DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu  

Hebu fikiria unarudi nyumbani au maskani kutoka kazini, umechoka kwa pilikapili za kutwa nzima, kama kawaida unajikuta unashika simu yako ya kiganjani na kuingia katika mitandao ya kijamii. 

Mitandao ya kijamii ni liwazo kwa watu wengi siku hizi, kwa kuwa ni huko ndiko unakokutana na kila aina ya mambo. Yapo ya kufurahisha, mengine ya kusikitisha na hata mengine unaamua kuyadharau tu kwa kuwa ni ya kipuuzi.

Mwisho kabisa unakutana na mmoja wa wazee watata sana kwa sasa nchini, huyu anafahamika kwa jina la mzee Mpili. Ni mtata na matata kweli kweli!

Unakutana naye mitandaoni na mikogo yake. 

Kwa kusema ukweli mzee Mpili ana mikwara. Ana mbwembwe. Kubwa zaidi mzee huyu ana kinywa chenye mamlaka. Kwa kifupi ameshatujua mashabiki wa soka wa Tanzania tunataka kusikiliza kitu gani kutoka kwake. Anatumudu sana siku hizi.

Waandishi wa habari bila kutambua tumejikuta tumeshageuka mateka wake. Wafungwa au wafuasi wa mzee Mpili. Aliko mzee Mpili hatua tano au saba utakuta amesimama mwandishi wa habari au kikundi cha watu kinachomshangaa. 

Ametuweka katika kiganja chake. Hatukukuruki hata kidogo.

Katika miezi ya hivi karibuni, mzee huyo amejenga hofu kubwa katika mioyo ya manazi wa Simba. 

Akizungumza manazi hao wanamsikiliza huku wanang’ata kucha zao kwa hofu. Tena hofu kubwa. 

Hii ni dunia ya ajabu kidogo. Kinywa cha mzee Mpili kinakuwaje tishio kuliko mbinu za kocha Nabi? Hii ni dunia ya ajabu. Kwa hakika dunia yetu Watanzania ni ya peke yetu kabisa.

Haji Manara ni mwamba. Tena mwamba kweli! Kwa miaka mingi sasa amefanikiwa kuwazima wasemaji wengi wa Yanga. Lakini kwa mzee Mpili, maisha yamekuwa tofauti sana kwa Haji. 

Kwa mzee Mpili Manara ameficha mkia wake kama mbwa koko anayeogopa hatari. Hana la kufanya, naye amegeuka kuwa shabiki mkubwa wa mzee Mpili.

Hizi sasa ni zama za mzee Mpili. Yaani ni mzee Mpili katika ubora wake. Haishangazi kuona kwa sasa ni yeye ndiye anayeuza zaidi kuliko hata yule mchezaji aliyefunga bao linalompa kiburi na jeuri aliyo nayo.

Ni shabiki gani aliyemzungumzia na kumpa sifa anazostahili Gift Mauya kwa kufunga bao pekee katika mechi dhidi ya watani wao wa jadi, Simba? 

Zunguka kote, Dar es Salaam na hata nje ya Dar es Salaam, unaweza usikutane na mtu anayemwaga sifa kwa mfungaji. 

Hii ni tofauti na zamani ambapo akina Salum Swed ‘Scud’ walizungumzwa na kusifiwa mwaka mzima kwa kufunga bao moja tu, lakini muhimu, dhidi ya Simba.

Sasa hakuna mtu anamtaja Mauya. Kila mtu anataka kumuona mzee Mpili na kuisikia mikwara yake kuelekea mechi ya Kigoma ya fainali ya Shirikisho dhidi ya Simba. Ni kama mechi ya marudiano.

Watanzania tunaishi dunia yetu katika soka. Hatuishi katika dunia ya wenzetu ambayo timu ikishinda sifa zinakwenda kwa timu yenyewe, sifa zinakwenda kwa kocha na benchi lake la ufundi. Hii ndiyo dunia ya wenzetu. Dunia yetu mzee Mpili anakoga sifa asizostahili. 

Dunia ambayo timu zinaajili makocha wa kimataifa na wachezaji wa kimataifa na kuwalipa mamilioni ya shilingi, dunia hii, mzee Mpili anaipaje ushindi Yanga na kuinyima ushindi Simba? 

Maisha ya mzee Mpili yanatuongezea siku za kuishi duniani na kutuondolea msongo wa mawazo. 

651 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!