DAR ES SALAAM

Na Aziza Nangwa

Moto uliozuka na kuteketeza sehemu kubwa ya Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam huenda ukasababisha athari kadhaa za kiafya kwa Watanzania.

Moto huo uliozuka usiku wa Julai 9, mwaka huu, mbali na kuathiri biashara na uchumi wa mtu mmoja mmoja, unadhaniwa pia kuathiri bidhaa ambazo zilinusurika kuteketea.

“Hatari kubwa ipo kwenye chakula. Chakula kilichonusurika kinapaswa kuzuiwa kuingia mitaani kwa kuwa kimeingiwa moshi unaoweza kuwa na sumu kutoka katika dawa za mifugo,” anasema Anna Christopher, mmoja wa wafanyabiashara walioathiriwa na janga hilo.

Anna, katibu wa umoja wa wafanyabiashara wenye vibanda kuzunguka Soko la Kariakoo, maarufu kama ‘Vigoli’, anasema:

“Tumeathirika na kupoteza mali nyingi. Lakini bidhaa za kula ndizo zimeathirika zaidi na zisipodhibitiwa zikaachwa kuingia mitaani, zitaleta madhara kwa jamii.”

Eneo la juu la Soko la Kariakoo ambako ndiko moto ulikoanzia lilikuwa maalumu kwa vifaa vya kilimo, zikiwamo dawa za kuua wadudu na za mifugo.

Anna alikuwapo wakati moto ukiwaka, naye ni mmoja wa waathirika, kwani amepoteza bidhaa zenye thamani ya Sh milioni 25, fedha alizokopa Benki ya Stanbic.

“Ni muhimu kwa mamlaka husika kukagua vyakula vinavyotolewa Kariakoo kwa sasa. Vinaweza kuathiri afya za walaji. Vinaweza kuwa na sumu,” anasisitiza.

Pamoja na hayo, ni wazi Anna bado hajarejea kwenye hali ya kawaida kutokana na mshituko aliopata baada ya duka lake kuungua, akisema:

“Hadi hapa tunapozungumza watoto wangu hawajakwenda shule. Hakuna ada! Hili duka ndilo lililokuwa tegemeo katika kuendeshea maisha yetu. Lakini walau kuna ahadi kadhaa kutoka serikalini za kutusaidia.”

Anashauri wakati soko likikarabatiwa na kuboreshwa kujengwe kisima cha maji kama tahadhari baada ya kazi ya uzimaji moto kusuasua kutokana na ukosefu wa maji.

“Soko lifanywe la kisasa na rafiki kwa wafanyabiashara na wateja. Kuwe na nafasi ili magari makubwa yafike kirahisi kuleta mizigo badala ya ilivyo sasa ambapo bidhaa hushushwa Soko la Buguruni au Tandale. Hii itasaidia kupunguza gharama za usafirishaji mizigo,” anasema.

Anasema miundombinu bora ya kuingia na kutoka itawarejesha wateja walioacha kufika Kariakoo kutokana na msongamano, hasa wa wamachinga.

Katibu huyo wa Vigoli anaomba mamlaka zinazojishughulisha na bima kutoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wake ili majanga yatakapotokea wasipoteze mitaji yao.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Gwilabuzu Ludigija, amewapatia maeneo mengine ya biashara waathirika wa janga la moto Soko la Kariakoo, kupisha uchunguzi na baadaye ukarabati.

Anasema serikali imedhamiria kuhakikisha wanaendelea kutafuta riziki zao, na sasa wamepelekwa katika masoko ya Machinga Complex na mengineyo yaliyopo sehemu mbalimbali za Dar es Salaam.

“Kila mmoja kabla ya kuondoka kwanza ajiorodheshe. Tumeweka utaratibu kuhakiki majina ya wafanyabiashara waliopo ili ukarabati ukikamilika iwe rahisi kurudi katika maeneo yao ya awali,” anasema Gwilabuzu.

Masoko yatakayotumiwa kwa muda na wafanyabiashara wa Kariakoo ni Machinga Complex, Kisutu na Kiwalani.

Watu wengi wanakiri kwamba ilikuwa ni bahati kwa ajali ile kutokea usiku, kwamba kama ingetokea mchana madhara yangekuwa makubwa zaidi.

