Serikali imeamua kwa makusudi kuwapanga wafanyabiashara wadogo na jana ilitarajiwa kuwa siku ya mwisho kwa wafanyabiashara hao maarufu kama wamachinga wa Dar es Salaam kuondoa vibanda vyao katika maeneo yasiyo rasmi.

Hii ni hatua muhimu katika utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuleta mwonekano mpya, mzuri na wa kuvutia kwa miji na majiji ya Tanzania.

Kwa miaka mingi biashara ndogondogo za uchuuzi zimekuwa zikifanyika kiholela kando ya barabara kubwa katika miji mingi ya Tanzania na kusababisha misongamano ya watu na magari isiyokuwa na lazima.

Vibanda vya wafanyabiashara hawa vimegeuka kuwa uchafu, vikificha uzuri wa mitaa na barabara zilizojengwa kisasa na hata kuziba njia za watembea kwa miguu.

Wadau wa biashara na walipa kodi wakubwa wamekuwa wakilalamikia utaratibu huu ambao mbali na kuwa bughudha kwa watumiaji wengine wa barabara, umesababisha kupunguza wigo wa makusanyo ya kodi; ukitumika pia kama njia mojawapo ya kukwepa kodi.

Juhudi za mara kwa mara za mamlaka za miji na majiji kuwaondoa wamachinga katika maeneo yasiyo rasmi zimekuwa zikikwamishwa na kauli za wanasiasa ambao huwatumia vijana hawa kama mtaji wa kura kwenye chaguzi mbalimbali.

Kauli ya hivi karibuni iliyosababisha kiburi na jeuri kwa wamachinga ni ile iliyotolewa na aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli, akitaka waachwe wafanye biashara sehemu yoyote wanayoitaka; kauli iliyosababisha wamachinga kuanza kupanga bidhaa hata kwenye barabara ya mwendokasi maeneo ya Kariakoo.

Tunaamini kwamba hatua iliyofikiwa sasa ya kuwapangia wamachinga maeneo mengine ya biashara itakuwa ni ya kudumu, ambapo mamlaka za miji na majiji zitapewa nguvu kisheria kuzuia biashara holela mitaani.

Tunafahamu kwamba wafanyabiashara hawa ni Watanzania wenzetu wanaojipatia riziki kwa kazi hiyo, lakini ukweli unabaki palepale kwamba ni lazima na ni muhimu kuwapo kwa utaratibu mzuri wa kufanya biashara kistaarabu katika miji yetu.

Hatuwezi kuwa na miji ambayo pembeni ya mitaa yake akina mama wanapika na kuuza ugali maeneo ya wazi; wateja wao wakijipanga na kula kinyume cha ustaarabu wa Kitanzania.

Hata hivyo, tunaamini kuwa mamlaka husika zitatekeleza maagizo haya kwa utaratibu stahiki bila kutumia mabavu na kusababisha vurugu mitaani, na ndiyo maana tunaipongeza serikali kwa kufanya uamuzi huu muhimu kwa maendeleo ya taifa.

309 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!