Je, wanahabari hawajui wanajua?

Katika jamii ya kibinadamu, yako makundi manne ya watu yanayotofautiana katika kuishi na kufanya kazi. Asili ya tofauti yao ni upeo na uwezo wa kufikiri, kutamka na kutenda mambo kupambana na mazingira waliomo.

Makundi hayo ni watu wasiojua na hawajui kwamba hawajui, na watu wasiojua lakini wanajua kwamba hawajui. Wengine ni watu wanaojua lakini hawajui kwamba wanajua, na mwisho ni watu wanaojua na wanajua kwamba wanajua.

 

Kwa vile makundi hayo yamo ndani ya jamii ya binadamu, ni dhahiri yamo ndani ya jamii ya Watanzania na ni dhahiri yamo ndani ya jamii ya wanahabari. Wanahabari hao ndiyo ninaowakusudia kuwazungumza kuhusu utendaji kazi wao.  Kati ya masomo yanayofunzwa katika taalumu ya habari ni somo la mawasiliano ya umma (Mass Comunication). Kimsingi mawasiliano ni kitendo cha kusafirisha mawazo, rai, fikra na habari.

 

Ili mawasiliano hayo yakamilike na yatokee sehemu tano muhimu ziwepo. Mpelekaji ujumbe, ujumbe wenyewe, chombo cha mawasiliano, mpokeaji ujumbe na majibu ya ujumbe uliopelekwa.

 

Tunapozungumzia wadau wa habari tunakusudia watoaji na wapokeaji habari. Tunapozungumzia wadau wa habari tunazungumzia watoaji na wapokeaji. Tunapozungumzia chombo cha mawasiliano ya umma tunamaanisha gazeti, radio, runinga, kitabu, simu, filamu au video, internet na vinginevyo vya aina hiyo.

 

Ukweli wadau  wanapolaumu ‘vyombo vya habari’, abadani hawamaanishi vyombo vya mawasiliano ya umma. Wanacholaumu ni waandishi na watangazaji wanaoendesha vyombo hivyo na kufanya kazi kwa upendeleo, ushabiki, uchache wa weledi na kutozingatia maadili ya taaluma ya habari.

 

Waandishi na watangazaji wanashiriki bila woga wala haya kuandika, kuhariri na kutangaza habari zenye viashirio vya chokochoko, chuki na ushabiki, kwa lengo la kuwafurahisha watoa habari bila kuangalia taaluma wala athari za mrejesho wa habari kwa wapokeaji.

 

‘Vyombo vya habari’ vinapopendelea kutoa habari za kundi moja ndani ya jamii moja na kuandika habari za kukijenga kikundi hicho na kuacha kikundi kingine – kwa misingi ileile ya utoaji habari – ni kujenga manung’uniko na chuki kati ya vikundi hivyo.

 

Ipo mifano mingi na vyombo vya habari vinafahamu. Sina haja ya kutoa mifano na kuvitaja vyombo hivyo. Lengo ni kukumbushana. Viache kwani nchi itakapoingia matatani vyombo havitakuwa salama tena kuandika habari za upendeleo na chuki. Kwa muhtasari tangu Awamu ya Kwanza hadi hii ya Nne ya utawala wa nchi yetu, vyombo vya habari vimelaumiwa hata kukosolewa kutokana na matangazo yao yenye migongano na maslahi ya wadau wa habari.

 

Tume ya Jaji Joseph Warioba imevitaja vyombo vya habari vinakula rushwa, Rais mstaafu Benjamin Mkapa amevikejeli havina weledi na viache kuandika na kupotosha habari zake.

Rais Jakaya Kikwete naye amesema vyombo hivyo vina makanjanja (waandishi wasio na taaluma) na kuwataka wasomee kazi zao. Waziri mweye dhamana ya habari, Dk. Finnella Mukangara, amevionya viache ushabiki na kujipachika unasiasa.

 

Je, kauli hizo zina ukweli ndani yake? Kauli hizo zinalenga kuvionya vyombo vya habari kuacha upendeleo, ushabiki na chokochoko, badala yake vijisahihishe na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari.

 

Leo asilimia kubwa ya habari zinazotolewa na kupewa aula ni malumbano ya watu kuhusu hadhi zao, misimamo yao kisiasa, nyendo zao za maisha na udidimizaji wa mila na utamaduni wa Mtanzania, badala ya kushabikia kwa uwezo wote habari za maendeleo ya uchumi wa nchi, huduma bora za jamii katika elimu, afya, maji na ushawishi wa haki, amani na upendo kwa Taifa.


Chimbuko la lawama zote hizo ni yale makundi manne ya watu niliyotaja awali. Nitaeleza. Katika vyombo hivyo, wapo wanahabari wanaojua kwamba wanajua wanachoandika na kutangaza kwa umma.

 

Hili ni kundi la kuenziwa na lifuatwe katika kazi zao. Wapo wanahabari wasiojua lakini wanajua kwamba hawajui kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha na kuwajengea Watanzania umoja na maendeleo.


Kundi hili halina budi kusaidiwa kupata weledi wa uandishi wa na utangazaji wa habari. Lipo kundi la wanaojua kuwa Watanzania wanataka maendeleo lakini hawajui kwamba wanajua kazi zao. Wanaandika na kutangaza kwa kuiga utendaji wa makundi mengine. Wanahabari hawa wanahitaji kuamshwa.

 

Wapo  wanahabari wasiojua na hawajui kwamba hawajui Watanzania wanataka nini katika ujenzi wa Taifa lao. Hawa ni hatari sana. Ndiyo wengi na wanaotangaza chuki, chokochoko na ubabaishaji. Ni kundi la kuangalia kwa makini na kuepukwa. Litaepukwa iwapo tu maswali yafuatayo yatajibiwa kwa dhati na kivitendo.

 

Ni kweli vyombo vya habari vinakula rushwa, vina makanjanja, havina weledi, vina ushabiki na upendeleo?

Tafakari. Mungu ibariki Tanzania.


1121 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!