“Tunawaomba wafanyabiashara kushikamana na serikali na tumewapa maeneo hayo ya biashara bure kwa miezi miwili wajipange,” anasema.

Mwenyekiti wa Soko la Kariakoo Shimoni, Ramadhani Kakandiro, pamoja na kukubaliana na maagizo ya serikali, anapendekeza wanaotoka shimoni wapelekwe eneo au soko moja badala ya kuwatawanya.

“Soko (la Kariakoo) limeharibika lote! Tumepoteza mali na fedha nyingi na hatujui pa kushika zaidi ya kuisikiliza serikali itakavyotusaidia katika kipindi hiki kigumu,” anasema Kakandiro.

Mfanyabiashara wa dawa na vifaa vya mifugo katika soko hilo, Emmanuel Mbise, anasema amepoteza Sh milioni 390 katika janga hilo.

Mbise anamiliki maduka mawili Kariakoo; namba 19 na 26, na japokuwa yana bima ya moto, lakini janga la moto Kariakoo limemshitua na kumtikisa kifedha.

“Ada za shule na marejesho ya mikopo vinaniumiza kichwa. Ninadaiwa na benki Sh milioni 10,” anasema.

Tayari Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameshawaahidi waathirika hao kwamba taasisi za mikopo na fedha zitawaongezea muda wa kulipa madeni yao.

Ofisa Biashara wa Manispaa ya Ilala, Solomon Mushi, anasema serikali itajenga miundombinu imara na rafiki kwa wafanyabiashara na wateja wa Kariakoo.

Anasema timu maalumu ya wataalamu wakishirikiana na wafanyabiashara inashughulikia uhamishaji wa wafanyabiashara hadi ukarabati utakapokamilika.

“Wasiwe na hofu kwa kuwa masoko wanakokwenda nayo ni mazuri. Hayana shida! Ni ya kisasa.

“Pia kwenda huko kutawapa nafasi ya kutanua biashara zao kwani watakuwa wanamiliki vizimba huko wanakokwenda sasa na baadaye hapa Kariakoo,” anasema Mushi.

Anasema tayari benki kadhaa zimeonyesha nia ya kuwasaidia wafanyabiashara na kuwapa mitaji ya kuanzisha biashara katika masoko mapya.

Beda Amuli: Mbunifu wa Soko la Kariakoo

Kwa mujibu wa makala iliyoandikwa na Mzee wa Atikali, mbunifu wa Soko la Kariakoo, Beda Jonathan Amuli, alikuwa mtu mweusi wa kwanza kutoka Tanzania (wakati huo Tanganyika), kutunukiwa shahada ya kwanza ya usanifu majengo (Architecture).

Mwaka 1969, Amuli alikuwa mtu ‘mweusi’ wa kwanza mwenyeji wa Afrika Mashariki na Kati kuanza shughuli binafsi za usanifu Tanzania na baadaye Kenya mwaka 1973. Amebuni na kusanifu majengo mengi maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Kuzaliwa na elimu

Amuli alizaliwa Mei 27, 1938 katika Kijiji cha Machombe, Masasi mkoani Mtwara.

Alipata elimu ya msingi huko huko Masasi. Mmoja wa waliosoma naye shule moja ni Edward Nicholaùs Akwitende aliyekuja kuwa mwanasoka wa aina yake wa timu ya taifa. Amuli alikuwa mwanafunzi mwenye akili sana.

Alipata elimu ya sekondari St. Andrew’s College (siku hizi Minaki, Pwani) baada ya kufanya vema shule ya msingi.

Mgiriki amfanya kuwa msanifu

Wakati akiwa darasa la 11 (kidato cha tano) Minaki, kulikuwapo mkandarasi wa majengo raia wa Ugiriki, aliyekuwa akijenga Kituo cha Afya na chuo.

Kazi iliyofanywa na Mgiriki huyo ilimvutia sana Amuli na kutamani kuwa mhandisi. Amuli amewahi kunukuliwa akisema:

“Awali, wazo la kuwa msanifu majengo liliniingia kichwani, nikitamani kuwa mhandisi.”

Mwalimu wake wa hesabu anayetajwa kwa jina la Leeson, raia wa Uingereza naye pia alichangia katika kumhamasisha kusoma usanifu majengo.

