Tindikali imetuchafua,  kauli za polisi ni zilezile

Wiki iliyopita, nchi yetu ilipata doa lenye taswira ya kuichafua mbele ya uso wa Dunia. Raia wawili wa Uingereza, Kate Gee (18) na Kirstie Trup (18) walikumbwa na mkasa wa kumwagiwa tindikali huko Mji Mkongwe, Zanzibar.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi kama ilivyo mazoea yake limeahidi kwamba litahakikisha linawasaka watu waliotenda unyama huo na kuwashughulikia kisheria. Rais Jakaya Kikwete naye amewahimiza polisi kufanya hivyo.

 

Lakini, hii siyo mara ya kwanza wala ya pili kwa Jeshi la Polisi kutoa tambo za kuwatia nguvuni watuhumiwa wa matukio ya uhalifu hapa nchini. Kauli za aina hiyo mara nyingi zimekuwa mithili ya nguvu ya soda, zimekuwa zikiishia kuyeyuka.

 

Wengi hatujasahau kwamba makamanda wa polisi wamepata kuahidi mara nyingi kuwasaka na kuwakamata haraka watuhumiwa wa uhalifu. Lakini idadi kubwa ya ahadi hizo imeishia patupu.

 

Waliahidi kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya habari watekaji na watesaji wa Dk. Steven Ulimboka, Absalom Kibanda na wengine wengi. Matokeo yake mpaka sasa wako kimya kana kwamba hawajui Watanzania wanasubiri kusikia na kuona utekelezaji wa ahadi hizo.

 

Sasa kwa mara nyingine tena Jeshi la Polisi limetoa maneno yaleyale ya kwamba litahakikisha linawakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watu waliohusika kuwamwagia raia wa Uingereza tindikali. Ingawa bado ni mapema kuhukumu lakini uzoefu tuliojifunza katika jeshi hilo kwa miaka mingi sasa unatusukuma wengi kuamini kuwa hata ahadi hiyo huenda itayeyuka.

 

Upungufu huo unaojidhihirisha ndani ya Jeshi la Polisi sio kwamba halina uwezo wa kuwasaka na kuwafikisha wahalifu kwenye vyombo vya sheria. Uwezo huo linao ila halina dhamira ya kweli. Taswira hiyo ndiyo wakati mwingine huwashawishi watu kuamini kwamba baadhi ya askari polisi wanashirikiana na wahalifu kula njama za kufanya uhalifu.

 

Jeshi la Polisi linapowaahidi wananchi kwamba litawasaka na kuwashughulikia wahalifu kwa uzito unaostahili lakini mwisho wa siku linakaa kimya, linajipunguzia heshima na uaminifu mbele ya umma. Hatuwezi kufurahia ahadi hewa zinazotolewa na vyombo vya dola juu ya matukio yanayoacha mateso makubwa miongoni mwa jamii.

 

Ni ukweli usiopigika kuwa tukio la kuwamwagia wasichana hao wa Uingereza tindikali wakiwa katika harakazi zao za kujitolea kufundisha watoto na vijana wetu Kiingereza limeipaka nchi yetu matope mbele ya uso wa Dunia. Ingefaa Jeshi la Polisi lichukulie tukio hilo kwa uzito mkubwa. Lifanye kweli kwa kuwasaka na kuwashitaki wahalifu husika ili angalao kuionesha Dunia kuwa Watanzania tumechukizwa kitendo hicho.

 

Hatuwezi kusema kwamba Jeshi la Polisi linaundwa na malaika wa mbinguni, la hasha! Ni jeshi linaloundwa na watu ambao hatuwezi kupinga kwamba miongoni mwao wamo wachache wasio waadilifu na waaminifu, wanaojitahidi kukwamisha juhudi za wengine wenye dhamira ya kweli ya kudhibiti uhalifu.

 

Rais wetu mara baada ya matukio makubwa ya uhalifu kutokea amekuwa akiviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwasaka wahalifu na kuwafikisha katika vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo. Hata hivyo, wengi hatuna uhakika kama kiongozi huyo wa nchi amekuwa akifuatilia kuhakikisha maagizo yake yanatekelezwa, na kama hayatekelezwi anachukua hatua gani dhidi ya walioshindwa kuyatekeleza.

 

Pengine mazoea ya Jeshi la Polisi ya kutoa ahadi hewa mbele ya umma yanaimarishwa hapa nchini ama na uoga, au udhaifu wa viongozi wa ngazi za juu wanaopaswa kuhakikisha chombo hicho cha dola kinawajibika kuwatumikia wananchi kwa kiwango cha kuridhisha.

 

Wahenga walisema kwamba muungwana ni kitendo. Watanzania tungependa kusikia na kuona Jeshi la Polisi linatekeleza ahadi zake kwa vitendo. Wahalifu wengi pengine hawaoni sababu ya kuacha uhalifu kwa kuwa wanaona jeshi hilo halijadhamiria kwa dhati ya moyo kuwashughulikia wahalifu na kukomesha uhalifu hapa nchini.

 

Matukio ya wananchi kutekwa, kuteswa, kuuawa, kumwagiwa tindikali na kujeruhiwa vibaya, miongoni mwa mengine yanaendelea kushika kasi hapa nchini. Matukio hayo yanatishia kuibadili Tanzania kutoka kisiwa cha amani kuwa mahali pasipo salama kwa kuishi.

 

Umefika wakati Jeshi letu la Polisi litambue kwamba ndicho chombo pekee kilichobeba dhamana kubwa ya kulinda usalama wa raia na mali zao katika taifa hili. Jeshi hili lijenge tabia ya kusimama kwenye ahadi zake. Liwajibike kusaka na kuwakamata watenda maovu wote wachukuliwe hatua za kisheria. Liache kauli za nguvu ya soda na ahadi hewa.

1048 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!