EWURA waomba subira ya wananchi

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imekiri kutokuwapo kwa mafuta ya kutosha nchini, kutokana mvurugano wa meli zinazoingiza mafuta nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Meneja Mawasiliano wa (EWURA), Titus Kaguo, alipozungumza na waandishi wa habari na kuwataka wanachi kuwa na subira wakati Mamlaka husika ikitafuta ufumbuzi wa kudumu wa suala hilo.

Alisema katika kukabiliana na upungufu huo, EWURA imeomba kibali cha kuuza mafuta lita 21,373,365 ambayo yalikuwa yapelekwe nje ya nchi. Kampuni tisa ziliomba kuuziwa nishani hiyo.


“Mafuta ambayo yapo hayatoshelezi mahitaji kwani dizeli ipo lita 35,825,282 ambayo ni matumizi ya siku (17) pekee. Petroli ni lita 21,247,361 ambayo ni ya siku 12, mafuta ya ndege ni lita 11,170,775 ambayo ni ya siku 25; mafuta ya taa ni lita 558,180 ambazo ni za siku tatu tu,” alisema Kaguo na kuongeza:


“Wastani wa kisheria wa takwimu halali siyo mzuri, hauridhishi kulingana na mahitaji, mfumo wa mafuta ukivurugika tangu mwanzo hugusa hadi vituo vilivyo mbali hasa maeneo ya mikoani, kwani huzidi kusonga mbele zaidi na inawezekana tatizo hilo limetokana na upungufu wa vituo vya kuuzia mafuta.


“Mafuta yanatoka kwenye depot yanaenda mikoani kwa usafiri wa magari, na ikumbukwe kwamba magari hayawezi kufika kwa siku moja na hali hii inasababisha upungufu wa mafuta hasa sehemu hizo kama inavyoonekana kwa sasa.”


Kuhusu mafuta ya taa, alisema, “Mafuta kwa wakati huu yakipanda bei ujue ni ulanguzi na itakapobainika kuwa kuna vituo vinadai havina mafuta tutaenda kupima na ikigundulika kuna mafuta hatua stahiki lazima zichukuliwe.


“Tatizo kama hili likitokea kwa hapa linaathiri zaidi mikoani kwani inasonga mbele zaidi kwa haraka. Tungekuwa na pipeline (bomba) kufikisha mafuta mikoani kwa haraka haya yasingetokea.”


Alipoulizwa kwanini tatizo hilo limekumba zaidi Singida, alijibu; “Inawezekana Singida wamiliki wa vituo vya mafuta wako wachache ndiyo maana tatizo limekuwa kubwa na pale linapotokea tatizo, mengi huzungumzwa.


“(EWURA) itabidi itoe takwimu kwa wananchi za mafuta yanayotoka kwenye depot, yanapelekwa wapi na mikoa ipi, taratibu na takwimu zinaonesha hii inatokana na changamoto zinazojitokeza kila mara. “Biashara ya mafuta ni ya kubadilika sana kulingana na wakati na changamoto zilizopo na pale panapotokea tatizo mengi husemwa.”