Hiyo ilikuwa mwaka 1957 alipokuwa akijiandaa kufanya mitihani ya mwisho ya Cambridge, ambapo Leeson alimshauri hivyo kutokana na umahiri wake mkubwa kwenye hesabu za maumbo (Geometry).

Alipojaza fomu za nini anataka kufanya baada ya kumaliza shule, chaguo la kwanza la Amuli likawa ni usanifu.

Akafaulu vizuri sana mitihani na kuwa mwanafunzi wa kwanza na Mwafrika pekee kuchaguliwa kusomea usanifu majengo, Royal Technical College of East Africa jijini Nairobi, Kenya.

Darasa lake lilikuwa na wanafunzi wanane, watano kati yao wakitokea Tanganyika ambao ni Mohamed Sumar, Joe Calaco, Jaghder Singh, Peter Rowlands na Amuli mwenyewe. Wote walidhaminiwa na Serikali ya Tanganyika.

Akiwa mwaka wa pili hapo Royal Technical College, Chama cha TANU kikatoa nafasi ya masomo ya usanifu majengo Chuo cha Technion Institute of Technology nchini Israel.

Akiwa na umri wa miaka 21, Amuli akaipata nafasi hiyo.

Alikuwa ni Joseph Nyerere, mdogo wake Mwalimu Julius Nyerere, akiwa kiongozi wa Umoja wa Vijana wa TANU (TANU Youth League), ndiye aliyefanikisha suala hilo huku akipata upinzani kutoka kwa Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi wa serikali ya kikoloni.

Mwaka 1960 Amuli akaanza miaka mitano ya kuisaka Shahada ya Usanifu Majengo huko Israel, akiwa Mwafrika wa kwanza kusajiliwa katika chuo hicho chenye zaidi ya wanafunzi 4,000 wakati huo.

Akaweka rekodi nyingine kuwa Mwafrika wa kwanza kusoma Kiebrania, lugha aliyojifunza kwa miezi minane kabla ya kuanza masomo yenyewe Oktoba 1960.

Mei 25, 1965, akatunukiwa shahada yake!

Ashiriki ujenzi Kilimanjaro Hotel

ZEVET, kampuni ya ujenzi ya Israel aliyofanya nayo kazi akiwa mwaka wa nne chuoni, ikashinda zaburi ya kubuni Hoteli ya Kilimanjaro ya Dar es Salaam, hivyo wakampa nafasi ya kazi baada ya kumaliza mitihani. Akakubali.

Wala haikuwa ajabu kwa kampuni hiyo kumhamishia Amuli Dar es Salaam na kuwa mwakilishi mkazi wa ZEVET. 

Ni yeye aliyesimamia mradi wa ujenzi wa Kilimanjaro Hotel mwaka 1965, Jengo la Ushirika (Mtaa wa Lumumba, Mnazi Mmoja) mwaka 1966 na Makao Makuu ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC, Mtaa wa Ohio) mwaka 1967.

Ni Amuli ndiye aliyechagua maeneo maarufu ya kujenga Ngorongoro Wildlife Lodge (1966), Mikumi Wildlife Lodge (1966), Mafia Fishing Lodge (1967), maghorofa ya Sea View kwa ajili ya TRC (1966) na majengo mengi ya binafsi.

Aachana na ZEVET

Mgogoro wa washirika waandamizi ulioikumba Kampuni ya ZEVET kuelekea mwishoni mwa mwaka 1968, ulisababisha Amuli kuachana na kampuni hiyo Februari 1969 na kuanza kufanya kazi binafsi.

Mwaka 1969 akawa wa kwanza kufungua ofisi binafsi ya usanifu majengo nchini, ghorofa ya juu kabisa ya Jengo la Ushirika.

Akafungua ofisi nyingine Mtaa wa Tom Mboya kwenye Jengo la Sunglora jijini Nairobi mwaka 1973.

Kazi ya kwanza binafsi

Alipewa kazi ya kwanza akiwa nje ya ZEVET mwaka 1969; Jengo la Biashara ya Umoja wa Vijana wa TANU.

Jengo la ghorofa 10 katika kiwanja ambacho sasa pamejengwa Benjamin Mkapa Tower, Mtaa wa Azikiwe, mkabala na Posta Mpya.

