Haki, ukweli ni nguzo za amani – 4

Katika makala tatu zilizotangulia nimezungumzia baadhi ya viongozi wa dini, siasa na wa serikali kutupilia mbali maadili na miiko ya uongozi na kuwa chanzo cha kutaka kuvunja amani ya nchi. Pili, haki na ukweli ni nguzo za amani.

Misingi mikuu ya taifa, tunu za taifa, maadili na miiko ya uongozi ni vikorombwezo vya misingi hiyo katika kustawisha amani. Amani ni hali ya usalama isiyokuwa na ghasia au fujo, au vita, ni utulivu.

 

Amani haijengwi na kubomolewa kama nyumba ya matofali. Haipandwi kama mbegu ardhini na kuvunwa kama mpunga shambani. Amani haiendeshwi kama motokaa barabarani na wala haipuliziwi upepo kama puto. Kamwe haijaribiwi kama nguo mwilini wala kuonjwa kama chumvi mchuzini.

 

Amani ni tunu na hali ya upendo na mshikamano miongoni mwa watu katika mambo yao huku wakizingatia adili bila kuwa na kasoro moyoni. Kuepuka shari na nuksani, dhuluma na batili na uhaba wa hisani. Kujaa wema na shukrani, wingi wa fadhila na amani, na wa kweli wa kauli na watendaji wa haki mbele ya dini zao.

 

Kuichezea amani ni sawa na kuchezea moto, sumu, silaha au maji kinyume cha matumizi yake. Matokeo yake ni kupoteza uhai. Ni kifo. Kifo hakina rufaa. Ndiyo maana rais wetu mara kwa mara analizungumzia jambo hili la kutunza amani na usalama wa nchi yetu.

 

Rais Jakaya Mrisho Kiwete anasema “Upendo, amani na mshakamano miongoni mwa Watanzania havina badala yake.” Anasisitiza kwa kusema “Sio mboga kama umekula njegere, kesho unaweza kula kabichi.” Hapana.

 

Rais Kikwete anakomelea na kuwanasihi Watanzania akisema “Amani haina badala yake. Badala ya amani vita. Badala ya upendo chuki, na badala ya mshikamano ni mfarakano.”

 

Rais Kikwete anathibitisha kauli yake hiyo kwa kutoa mfano hai kwa maneno yake yafuatayo: “Wote sisi ni mashahidi wa matatizo yaliyotokea hivi karibuni ya chuki baina ya Waislamu na Wakristu. Yalipoanzia hapajulikani. Ghafla tu Waislamu na Wakristu wanapigana.

 

“Kumetokea nini. nani achinje. yaa Rabii, toba! Mifumo mema maana mifumo hii haikutungiwa sheria. Haiko kwenye sheria yoyote. Lakini mababu na mababu zetu walipokaa huko wakakubaliana tufuate utaratibu huu. Nchi imekuwa na amani haina migogoro. Sasa wanakuja watu wanadhani wao wanajua zaidi. Mmeona majaribio ya kubadili mfumo. Tunauana.”

 

Nimeweka kauli hiyo ya Rais Kikwete aliyoitoa Mei mosi, mwaka huu, katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, jijini Mbeya kuonesha thamani, ubora na umuhimu wa amani.

 

Katika makala haya ya amani, nimetaja viongozi baadhi yao kutoka kwenye dini, serikali na siasa ndiyo chanzo cha kutaka kuvunja amani kutokana na kutochunga ndimi zao, kutosema ukweli na kutotenda haki kwa wananchi.

 

Hivi leo kote nchini tunashuhudia viongozi hao katika umoja wa makundi yao, wanavyolumbana maneno makali na kunyoosheana vidole, kila kundi likituhumu, likilaumu na likilalamikia kundi jingine ndiyo chanzo na mkolezo kutaka kuvunja amani. Haya ni majanga.

 

Nakumbuka wimbo wa ‘Kuku Watatu’ wa mwanamuziki wa Tanzania, Salum Abdallah (kwa sasa ni marehemu), mtunzi, mwimbaji, mpiga mandolin na kiongozi wa bendi ya Lapaloma/Cuban Marimba kuanzia 1942-1965 iliyokuwa na maskani yake mjini Morogoro.

 

‘Kuku watatu wanapigana barabarani, kuku mweupe anampiga kuku mweusi, kuku mweusi anampiga kuku mwekundu, na mwekundu anampiga mweupe. Nambieni mwenye nguvu ni nani?’ Utatu huu una falsafa nyingi ndani yake. Tafakari.

 

Viongozi wa serikali wanalaumu na kuwatuhumu viongozi wa dini, kutoa lugha za kuchochea chuki miongoni mwa waumini wa dini mbalimbali katika mihadhara ya dini. Aidha, wanalaumu na kuwatuhumu viongozi wa siasa kushawishi na kuhamasisha wananchi kufanya vurugu kwa madai ya kuishinikiza serikali kusikiliza malalamiko na kutoa haki kwa wananchi.

 

Viongozi wa siasa nao wanailaumu na kuituhumu serikali kutumia mabavu na silaha za moto kuwadhuru na kuwadhibiti wananchi wanaodai haki zao. Nao viongozi wa dini wanalaumiwa kijiingiza katika majukwaa ya siasa na kupokea fedha zinazolalamikiwa ni chafu kuendeshea shughuli za dini kutoka kwa waumini wao.

 

Viongozi wa dini wanailaumu na kuituhumu serikali kulea maovu, kupendelea baadhi ya dini na kutochukua hatua za haraka kuwatia mbaroni watuhumiwa wa mauaji ya viongozi wa dini. Aidha, viongozi wa siasa wanalaumiwa na kutuhumiwa kutosema kweli, kutoa maneno ya kashfa na matusi kwenye vikao vya kitaifa na kushindwa kutimiza ahadi zao kwa wananchi.

 

Utatu huu unayumba mbele ya macho ya wananchi wazalendo. Unatia hofu na mashaka katika mustakabali wa amani, usalama na utulivu wa Nchi. Ndiyo maana Rais Kikwete ameanza kutafuta kiini cha utatu huu kuyumba.

 

Rais anasema “Nimefanya mazungumzo na viongozi wa dini. Nimefanya na viongozi wa Waislamu, nimefanya na viongozi wa Wakristo, na sasa tunafanya matayarisho ya mkutano wa viongozi wote hao wawili au makundi hayo mawili.’’

 

Mimi nasema utatu huu haujakamilika kwa sababu viongozi wa siasa hawamo. Nashauri Rais wangu, kabla ya kukutana na viongozi wote wa dini, kwanza fanya muamala wa kukutana na viongozi wa siasa kwa maana ya chama tawala na vyama vyote vya upinzani.

 

Pili, baada ya kukutana na viongozi wote hao, tafuta wananchi wazalendo, watu wazima wenye busara, hekima na uadilifu nje ya washauri wako wa kiserikali na kichama (CCM) uzungumze nao. Nina hakika utapata mengi na mapya ambayo yanafanywa na viongozi wa utatu huu. Hapo utanusuru taifa.

 

Nakamilisha makala haya kwa wito wako Rais Kikwete. “Sasa ndugu zangu lazima tuwe tunapima, jambo gani jema, jambo gani siyo jema. Jambo gani linajenga, jambo gani linabomoa. Yale yasiyojenga yanabomoa tuachane nayo. Tushikilie yale yanayojenga, yanayotuunganisha wote, yanayojenga upendo. Yanayojenga chuki tuachane nayo. Yanayojenga mshikamano katika jamii hayo ndiyo tuyashikilie.’’

By Jamhuri