Prodyuza anayetamani  kumiliki kituo cha redio

Imekuwa jambo la kawaida kwa vijana wengi kukaa vijiweni, kwa kisingizio kuwa Serikali imeshindwa kuwapatia ajira.

Lakini kwa upande wake, Kelvin Christopher anayefahamika kwa jina la utani la ‘Kiba Gita’, mkazi wa Dar es Salaam, ni kijana aliyejikwamua na kukataa maisha ya kukaa vijiweni.

Kwa sasa anamiliki studio ya kurekodi muziki inayojulikana kama Kausha Records Music iliyoko Kinondoni, Dar es Salaam. Yafuatayo ni mahojiano maalum kati yake na JAMHURI akielezea jinsi alivyoweza kujikwamua kimaisha.

 

JAMHURI: Kwanza kabisa kwanini watu wanapenda kukuita Kiba Gita wakati wewe jina lako halisi ni Kelvin Christopher?

 

Kiba Gita: Ni kwa sababu zamani nilikuwa napendelea kupiga gitaa.

 

JAMHURI: Ni kitu gani kilichokusukuma kufanya biashara hii ya utengenezaji wa muziki?

 

Kiba Gita: Baada ya kumaliza masomo yangu ya Teknolojia ya Mawasiliano (IT) katika Chuo cha Technobrain mwaka 2010, sikuona haja ya kusubiri ajira, badala yake nikaangalia jinsi ya kuweza kujiajiri. Kwa haraka haraka niliwaza kutumia elimu yangu kujiajiri mwenyewe, ndipo nikafungua studio ya kurekodi muziki na kuipa jina la Kausha Records Music. Kuna watu walioniongezea ujuzi katika taaluma hii, kwa mfano John Mabula na jamaa mwingine anayeitwa Roy, hawa wote ni maprodyuza wa muziki.

 

JAMHURI: Watengenezaji wengi wa muziki hapa Tanzania utakuta ni wanamuziki au wana historia ya kuimba muziki? Wewe hili kwako likoje?

Kiba Gita: Awali nilikwambia kuwa jina ka utani la Kiba Gita, ni kwa sababu ya kupenda kupiga gitaa. Kwa hiyo, mpaka hapo una jibu kuwa hata mimi ni mwanamuziki pia. Kazi hii inapendeza zaidi ukiwa mwanamuziki kwa sababu inakuwa rahisi kumwelekeza msanii cha kufanya wakati wa kurekodi.

 

JAMHURI: Studio za siku hizi zina ushindani wa kila hali, kitu gani ulichonacho na unafikiri wengine hawana?

 

Kiba Gita: Kwanza kabisa nina elimu, kitu ambacho kinanipa ufahamu wa kujua ni kitu gani ninakifanya. Jambo la pili nina vitendea kazi vya kisasa vya kutengeneza kazi yenye viwango vinavyokubalika. Jambo jingine nina upendo, ninawaheshimu wateja wangu na kuwapa msaada wa ziada pale inapohitajika. Hata kama utakuwa na studio kubwa kiasi gani yenye mitambo ya kisasa, lazima uwaheshimu wateja wako na kuwathamini, hali kadhalika kuwapa maelekezo ya ziada ambayo yatawapeleka katika kilele cha mafanikio.

 

JAMHURI: Nitajie kazi ambazo umekwishazifanya katika studio yako.

Kiba Gita: Zipo nyingi ila naweza kukutajia baadhi kama vile ya Makomando wa THT, Harmonise ya Q Chief, wimbo wa Jose Mtambo, Wimbo wa Z-Anton na wimbo wa Kisungura wa Tip Top Connection. Hizi ni baadhi tu ila zipo nyingi. Studio yangu pia imekuwa ikipata kazi ya kutengeneza na kurekodi baadhi ya matangazo kwa ajili ya kurushwa redioni.

 

JAMHURI: Kuna wanamuziki ambao wana imani kuwa lazima avute bangi kwanza ndiyo aingie studio kurekodi, na kwako wanafanya hivyo?

Kiba Gita: Bangi haisadii chochote. Hizo ni imani za hao wanaotumia, na katika studio yangu sikubaliani na vitendo vya namna hiyo. Na kama utakutana na mwanamuziki anayetegemea nguvu ya bangi, basi hapo hamna kitu.

 

JAMHURI: Unasemaje kuhusu vijana wanaokaa vijiweni kwa kisingizio kuwa Serikali imewanyima ajira?

 

Kuna haja ya kuacha tabia hii na kujishughulisha. Hakuna mafanikio ambayo kijana anaweza kuyapata kupitia kijiweni, njia pekee ni kila kijana kujishughulisha kadiri ya upeo wake.

 

JAMHURI: Ni prodyuza gani ambaye unampenda?

 

Kiba Gita: Nampenda sana P Funk, ninatamani kufikia kiwango chake katika taaluma hii ya kutengeneza muziki.

 

JAMHURI: Nini matarajio yako kwa siku za baadaye?

 

Kiba Gita: Nataka kuwa msanii bora na prodyuza mkali. Lakini nina ndoto ya kumiliki kituo cha Redio, ambacho kama Mungu akipenda nikifungue kule Bagamoyo katika shamba langu.

 

JAMHURI: Unaonaje uhusiano uliopo kati ya wanamuziki na watangazaji wa redio?

 

Kiba Gita: Mahusiano ni mazuri ila tatizo ni kwamba nyimbo za wanamuziki wanaochipukia hazipigwi sana kama ilivyo kwa wale wanamuziki maarufu. Staili hii inachangia kuua vipaji vya wanamuziki chipukizi.

 

JAMHURI: Kuna changamoto gani katika biashara hii?

 

Kiba Gita: Changamoto zipo. Kuna wasanii wengine wana uwezo mdogo na hivyo hutumia muda mwingi kurekodi wakiwa studio na wengine pia ni wabishi. Kuna suala la malipo kwa baadhi ya wasanii. Narudia kusema kuwa changamoto kubwa zaidi ni ile ya watangazaji kutopiga nyimbo za wasanii chipukizi redioni. Hii inaua vipaji kwa sababu hata hao maarufu walikuwa huko huko.

 

1371 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!