Watanzania na imani potofu ziara ya Obama

Ziara ya Rais wa Marekani, Barack Obama, hapa Tanzania imenilazimu kuleta mada hii mapema tofauti na nilivyokusudia awali. Watanzania wengi wamezungumza ya moyoni mwao kuhusu ugeni huu.

Binafsi nimeshuhudia na kusikia watu mbalimbali katika maeneo tofauti hapa nchini, wakijadili na kuanika wazi mitazamo, imani na hisia zao kuhusu ujio wa kiongozi huyu.

 

Baadhi ya wananchi wanahisi kuwa Rais Obama amekuja kumilikishwa rasilimali muhimu za nchi yetu. Wengine wanaamini anasaka vibali vya kuwekeza katika sekta za madini na utalii. Imani na hisia za aina hii zinadhihirisha kuwa Watanzania wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya kidiplomasia. Hawaoni umuhimu wa taifa letu kuanzisha, kujenga na kuendeleza uhusiano na mataifa mengine.

 

Inapofikia hatua mtu akahisi kinyongo na kuchukia kuona na kusikia viongozi wa mataifa mengine wanazuru hapa Tanzania, basi huyo tunaweza kumfananisha na mtu mwoga na mbinafsi asiyependa kujichanganya na wengine. Ni mtu asiyelitakia taifa letu mema, anayependa kujitenga katika kisiwa cha peke yake mambo yake yasifahamike na yeye asijue yanayofanyika kwa wengine.

 

Ziara ya Rais wa Marekani hapa Tanzania ni kielelezo cha uhusiano na uelewano baina ya wananchi wa mataifa haya. Kuna nchi katika dunia hii zinazotafuta kwa udi na uvumba kutembelewa na viongozi wa mataifa makubwa bila mafanikio.

 

Marekani ni taifa lenye nguvu kubwa za kijeshi na kiuchumi kuliko mengine yote duniani. Ni taifa lililoendelea. Tanzania kama nchi changa inayoendelea inahitaji kujifunza mengi kutoka taifa hili. Hatuwezi, kwa mfano, kukuza uchumi wetu bila kujua mbinu zilizotumiwa na vinara wa uchumi imara duniani ikiwamo Marekani.

 

Hivi karibuni, nchi yetu ilipata bahati nyingine ya kutembelewa na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping. Tanzania imejifunza mengi ya maana kutoka China kupitia kwa kiongozi huyo na ujumbe aliofuatana nao.

 

Leo kiongozi wa taifa la Marekani mwenye asili ya Afrika yupo hapa nchini kwetu. Wafanyabiashara wenye hoteli na nyumba za kulala wageni hapa kwetu watapata neema ya kuvuna fedha za kigeni kutoka kwa Rais Obama na ujumbe aliofuatana nao. Hili nalo baadhi yetu hawalioni, wananung’unika na kuumia mioyoni.

 

Kwanini tuhofu na kuogopa? Rais Obama pamoja na nchi yake kuwa na uwezo mkubwa wa kijeshi hawezi kujitwalia rasilimali zetu. Nimesikia mengi yakisemwa kuhusu ziara ya Rais Obama lakini nafsi inanisukuma kuzungumzia kauli ya mmoja. Huyu tulikutana naye kwenye daladala jijini Dar es Salaam wiki moja kabla ya kiongozi huyu wa Marekani kutua hapa.

 

Alisema, “Hawa marais Wazungu wameizoea Tanzania, wanakuja kukomba madini na wanyama wetu. Bush [Rais mstaafu wa Marekani, George W. Bush] alikuja akatudanganya na vyandarua lakini alivyoondoka navyo ni siri yake na vigogo wa nchi hii.”

 

Ukisoma na kusikiliza kwa makini maneno hayo utabaini kuwa ndugu yetu huyu amegubikwa na mawazo mgando kama si imani potofu kuhusu ziara za viongozi wa Marekani, na hata mataifa mengine hapa nchini.

 

Jamaa huyu kwanza, anaamini kimakosa kuwa marais wa Marekani miongoni mwa mataifa mengine huwa wanakuja hapa Tanzania kuchukua mali za Watanzania. Lakini pia, amejenga dhana potofu kuwa kila rais anayezuru hapa kwetu anapaswa kuja na misaada mikubwa, ndiyo maana ‘ameponda’ msaada wa vyandarua.

 

Hisia na mitazamo hasi kama hiyo, haiwezi kutuonesha mwanga wa kupata ufumbuzi wa matatizo yanayoendelea kuhuisha umaskini kwa Watanzania wengi. Hebu tusiogope, tuthubutu na kuwa tayari kukutana na kuchanganyikana na watu wa mataifa mengine, hususan yaliyoendelea kama Marekani tuvune siri ya kukuza na kuimarisha uchumi.

 

Hivi, kwa mfano, tutajisikiaje nchi yetu isipotembelewa na viongozi wa mataifa mengine? Je, hatutajiona tuko kisiwani na wenye dosari ya kukosa uhusiano na mataifa mengine? Umefika wakati Watanzania tujiamini katika zama hizi za ushindani mkubwa wa masuala ya uchumi na diplomasia duniani.

 

Hatuwezi kupiga hatua ya maendeleo tunayohitaji kama tutaendelea kukumbatia imani potofu kwamba marais wa mataifa mengine likiwamo Marekani wanazuru hapa Tanzania kwa nia ya kumiliki na kuondoka na rasilimali zetu. Nasema hatuwezi.

 

1287 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!