Nishati na Madini ni Mfano  wa kuigwa

 

Mwishoni mwa wiki iliyopita Wizara ya Nishati na Madini iilitoa taarifa ya utekelezaji wa kipindi cha miezi mitatu iliyopita chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa sasa (BNR).

Wizara hiyo imekuwa ya kwanza kati ya wizara zote kujitokeza hadharani na kutoa ufafaunuzi kuhusu hatua ilizochukua katika kutekeleza BRN.


Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakimu Maswi katika taarifa hiyo amesema kuwa Serikali inaamini kuwa huduma ya umeme ni kitu muhimu na cha lazima kwa kila  Mtanzania.


Amesema  kwa kutambua hilo Serikali kupitia wizara yake itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kila Mtanzania anapata umeme.


Katika taarifa yake Maswi amesema wizara inaendelea kutekeleza miradi 29 ya ufuaji umeme usafirishaji usamabazaji na ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam


Amesema kuwa kitengo cha ufuaji umeme kimebeba miradi saba, kitengo cha usafirishaji nacho kina miradi saba wakati kitengo cha usambazaji kimebeba miradi 14.


Maswi amesema Serikali kupitia wizara yake tayari imeishasaini na wahisani na wakandarasi mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza miradi huska.


Kuhusu usambazaji umeme vijijini Maswi amesema kuwa Wakala wa Umeme Vijijini (REA)  imeishapokea fedha kutoka serikalini kwa ajili ya utekelezaji wa miradi.


Maswi alisoma taarifa hiyo na kuulizwa maswali kutoka kwa wananchi mbalimbali waliokuwa na shauku ya kujua kuhusu taarifa hiyo naye alijibu kiufasaha hali iliyomridhisha kila mtu aliyepata nafasi ya kuuliza swali.


Sisi JAMHURI tunaipongeza wizara hiyo kwa kuonesha ukomavu, uzalendo na utii kwa wananchi ambao kimsingi ndio walengwa katika utekelezaji wa BRN.


Ni matumaini yatu kuwa kila wizara itaiga mfano huu na kuwaeleza wananchi ni nini kimefanyika katika mpango huo.


Kufanya hivyo kutatoa majibu sahihi ya utendaji wa kila wizara katika mpango huu, kuliko kuishia kusikia waziri akijibu bungeni katika maswali na majibu.


Utaratibu huo wa Maswi kama ukifuatwa na wizara nyingine utaongeza uwajibikaji miongoni mwa watendaji katika wizara hizo hasa pale wananchi  watakaposhindwa kuelewa ufafanuzi uliotolewa na wizara husika.