTA kushindwa kutii amri yake,
amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Dodoma kuwatia nguvuni. Hata hivyo,
imebainika kuwa agizo hilo la mkuu wa
mkoa nalo halijatekelezwa.
Uchunguzi umebaini kuwa ofisi za umoja
huo mara kadhaa zimefungwa bila hata
kuwapo tangazo lolote la kuonyesha kama
wamehama au wamefunga shughuli zao.
Mkurugenzi Mtendaji wa VIGUTA, Christina
Rwebangira, amekiri kuwa wanadaiwa na
wateja hao, na kudai kuwa hali hiyo

imesababishwa na baadhi ya wabunge
walioingia nao makubaliano ya ujenzi wa
nyumba kwa pesa taslimu kushindwa
kuwalipa.
Amesema umoja huo una wateja wa aina
mbili – walioingia makubaliano ya ujenzi wa
nyumba za gharama nafuu kwa
makubaliano ya kulipa kwa awamu ndani ya
miaka 10, lakini ndani ya miezi minne
wanakuwa wamekwisha kuwakabidhi
nyumba; na wengine wanaolipa kwa fedha
taslimu.
“Iwapo wale wa malipo ya fedha taslimu
wangelipa fedha zote wanazodaiwa, hali
isingekuwa kama ilivyo, ila ninakuhakikishia
kwamba hakuna tatizo lolote, wateja wetu
watajengewa nyumba kama
tulivyokubaliana,

” amesema Rwebangira.
Akijibu hoja ya kwanini wamefunga ofisi bila
kutoa tamko kwa wateja wao, amesema ni
kweli wamefunga ofisi na sasa wanatafuta
sehemu nyingine ya kupanga.
Kuhusu kuvunja makubaliano ya
kuwakabidhi wateja wao nyumba kwa
wakati kama mkataba unavyoainisha,
amesema: “Hakuna tatizo, watajengewa
nyumba zao.” Hata hivyo hasemi ni lini
zitakamilika.

Kuhusu kukaidi mwito wa Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma, Rwebangira, amesema
walifika na wakatoa maelezo yao ambayo
Dk. Mahenge aliridhika nayo.
Katika hatua nyingine, Dk. Mahenge aliahidi
kuzungumza na JAMHURI jana kueleza
undani na hatima ya sakata hilo.
VIGUTA ilianzishwa kwa lengo la kutoa
mikopo kwa riba nafuu ikiwa ni pamoja na
ujenzi na uuzaji wa viwanja kwa bei nafuu.
Awali, mpango huo ulionekana kupokewa
vema na wananchi wa Dodoma.
Mapema mwaka jana viongozi wa VIGUTA
walifika bungeni Dodoma kwa lengo la
kuwahamasisha wabunge kujiunga na
umoja huo.
Walisema wanajenga nyumba kuanzia
gharama ya Sh milioni 10 hadi Sh milioni 60
kulingana na ukubwa, lakini pia wamekuwa
wakiuza viwanja vyenye ukubwa wa mita za
mraba 600 kwa Sh 800,000. Viwanja hivyo
vipo katika Kijiji cha Vikonje, kilometa 20
kutoka katikati ya Jiji la Dodoma.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Vikonje, Robert
Mshama, amesema umoja huo umenunua
ardhi yenye ukubwa wa ekari 50 kutoka kwa
mmoja wa wanakijiji.

“Ni kweli wana eneo katika kijiji changu,
lakini hawakununua eneo la kijiji, lile lilikuwa
eneo la mtu binafsi, na wakati wa
makubaliano yao serikali ya kijiji
haikushirikishwa, yanayaoendelea siyajui.
“Hata hao watu wanaouziwa na VIGUTA
bado sisi hatujashirikishwa. Wao wanakuja
na watu wao wanawauzia sisi hatujui, lakini
majuzi VIGUTA walikuja pale ofisini na
orodha ya watu waliowauzia eneo lile ili ofisi
yangu iwatambue.
“Tuliwauliza mbona hawajatushirikisha
tangu mwanzo? Hawakuwa na majibu,
wakaacha karatasi zao pale zenye majina
zaidi ya 300, ingawa namba kamili bado
sijaikariri,

” amesema Mshama.

Mwisho