Mandela  ataenziwa au atakumbukwa?

Ni muda wa wiki tatu sasa, dunia imepata mzizimo na simanzi kutokana na kifo cha mtoto wa Afrika, shujaa, mpenda haki na usawa na kipenzi cha dunia, mtoto huyo ni Nelson Mandela. “Madiba.”

Mandela hayupo duniani, na kamwe hatutamuona tena katika umbile lake halisi la kibinadamu wala kusikia sauti yake hai na tamu inayorindima na dhana za huba, busara na nasaha. Achilia mbali msimamo wake wa kusamehe waliomkosea.

Madiba ametangulia mbele ya haki. Wala hakufanya kosa. Hata mimi na wewe tutakwenda huko. Ni lazima. Kumbuka hata wazazi wake walikwisha mtangulia; na leo, yeye amewafuata, lakini hatawaona. Ni mapenzi ya Mungu.

Wewe na mimi tungependa tuendelee kuwa naye. Afrika na dunia ingependa kuendelea kumlea, kumtunza na kumliwaza, lakini Mwenyezi Mungu amempenda zaidi yetu. Amemchukua.

“Baba wa milele, mpokee katika makao yako ya milele mtumishi wako uliomwita kutoka kwetu, Baba wa Afrika na kipenzi cha umma.” Amin!

Kusema ukweli nilijipurukusha kutoandika neno lolote kuhusu kiongozi wangu, masha’allah Nelson Mandela kwa sababu watu wengi wameandika habari zake. Lakini purukushani zangu hazikufua dafu. Imenibidi kushika kalamu na kuandika.

Dunia ni ukumbi mpana wenye kila tendo la raha na karaha. Wenye vitamu na vichungu. Uliojaa mapenzi na maovu, furaha na huzuni. Yote hayo Mandela ima ameyaona, ameyasikia au ameyatenda. Hatimaye ameyapa kisogo na dunia bado yamuhitaji.

Tangu Desemba 5, 2013 mara tu taarifa ya kifo chake kutangazwa, hadi leo, waandishi kadha  wa kadhaa wameandika na kusimulia kuhusu nasaba, makuzi, tabia, sifa, hadhi na uadilifu enzi za uhai wake.

Jumapili, Desemba 15, 2013 Nelson Mandela amezikwa kijijini kwake Qunu katika Jimbo la Cape Mashariki kwenye makazi yake ya milele. Maombolezo yataendelea na maadhimisho ya kumbukumbu zake yatafanywa na kizazi cha leo na vijavyo.

Si nia yangu kukujaza maumivu na majonzi makali kuhusu hayati, isipokuwa nimetingwa na hoja nzito na kujiuliza, Mandela ataenziwa au atakumbukwa na watu waliomfahamu, waliofanya kazi naye au waliomsikia?

Nauliza hivyo kwa sababu baadhi ya viongozi, watendaji na watumishi duniani na hasa Afrika, wameonekana na kusikika wakilia kwa uchungu, na kumjaza sifa njema kemkem na kusema, “tuyaenzi mambo yake mema.”

Viongozi hao wametukumbusha na kutusisitiza, kujifunza kutoka kwa Mandela tabia ya kusamehe. Kutenda haki na kujali usawa.

Mandela si kiongozi mwadilifu wa kwanza wa Afrika kufariki dunia. Wapo wengi waliomtangulia katika kundi lao la kupigania uhuru, haki, umoja na usawa. Wao ni viongozi wakombozi wa mwafrika wa leo.

Baadhi yao ni Kwame Nkrumah wa Ghana, Modibo Keita wa Mali, Gamal Abdel Nasser wa Misri, Sir Abubakar Tafawa Balewa wa Nigeria na Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania. Wote hao wametufunza suala la uzalendo na ukombozi wa Mwafrika.

Je, viongozi wetu wa Afrika ya leo, wanaenzi kauli na matendo hayo yenye busara, uzalendo, haki na usawa? Au wanakumbuka visa na vitimbi vya baadhi ya viongozi wachache vya kufanya maovu, mauaji, na kuwa matajiri na kuishi kifahari?

Kumbukumbu bado zinatuonesha Afrika na watoto wa Afrika bado maskini. Lau kama juhudi zilifanywa na viongozi tangulizi za kupata uhuru kututoa utumwani na kutukomboa kifikra na kiuchumi. Afrika bado inahujumiwa.

Wakati tunaendelea kuomboleza kifo cha Nelson Mandela, naunga mkono kauli ya aliyekuwa Katibu Mtendaji wa tatu wa Kamati ya Ukombozi wa Bara la Afrika, Brigedia Jenerali Hashim Mbita, alipozungumza na JAMHURI wiki iliyopita.

Nanukuu, “Mandela ni aina ya viongozi ambao Afrika ilikuwa inawazalisha zamani. Naweza tu kusema kwamba joto lile la kunyonywa, kubaguliwa na utumwa ndilo  lililozalisha viongozi waliokuwapo wakati huo.  Sasa hivi wamekuwa adimu kwa sababu joto lile lililowapika akina Mandela, Nyerere, Kaunda na wengine halipo tena.

“Tusijaribu kulinganisha viongozi wa zamani na wa sasa. Mazingira ni tofauti. Joto lililopo sasa hivi la utandawazi, teknolojia uzalendo na umajumui wa Afrika ndilo hilo hilo linalotakiwa kuwapika viongozi wetu wa kizazi kijacho” mwisho wakunukuu.

Maelezo hayo kwa mtazamo wangu yanakumbusha viongozi wetu wa leo kuandaa viongozi wajao katika mazingira yaliyopo kama walivyoandaliwa wenzao. Pili waoneshe uzalendo wao katika harakati za kulinda, kugawa na kutumia rasilimali za Afrika kwa haki na usawa.

Wazalendo wa Afrika tuko tayari kusamehe. Je, viongozi  wetu wako tayari kuacha mali? Huko ndiyo kusamehe

1364 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!