FC Lupopo yasifu wachezaji wa Tanzania

*Huenda Kaseja akasajiliwa huko

Katika hali inayoonesha kuwa wanandiga wa Kitanzania wanaosakata kabumbu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wanakubalika, Klabu ya Soka ya FC Lupopo imesema wachezaji kutoka Tanzania wanapendwa nchini humo kutokana na uwezo wao kisoka.

Hivi karibuni, kiongozi wa timu hiyo, Balanga Ismail, alitua hapa nchini kufanya mazungumzo na golikipa namba moja wa Timu ya Taifa kwa ajili ya kumsajili.

 

Alisema wachezaji wa Tanzania ni wazuri na wana uwezo kisoka, akitoa mfano wa mchezaji Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa nchini humo katika klabu ya TP Mazembe. Mchezaji mwingine anayechezea timu hiyo ni Thomas Ulimwengu.

 

Kiongozi huyo alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema wachezaji wa Kitanzania wanapendwa sana nchini DRC, na ndiyo maana amekuja hapa nchini kufanya maongezi na Kaseja ili aweze kusajiliwa na timu yao ya FC Lupopo.

 

Alimsifia Kaseja kwa kusema kuwa ni golikipa mzuri ambaye wamemfahamu kwa muda mrefu, na hivyo, endapo watamsajili ataweza kufanya vizuri katika timu yao.

 

“Tumemfahamu Kaseja muda mrefu na wachezaji wa Tanzania tunawapenda kwa sababu wanajituma, tumeona mfano wa Samatta anayechezea TP Mazembe,” alisema kiongozi huyo.

Kauli ya FC Lupopo inadhihirisha kuwa Tanzania kuna vipaji vya soka, lakini huenda mipango iliyopo katika kuvikuza na kuviendeleza ndiyo haiwapi vijana nafasi ya kuvionesha, ili hatimaye waweze kufikia hatua kama ya akina Samatta na Ulimwengu, ambao sasa wanafanya vizuri katika ulimwengu wa soka.

Samatta na Ulimwengu wamekuwa na mchango mkubwa katika timu ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) katika mechi kadhaa za kimataifa.

Ulimwengu ni matunda ya mpango maalum wa kukuza soka unaoendeshwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), wenye lengo la kukuza vipaji vya mchezo huo.