Kama tujuavyo, Serikali ya leo ya Tanzania ni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ni sawa na kusema kwamba Serikali ni mtoto wa CCM.

Serikali ikifanya vizuri CCM inapata sifa nzuri na itaendelea kuchaguliwa kuwa chama tawala. Isipofanya vizuri wananchi watachagua chama cha upinzani kitawale. Hilo si jambo lisilowezekana.

 

Haijulikani Serikali inajua kwa kiwango gani ukweli huo. Nionavyo mimi haijui. Serikali ya leo haiwajali watu wake. Inajali zaidi maendeleo ya vitu kuliko watu. Kumbe ni watu wanaoiweka madarakani.

 

Kila mtu anajua kuwa wakazi wa Dar es Salaam, watu wa kawaida, wameendelea kukumbwa na tatizo la maji. Hali imekuwa zaidi baada ya kufutwa kwa Azimio la Arusha ikizingatiwa kuwa kipindi hicho huduma za maji, afya na elimu zilitolewa bure kwa wananchi wa kawaida.

 

Leo unakuta akina mama wa kawaida wanahangaika kando ya Mto Msimbazi kutafuta maji ya matope. Na ukitaka kusema kweli tatizo la maji haliko Dar es Salaam pekee. Liko pia mikoani, hasa vijijini.

 

Wapinzani wamekaa kimya. Lakini hawakukaa kimya kabisa. Wanasuburi mwaka 2015. Watawaahidi wakazi wa Dar es Salaam kuwaletea maji safi wakati Serikali itakapojitapa imejenga barabara ya kisasa.

 

Katika mazingira hayo wananchi watachagua maji ambayo Serikali haikujali kuwaletea. Ndiyo maana inasisitizwa kuwa Serikali imejipanga kuiangusha CCM.

 

Tazama! Majuzi Bill Clinton, Rais mstaafu wa Marekani, alikuja Dar es Salaam na akafanya ziara katika makazi ya watu wa chini eneo la Vingunguti, Wilaya ya Ilala. Huko alikagua miradi midogo midogo ya wananchi wa hali ya chini inayofadhiliwa na mfuko wake (Bill Clinton Foundation).

 

Wananchi walishangilia kuona mtu mkubwa kama huyu kutoka nchi nyingine anaingia mitaa ya watu maskini na kuzungumza nao. Walimweleza pia kwamba tangu alipowafadhili hawajatembelewa na kiongozi wa juu serikalini. Hawana muda wa kutembelea mitaa ya maskini.

 

Ni aibu kubwa kwa Serikali kushindwa kufuatilia miradi inayofadhiliwa na watu wa nje wenye nia njema na wananchi wa kawaida wa nchi hii. Ni juu ya Serikali kuwatia moyo wananchi wanaofadhiliwa na kuhakikisha kuwa wanafanya vizuri ili mfadhili anapofuatilia miradi aliyoifadhili aridhike na aendelee kuwasaidia Watanzania maskini. Kwa hiyo, Serikali haiwatakii mema maskini wa Tanzania.

 

Tazama! Dawa za kulevya zilivyosababisha maelfu ya vijana Watanzania kupata vifungo nchi za nje. China peke yake ina vijana wetu 176 wanaotumikia vifungo.

 

Sababu ni kwamba Serikali ya Tanzania haikuchukua hatua madhubuti za kudhibiti biashara ya dawa za kulevya mbali ya madai kuwa tuna kikosi cha kupambana na dawa hizo. Leo Tanzania imekuwa soko kuu la dawa za kulevya barani Afrika! Inatisha!

 

Imebainishwa kuwa uchochoro mkubwa wa kuvusha dawa za kulevya ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. Pale watoto wa wakubwa, matajiri, wabunge na wanasiasa wengine wanapitisha dawa za kulevya. Hawapitishi njia za panya. Wanazipitisha pale baada ya kutoa rushwa. Na bila shaka Serikali yenye watu wa Usalama wa Taifa inajua hivyo. Lakini imeruhusu iwe hivyo.

 

Huko nyuma, watu wanaoitakia mema Tanzania waliwasilisha serikalini orodha ya wafanyabiashara ya dawa za kulevya. Serikali ikakaa kimya. Kama kukaa kimya hakukuwa na maana ya kubariki biashara ya dawa za kulevya mimi sijui kilikuwa kitu gani.

 

Sasa kijana Mtanzania anayesota gerezani nchini Hong Kong kaleta orodha ya wafanyabiashara ya dawa za kulevya na mitaa yao. Serikali isipowachukulia hatua ya wazi watu hao, basi ijue inaendelea kujipanga kuiangusha CCM. Watachagua Serikali itakayopambana na dawa za kulevya.

 

Watanzania walio wasomi wengi hawataki dawa za kulevya. Dawa za kulevya zimeharibu tabia na afya za watoto wao. Dawa za kulevya zimewaletea watoto wao vifungo na vifo. Dawa za kulevya zimeendelea kuchangia maendeleo ya rushwa. Juu yake dawa za kulevya zimeharibu kwa kiasi kikubwa sifa ya Tanzania duniani kote.

 

Nina hakika hata rafiki yetu Marekani hafurahishwi na hili. Siku moja wauza dawa za kulevya watatawala nchi hii kama bado hawajaanza kutawala.

 

Tazama! Kuna tatizo la muda mrefu la watoto wa mitaani na ombaomba. Tuliposikia Rais wa Marekani, Barack Obama, anakuja tuliwakusanya hao wote tukawaficha mahali ili aone kuwa nchi hii haina watoto wa mitaani wala ombaomba.

 

Obama amekwenda zake Marekani nao watoto wa mitaani na ombaomba wamekwenda zao mitaani na barabarani kuwasumbua watu wenye magari ikiwa ni pamoja na wageni. Ombaomba wengi wanashinda kwenye mahekalu ya Wahindi ambako hapana shaka kule mtu mweusi anadhalilishwa.

 

Idara ya Ustawi wa Jamii ambayo ni sehemu ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ni kama haipo. Hata halmshauri za manispaa ni kama hazipo. Hakuna anayetembea mitaani.

 

Leo kila baada ya hatua kumi unamkuta ombaomba na mara nyingi ni mlemavu mwenye mikono inayoweza kufanya kazi. Pale kando ya Kanisa la Mtakatifu Albano  ni makao makuu ya ombaomba anayelala hapo. Asubuhi wageni wanamkuta pale. Serikali inawatia aibu Watanzania.

 

Hata waliokuwa mashabiki wa Serikali ya CCM sasa ni mashabiki wa wapinzani. Wameichoka Serikali ya CCM inayoendelea kujipanga kuiangusha CCM mwaka 2015.

 

Tazama! Serikali ya leo imegeuza utamaduni wa Tanzania kuwa biashara. Ni sehemu ya Wizara ya Maliasili na Utalii! Kijiji cha Makumbusho kilichoko Kijitonyama, Dar es Salaam, leo kimekuwa kijiji cha ngono. Pombe zinazouzwa pale ni za Kizungu. Marufuku kuuza pombe za Afrika. Muziki unaotawala pale ni wa Congo kana kwamba Tanzania imekosa muziki wake. Serikali imetuangusha!

 

Serikali ya Tanzania imeifikisha CCM pabaya. Imekosa uzalendo na haijali watu wake. Hakika imejipanga vizuri kuiangusha CCM 2015.

952 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!