Dodoma yakabiliwa na upungufu wa nyuma

Elias Kuandikwa, naibu waziri

NA EDITHA MAJURA

Dodoma

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kuandikwa, amesema wenye uwezo wa kujenga nyumba za kupangisha, kufanya hivyo mkoani Dodoma ili kusaidiana na Serikali kuwapatia  makazi bora watumishi wanaohamia mjini humo.

Kuandikwa amesema licha ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kumiliki nyumba 960 za kibiashara mkoani humo, hawajakidhi mahitaji ya nyumba yaliyopo kwa sasa.

Kaimu Meneja wa TBA wa Mkoa wa Dodoma, Steven Simba, amesema pamoja na changamoto nyingine, majengo wanayopangisha yamechakaa, hali inayosababisha kupata kipato kidogo.

Amesema hata majengo yaliyokuwa ya CDA, yanahitaji ukarabati utakaogharimu jumla ya Shilingi Bilioni 17,781,373,628.30.

Mpango wa kukabiliana na changamoto hiyo umeelezwa na Simba, kuwa ni kutumia makusanyo ya kodi kukarabati majengo hayo ili kuyaongezea thamani.

Ametoa wito kwa Serikali kuzishinikiza taasisi zake zilizopanga kulipa kwa wakati madeni wanayodaiwa.

Ametoa mfano kwa kutumia nyumba 458 ambazo tangu awali zilikuwa zikimilikiwa na TBA, ilitegemewa katika mwaka 2017/2018 wakusanye jumla ya Shilingi 1,108,800,000.00, lakini mpaka sasa wamekusanya Shilingi 464,879,296.00

Amesema nyumba zinazotumiwa na viongozi, watumishi na taasisi za Serikali zinadaiwa jumla ya shilingi 1,285,983,450.00. 

Samba ameiomba Serikali kuendelea kutenga fungu kwa ajili ya kukarabati nyumba za viongozi na kununua samani, kwani kumekuwa na malalamiko kutoka kwa viongozi kwamba zilizopo ni chakavu na hazibadilishwi kwa wakati.

Baada ya kufanya ziara kwenye majengo ya TBA yakiwemo makazi ya viongozi yaliyopo Area D na Kisasa, Kuandikwa amesema ipo haja ya kufanyiwa ukarabati, ikibidi kwa kutumia mkopo wa benki.

Amesema pamoja na uchakavu wa majengo, hata hali ya usafi wa mazingira katika makazi mengi hairidhishi, hivyo akaishauri TBA kuongeza gharama za usafi kwenye kidi ya wapangaji.

Amesema hatua hiyo itawezesha jukumu la usafi kuwa kwa TBA badala ya mpangaji.

Amesema pia ni muhimu kuweka utaratibu wa kuwawajibisha wapangaji wanaofanya uharibifu wa nyumba ama mazingira wanamoishi.

Ujenzi wa jengo la Tume ya Uchaguzi (NEC) unaosimamiwa na TBA na kutarajiwa kukamilika Julai mwaka huu, umesimama.

Msimamizi Mkuu wa mradi huo, Mhandisi Yohana Mashausi, amesema miongoni mwa sababu zilizokwamisha ujenzi huo ni kuadimika kwa vifaa vya ujenzi ikiwamo kokoto.