Mwanamichezo na mwanamasumbwi mashuhuri Mohammed Ali ameugua kwa muda mrefu na kufariki hivi karibuni na tayari wanatafutwa wachawi wake.

 Si uchawi ule tuliozowea kuusikia Waafrika lakini ni uchawi unaokuzwa na kushamiri kwa sababu binadamu wote asili yao moja na hata wajipambanue kiasi gani kuna tabia zitakazowaunganisha wakati wote. Na hakuna jambo linalowatambulisha wanadamu kwa asili yao kama kufanana kwao kitabia katika kukabiliana na misukosuko ya maisha.

Kwa mtazamo wa baadhi ya wachambuzi ni kwamba bara la Afrika ndiyo huongoza kwa kushika mkia kimaendeleo kwa sababu ya kung’ang’ania mawazo, fikra na desturi zinazorudisha nyuma maendeleo. Mojawapo ya vikwazo hivi vya kuleta fikra chanya ni imani za uchawi.

 Lakini pamoja na kusemwa hivyo, uchawi unapewa nafasi muhimu sana na ya lazima na wataalamu. Uchawi unaelezewa na wana sosholojia, wana taaluma wa sayansi inayohusu asili na maendeleo ya jamii pamoja na tabia zake, kuwa ni hali inayojitokeza kuwapa wanajamii majawabu juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili maishani, mathalani, katika masuala ya afya au mahusiano. Tunaamini kuwa waganga na wapiga ramli wanajibu maswali na kutupatia ufumbuzi juu ya matatizo yetu. Hii ilikuwa sehemu ya elimu yetu asilia iliyotokana na tamaduni zetu.

 Lakini elimu hiyo ilibadilika na mitaala ikabadilika baada ya kutembelewa na wageni na kuanza kwa ukoloni. Na kadiri tulivyoendelea kupata elimu kwa muongozo wa mitaala hii mipya sehemu ya jamii ikaandika ukurasa mpya kuelezea sababu ya baadhi ya changamoto zinazotukabili. Imani za uchawi zikapisha maelezo ya kisayansi. Sayansi inatufundisha kuwa radi inaposhuka toka kwenye mawingu kuja ardhini, kwa kawaida hutua kwenye sehemu au kitu kilicho kirefu kuliko vyote katika eneo inaponyesha mvua iliyoambatana na radi. Kwa sababu hiyo, anayetaka kuepuka kupigwa na radi hapaswi kujikinga na mvua kwa kusimama chini ya mti.

 Tunasikia simulizi kuwa wapo wachawi waandamizi ambao huweza kuelekeza radi ikamtoa mtu uhai. Pamoja na uwepo wa mitaala mipya, mizizi ya tamaduni zetu bado ipo imara.

 Ni mizizi inayothibitisha tu ukweli kuwa mwanadamu siku zote huwa na kiu kikubwa cha kufahamu chimbuko la matukio na changamoto zinazomkabili. Na hutaka majibu haraka. Yakichelewa kumfikia yuko tayari hata kuyatunga. Hii ni kweli kwa Mwafrika, na kwa wanadamu wengine pia.

 Mohammed Ali hakupata umashuhuri kwenye masumbwi pekee, bali alikuwa ni mwanaharakati aliyetetea haki za watu weusi. Alikataa kujiunga na jeshi la Marekani ili akapigane kwenye vita ya Vietnam na alishtakiwa na kutumikia kifungo gerezani kwa sababu hiyo. Alibadilisha dini kutoka Ukristu na kujiunga na dini ya Kiislamu katika nchi ambayo sehemu kubwa ya wakazi wake ni waumini wa madhehebu za Kikristu ambazo enzi hizo za miaka ya sitini zilikuwa na misimamo mikali ya kihafidhina dhidi ya imani nyingine kuliko ilivyo sasa. Kwa kifupi alikuwa na maadui wengi.

 Na mmoja wa maadui hawa, mmoja wa wachawi hawa ndani ya muktadha wa mada yangu, ni Serikali ya Marekani. Hoja ni kuwa misimamo yake mbalimbali dhidi ya sera za Serikali ya Marekani inashukiwa kuwa sababu ya yeye kudungwa sindano iliyompa maradhi yaliyosababisha mauti yake.

 Nasema kuwa haiwezekani kuwa huo ndiyo ukweli? Hapana. Nasema kuwa inanikumbusha tu kwa jinsi gani binadamu wote asili yao moja. Kwenye jamii zetu za Kiafrika tukikaa kwenye misiba mada kuu huwa: mchawi aliyemuua mpendwa wetu ni nani? Na Marekani ni hivyo hivyo. Kimuonekano, labda mchawi wetu kavaa tunguli na  hirizi na yule wa Marekani kavaa suti. Labda yule wa Marekani anatumia sayansi ya mitaala mipya, na pengine huyu wetu anatumia sayansi hiyo hiyo ambayo tunaiita uchawi.

 Kwa wenzetu, siyo yule mchawi asilia tunayemfahamu ila ni huyo huyo tunaemjadili mara kwa mara kwenye misiba.

1325 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!