Ukosefu wa fedha ukasababisha mradi huo kutotekelezwa, lakini Amuli alilipwa kwa kazi yake, na amewahi kunukuliwa akisema: “Fedha zile ndizo zilifungua njia kwa ‘B.J. Amuli Archtects’.”

Mradi wa Soko la Kariakoo

Soko la Kariakoo (ambalo lilishika moto Julai 9, mwaka huu) lipo kwenye makutano ya mitaa ya Mkunguni, Swahili, Sikukuu na Nyamwezi.

Kabla ya ujenzi wake, pale palikuwapo jengo la vyuma, kambi ya jeshi ikifahamika kama ‘Carrier Corps’, kombania ya mizigo ya jeshi la Uingereza.

Ni matamshi ya Waswahili kwa maneno hayo ya Kiingereza ndiyo yakazaa jina ‘Kariakoo’.

Kombani hiyo ilipoondoka, jengo likatumika kama soko lakini baadaye likachakaa sana.

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam mwaka 1970, ikaamua kujengo jengo la kisasa, mradi uliodondokea mikononi mwa Amuli.

Akafanyiwa usaili na mhandisi wa jiji; Amuli akamuonyesha michoro ya masoko kadhaa ya Israel. Mhandisi huyo amewahi kusema:

“Akiwa mwaka wa nne wa masomo yake Israel, ‘project’ aliyoifanya Amuli ilikuwa ni ya soko na alifanya utafiti wa kina. Ni wazo lake ndilo lilinipa mwongozo wa kuwa na soko la Kiafrika.”

Wazo alilowasilisha Amuli lililenga soko lenye utamaduni wa Kiafrika. Anasema: “Kwa kawaida soko la Kiafrika huwa chini ya miti. Kwa hiyo tukatengeneza miti kwa zege. Mteja (Jiji) hakuwa na wazo la nini anahitaji. Lakini kutokana na tafiti nilizowahi kufanya kabla, nilijua nini kinapaswa kujengwa.”

Michoro ya Amuli ilipewa baraka na Halmashauri ya Jiji kwenye Ukumbi wa Karimjee. Kampuni ya uhandisi ya Gordon Melvin & Partners ilimtengenezea mfano, aliporidhika, Amuli akaanza ubunifu na usanifu wa Soko la Kariakoo. 

Jiji likataka ujenzi ufanywe haraka na kuwapa kazi ya ujenzi Kampuni ya MECCO bila zabuni.

Kazi ya ujenzi ikaanza mwaka 1971; jiwe la msingi likiwekwa Septemba 7, 1973 na Makamu wa Kwanza wa Rais, Aboud Jumbe Mwinyi.

Jengo la Kariakoo limegharimu Sh milioni 23.3 na kufunguliwa na Mwalimu Nyerere Desemba 8, 1975, ikiwa sehemu ya sherehe za miaka 14 ya Uhuru.

Miradi yake mingine

Kwa hakika ukizungumzia eneo la ubunifu na usanifu majengo Tanzania, Amuli hana mpinzani.

Miradi yake mingine ni Chuo Kikuu cha Ruaha, Iringa; Chuo cha IFM, Dar es Salaam; Mzumbe, Morogoro, majengo kadhaa ya UDSM, Makao Makuu ya CCM; Moshi, karibu majengo yote ya NBC nchini pamoja na makao makuu ya Ushirika katika mikoa mbalimbali.

Pia kuna misikiti, makanisa, magodauni ya NMC, viwanda, majengo ya NHC, CRDB, shule, hoteli, posta na NSSF.

Nyumba ya Rais wa Nne, Jakaya Kikwete huko Bagamoyo, pia ni kazi ya Amuli.

Mwaka 2007, Amuli akaiunganisha kampuni yake na msanifu mwingine, N. Alute na kuitwa BJ AMULI Architects Partnership. Baada ya hapo, Amuli akaamua kufanya kazi kimyakimya!

Afariki dunia

Beda Jonathan Amuli alifariki dunia Julai 10, 2016 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, akiacha watoto wanane na wajukuu kadhaa, ambapo hakuna hata mmoja aliyerithi kazi ya usanifu na ubunifu majengo.

By Jamhuri