Bunge likipata Lugola 10 litainyoosha Serikali yetu

Ninatamani kuona siku moja Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linafanikiwa kuwa na angalau wabunge 10 aina ya Alphaxard Kangi Ndege Lugola, ambao watatosha kuinyoosha Serikali yetu.

Lugola, Mbunge wa Jimbo la Mwibara mkoani Mara kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni mfano mzuri wa watu wanaostahili kuwakilisha wananchi bungeni.

Lugola siku zote amekuwa jasiri wa kutekeleza alichotumwa na wananchi wa Jimbo la Mwibara kwenda kukifanya bungeni, lakini pia kupaza sauti ya kukemea vitendo viovu serikalini ukiwamo ufisadi unaohusisha matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za umma.  Amekuwa hodari wa kusimamia ukweli bila kujali kuburuzwa na chama chake.

Mwenyewe amekuwa akisisitiza kwamba dhamira safi ya CCM ndiyo inayomwongoza kutetea maslahi yatakayowanasua Watanzania wengi kwenye lindi la umaskini.

“Nina imani na chama changu, nina imani na Rais Kikwete ambaye nahisi naye amechoshwa na mafisadi ambao siyo sera ya CCM,” amepata kusema mbunge huyu.

Lugola ambaye ni askari aliyepata kuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Magomeni, Dar es Salaam, kabla ya kustaafu mwaka 2000, ni mchumi aliyepata pia kuwa mtumishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kati ya mwaka 2002 na 2010.

Uchaguzi Mkuu 2010 ndiyo uliomwezesha Lugola kuingia bungeni. “Niliacha kazi polisi saa 24, lengo likiwa ni kuwasaidia Watanzania wenzangu,” anasema Lugola. Pamoja na juhudi nyingine, mbunge huyu wa Mwibara atakumbukwa na umma kutokana na msimamo wake wa kupinga waziwazi hoja za Serikali zinazohusu bajeti na mipango isiyowezesha ufumbuzi wa matatizo lukuki yanayowanyima Watanzania maendeleo ya kweli.

“Hapa tunapiga kelele kupitisha bajeti tukienda kwenye halmashauri fedha hakuna, wafadhili hawajaleta, kwani tulidai Uhuru kutegemea fedha za wafadhili?” Lugola alipata kuhoji bungeni. Pia alipata kusisitiza; “Sisi tunaopinga baadhi ya bajeti za wizara ndiyo tunaojua uchungu wa chama chetu [CCM] kwa sababu tunataka kiendelee kubaki madarakani, lakini hao wanaopitisha pamoja na madudu si wema kwa chama hata siku moja, watakosa majibu siku ya mwisho.”

Inakumbukwa kwamba Lugola alipata kuunga mkono hoja ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutokana na kilichoelezwa kuwa alishindwa kuwawajibisha mawaziri wazembe na wabadhirifu wa fedha za umma. Wabunge wengine wanachama wa CCM walioungana na Kambi ya Upinzani Bungeni kutia saini hoja hiyo ni Nimrod Mkono wa Jimbo la Musoma Vijijini na Deo Filikunjombe wa Jimbo la Ludewa.

Pia Lugola ni miongoni mwa wabunge wachache wa CCM waliopata kuwashambulia mawaziri waliopata kutuhumiwa kwa ufisadi hapa nchini, na kuishauri Serikali iwawajibishe bila huruma ili iwe onyo kwa wengine wenye nia ya kutenda uovu huo.

“Wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waliongezewa mishahara ili wasichukue rushwa, kwanini Serikali inapata kigugumizi kuongeza mishahara ya polisi?” Kauli hii ilitolewa na Lugola bungeni, ambapo alisisitiza kutounga mkono hoja kutokana na Serikali kutochukua hatua ya kuanzisha mfuko maalum wa kuboresha maslahi ya askari polisi.

Nakumbuka kuna wakati Lugola alipaza sauti bungeni kutaka mamilioni kadhaa ya dola za Marekani yarejeshwe mara moja serikalini, baada ya kudaiwa yalihujumiwa kupitia kampuni ya uwekezaji ya PAT, inayofanya kazi kwa niaba ya kampuni ya Songas ya Canada, ambayo iliingia mkataba na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa niaba ya Serikali katika kuzalisha gesi kutoka Songosongo, Mnazi Bay na Bahari ya kina kirefu.

Kwa upande mwingine, mbunge huyu alipata kuweka historia bungeni pale alipojifananisha na mhubiri na kuliomba Bunge nafasi ya kubandika picha ya kero ya maji bungeni, ambayo aliiita kuwa ni mfano wa nyoka wa shaba. Aliwataka wabunge wanapojadili suala la maji kutazama nyoka huyo wa shaba kwa imani ya kufikia ufumbuzi wa kero ya maji hapa nchini.

“Sikuingia bungeni kwa maslahi binafsi, hii ni kwa sababu nasimamia ukweli na ndivyo nilivyo na ndivyo nitakavyokuwa,” Mbunge Lugola alipata kusema haya na kusisitiza kuwa ni vigumu Tanzania kupata maendeleo katika huduma za kijamii, hususan elimu, afya, maji, miundombinu ya barabara ikiwa wabadhirifu wa rasilimali za umma wataachwa bila kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Ukiacha wabunge wachache wanachama wa vyama mbalimbali vya upinzani wakiwamo David Kafulila (Kigoma Kusini – NCCR-Mageuzi), James Mbatia (Kuteuliwa – NCCR-Mageuzi), Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini – Chadema), Tundu Lissu (Singida Mashariki – Chadema), Hamad Rashid Mohamed (Wawi – CUF) na Moses Machali (Kasulu Mjini – NCCR-Mageuzi), ninatamani kuona siku moja Bunge letu linakuwa na angalau wabunge kumi wanachama wa chama tawala – CCM wenye ujasiri wa kupigania maslahi ya umma kama anavyofanya Lugola.

Nguvu ya Lugola, Edward Lowassa (Monduli), Deo Filikunjombe (Ludewa), Anne Kilango Malecela (Same Mashariki) na Christopher ole Sendeka (Simajiro) inahitaji wabunge wengine zaidi ndani ya CCM, ili kuinyoosha Serikali itambue wajibu wake wa kuwatumikia wananchi kwa uzito unaostahili chini ya misingi ya usawa, uwazi, uadilifu na uaminifu usiotiliwa shaka.


1540 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!