Katika toleo la leo tumechapisha habari za kusikitisha juu ya matumizi mabaya ya madaraka katika Idara ya Mahakama Tanzania. Tumechapisha habari kuwa mtuhumiwa mwenye asili ya China alikamatwa Alhamisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akiwa na madini ya tanzanite yenye thamani karibu Sh milioni 200.

Raia huyu wa China alikamatwa na Afisa wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA). Baada ya kukamatwa akajaribu kumhonga, Afisa huyu akakataa. Alijaribu kumhonga hadi Sh milioni 20, Afisa huyu akakataa. Madini haya inaonekana Mchina huyu aliyanunua kutoka katika kituo cha Cultural Heritage cha Arusha. Kituo hiki kinadaiwa ndicho kinapigana kufa na kupona madini yarudishwe.

 

Kifungu cha 18 (4) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kinatamka bayana kuwa mtu yeyote atakayekiuka sheria kuhusiana na umiliki wa biashara ya madini akipatikana na hatia atatotzwa faini ya kiasi kisichozidi milioni 10 au kifungo kisichozidi miaka mitatu au adhabu zote mbili.

Kifungu cha 6 (4) kinampa Kamishina wa Madini uwezo wa kutaifisha madini yaliyopatikana kinyume cha sheria pamoja na vifaa vilivyotumika kuzalisha madini hayo. Kupatikana kinyume cha sheria ni pamoja na hivi alivyokutwa huyu Mchina akiwa na madini ambayo hayakulipiwa kodi na wala hakuwa na stakabadhi yoyote ya Serikali.

Kilichotokea ni kwamba Mchina huyu alikuwa ametoa malipo ya awali kwa Cultural Heritage ambapo walikubaliana kuwa akiishauza angewalipa kiasi kilichosalia. Cultural Heritage walionyesha kuwa thamani ya madini haya ilikuwa Sh milioni 89, wakati kwa uhalisia TMAA walipokagua wakakuta thamani halisi ya madini haya ni karibu Sh milioni 200.

Kitendo cha kupeleka madini nje ya nchi bila kuyalipia kodi, na kitendo cha kujaribu kumhonga Afisa wa TMAA kiasi cha Sh milioni 20 ni ushahidi tosha kuwa Mchina huyu na waliomuuzia madini wanajua kinachoendelea na huenda si mara yao ya kwanza kufanya hivyo. Kilichofuata baada ya msuguano huu ndicho kichekesho.

Hakimu D. J. Mpelembwa wa Mahakama ya Wilaya ya Hai, Bomang’ombe alipelekewa kesi hiyo siku ya Ijumaa (Oktoba 18) na Mchina huyu akakiri kosa. Baada ya kukiri kosa, Hakimu Mpelembwa akamhukumu kwa mujibu wa sheria kuwa Mchina huyu apelekwe jela mwaka mmoja au alipe faini Sh 300,000. Mchina hakufanya hiyana. Alilipa faini akaachiwa huru.

Mpaka hapo, hakimu hakuwa ametenda kosa lolote. Kosa lilianzia katika maelekezo yake kwamba Mchina huyu arejeshewe madini aliyokutwa nayo, hata baada ya yeye kukiri kuwa amekutwa nayo kinyume cha sheria. Sheria inasema ukikutwa na madini ambayo hayajalipiwa kodi unayasafirisha nje ya nchi yanataifishwa. Tunachojiuliza, Hakimu Mpelembwa alipata wapi mamlaka ya kuamru Mchina arudishiwe madini haya?

Wala sisi hatutilii shaka kasi iliyotumika kusikiliza kesi husika, pengine kwa kuwa Mchina hakutaka kuisumbua Mahakama kwa kukiri mwenyewe, lakini tunasema kutoa maelekezo nje ya mamlaka ya kisheria (ultra vires) kuwa Mchina arejeshewe madini yake ndio shaka yetu. Hiyo ndio nguzo ya maoni haya kutaka Hakimu huyu ashughulikiwe.

Uamuzi kama huu unapotolewa, inachafuka Idara yote ya Mahakama. Watu wenye kujua kilichokuwa kinaendelea wanaona huenda shinikizo alilolikataa Afisa wa TMAA pengine limekubaliwa na Hakimu huyu ndio maana akahemuka na kutoa maelekezo nje ya sheria. Mahakama ikimnyamazia hakimu huyu, wote walioshuhudia sakata hili tangu awali watajua kuna shinikizo limemsukuma kufikia uamuzi huu.

Ni kwa mantiki hiyo, tunasema kila iwavyo lazima Hakimu huyu achukuliwe hatua kwa haraka kuepusha tabia ya baadhi ya watu kujisahau na kutoa uamuzi nje ya mipaka ya mamlaka yao. Wanapofanya uamuzi kama huu, matokeo yake Idara nzima ya Mahakama inatuhumiwa kwa vitendo vya rushwa na hatimaye heshima yake inashuka. Sisi tunasema kwa hili hapana. Tudhibiti matendo haya.

 

 

1031 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!