Gharama KCMC zinatisha

Serikali inajitahidi kuboresha huduma kwa wananchi wenye kipato cha chini, lakini baadhi ya hospitali haziko kwa ajili ya huduma za tiba ila ni biashara tu! Ni Watanzania wangapi wanaweza kumudu gharama za sasa za KCMC kama sio kufa kwa wagonjwa?

Mtanzania mzalendo, Moshi

Kila la heri wana JAMHURI

Mungu awajalie nguvu wana JAMHURI, mwendelee kutuhabarisha. Watanzania tutapata shule kutokana na kalamu zenu wanahabari. Baadhi ya viongozi tuliowapa dhamana ya kulinda rasilimali za nchi yetu wamegeuka watu wa kutanguliza maslahi yao binafsi.

Eng. Nyangira, Mara

 

Wanaokipoteza CCM watoswe

Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali viwafukuze vigogo wake wachache ambao wanachangia kwa kiasi kikubwa kukipotezea chama hicho mwelekeo mzuri.

Mpenzi wa CCM, Mtwara

 

Viongozi wachunge ndimi zao

Viongozi wa serikali na vyama vya siasa Tanzania wachunge ndimi zao. Waepuke kutoa kauli kali zinazoweza kuchochea hasira na chuki ya wananchi dhidi ya serikali na vyama vyao.

Maulidi, Lindi

 

Waziri Mkuu amekurupuka

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amekurupuka kutoa kauli inayolipatia Jeshi la Polisi nguvu ya kutembeza kipigo ovyo kwa wanasiasa na wananchi kwa jumla. Ninamshauri awe anafikiri kabla ya kutoa matamshi.

Mpenda amani, Pwani

 

Waliomvamia Machali walaaniwe

Raia wema na Watanzania wapenda amani kwa jumla tuungane kuwalaani   kwa nguvu kubwa vibaka waliomvamia Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali, wakampiga na kumpora simu ya kiganjani. Mungu amjalie apone haraka, amina.

 

Simon B, Kigoma

 

Waliotupa bomu waadhibiwe

Vyombo vya dola viwajibike ipasavyo kwa kuhakikisha vinawasaka, kuwatia mbaroni na kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote waliohusika kulipua bomu lililoua na kujeruhi watu kadhaa mkoani Arusha.

Gladness Kimaro, Moshi

 

Bajeti ituletee unafuu

Bajeti ya Serikali inayopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania izingatie kuwaletea Watanzania unafuu wa maisha katika kipindi hiki kigumu cha mfumko wa bei za bidhaa hapa nchini.

Kulwa, Dodoma

 

Please follow and like us:
Pin Share