*Kauli ya Simbachawene yadaiwa kudhalilisha makonstebo

DAR ES SALAAM

Na Dennis Luambano

Sifa za vijana wanaoomba ajira katika majeshi kuwa na ufaulu wa daraja la nne zimezidi kuibua mgongano wa kauli baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, kusema wanawaajiri hao kwa kuwa wanataka askari watakaobeba bunduki za kulindia benki, watakaocheza gwaride, watakaokamata wahalifu mitaani na watakaofanya doria nyakati za usiku.

Mgongano huo umewaibua watu mbalimbali baada ya Simbachawene kunukuliwa Oktoba 11, mwaka huu akitoa ufafanuzi kuhusu ajira za majeshi hayo likiwamo Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Magereza na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kupitia Kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na ITV.

Kutokana na ufafanuzi huo, Oktoba 12, mwaka huu kupitia mtandao wa Twitter, Mchambuzi wa siasa na mwanahabari mkongwe hapa nchini, Absalom Kibanda, anasema kauli ya Simbachawene kuhusu madaraja ya ufaulu na kazi ya upolisi ni potofu na hatari kitaaluma kwa Jeshi la Polisi.

“Ufaulu pekee si kigezo cha uwezo/ujinga. Ingetosha kusema waliopata madaraja ya juu walikuwa na fursa vyuoni. Ana bahati Rais Samia ni mpole na mstahamilivu,” anasema Kibanda.

Naye Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, akikazia hoja ya Kibanda kupitia mtandao huo anasema alipokuwa mbunge amekutana na askari mwenye elimu ya shahada akilinda Benki ya CRDB.

“Mwaka 2001 tukiwa viongozi wa Daruso (Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) tuliwawezesha vijana 606 kupata udhamini wa serikali. Hapo kabla walikuwa wamenyimwa. Siku moja nikiwa tayari ni mbunge nilikutana na mmoja wa viongozi wa vijana wale akiwa CRDB analinda. Alikuwa na shahada na alishika bunduki kulinda benki,” anasema Zitto.

Wengine kupitia mtandao huo akiwamo Imma Mbuguni, anasema nchini China, polisi ndio wanalipwa mishahara mikubwa kuliko kada yoyote na kusababisha ushindani wa kupata kazi kuwa mkubwa kwa kigezo cha elimu.

“Kwa mfumo huo, China imefanikiwa mno katika kukabili uhalifu, kwa sababu uwezo wa polisi ni mkubwa hata kifikra. Kwetu polisi ni force na si service,” anasema Mbuguni.

George Damas anasema suala si kuchukua waliofeli au wenye daraja la nne bali kinachotakiwa ni kuboresha masilahi yao na yakiwa mazuri hata mwenye shahada ya chuo kikuu atashika bunduki kulinda benki kwa kuwa watalipwa mishahara mizuri.

Mnaku Mbani, yeye anasema Simbachawene amewasimanga askari washika bunduki, wapiga kwata na wanaofukuzana na wahalifu mitaani huku Jarateng akisema polisi ndio kada ya hali ya chini na hata uamuzi wanaochukua katika utekelezaji wa mambo mbalimbali unaakisi uelewa na elimu zao.

Katika hatua nyingine, Midraj Maez, anasema sifa za kujiunga na Chuo cha Reli Tabora ni kwa wale wasiokuwa na sifa za kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kwa sababu wakishahitimu kama ‘railway man’ wanatakiwa kuendelea hivyo na kinyume chake kada za reli hazitajitosheleza.

“Maana mass exodus kujiunga vyuo vya elimu ya juu itatokea. Kibinadamu mindset zetu tunafikiri ukiwa na taaluma ya chuo ndiyo utatoboa,” anasema Maez.

Januari 24, mwaka jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Vyuo vya Jeshi la Polisi na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Profesa Elifas Bisanda, amenukuliwa akisema jeshini ni mahala kunapotakiwa kwenda watu waliobobea katika taaluma mbalimbali.

Bisanda anasema si sahihi kufikiri kwamba watoto wasiofanya vizuri wanatakiwa kwenda polisi na waliofaulu vizuri waende kada za udaktari au uandisi.

“Nchi zetu za Afrika bado hazijatambua hilo, ukiangalia katika nchi zilizoendelea kama Marekani wale wanaofanya vizuri kabisa wa daraja la kwanza wanakwenda jeshini, tuamke,” anasema na kuongeza:

“Jeshini ndiko kunakotakiwa kuwa chimbuko la utafiti, kuwe na vitu vizuri vinakoanza, nitoe mfano tu, simu za mkononi zimeingia uraiani baada ya kutumika katika majeshi kwa zaidi ya miaka 10.

“Internet tunayoijua sisi ilianza kutumika miaka 1970 katika majeshi ya wenzetu na uraiani ilianza miaka ya 1989 hadi 1990 baada ya wao kugundua teknolojia nyingine ndipo wakatupatia sisi raia.”

Wiki iliyopita, Gazeti la JAMHURI limemtafuta Bisanda atoe ufafanuzi zaidi baada ya Simbachawene kutoa kauli hiyo lakini kupitia kwa Meneja wake, Dk. Albert Memba, anasema aliyoyazungumza wakati ule yalikuwa ya hadharani na hataki kuyarudia upya.

Awali, Simbachawene, anasema ajira hizo 2,300 zimetangazwa mahususi kujaza nafasi za askari watakaokwenda katika malindo muda wote na si maofisa.

“Ni kweli, suala la ajira 1,000 za Polisi, 350 za Uhamiaji, 250 za Zimamoto na 700 za Magereza zimekuwa gumzo baada ya kuzipata, hata mimi hilo jambo nimeliona katika mitandao ya kijamii na limechukua nafasi kubwa katika mijadala hata wasomi wakiwa wanatoa maoni yao,” anasema.

Simbachawene anasema kwa sasa shida ya majeshi yaliyopo chini ya wizara yake ni kwamba ina maofisa wengi wanaosimamia operesheni kuliko askari wa kawaida wanaoshiriki kufanya operesheni.

“Vyombo vyetu vina maofisa wengi kuliko askari wa kwenda field. Maofisa ni wengi kule juu lakini chini hakuna kitu, ni kama jeshi linakuwa na kichwa lakini miguu halina,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, anasema ndiyo maana ajira hizo zimetangazwa kwa vijana wenye sifa hizo ili waje kushika nafasi za konstebo.

Kupitia nafasi na sifa hizo, anasema vijana watakaoajiriwa na majeshi hayo hawataweza kupanda vyeo zaidi ya kuishia sajenti meja.

“Vijana hao wote wanaingia katika ajira na baada ya mafunzo wanakuwa konstebo kwa maana hawana cheo chochote ila wakifika pale kuna kuachana na baada ya miaka mitano tumeshawatumia vya kutosha na hata wakipanda vipi hawawezi kuzidi cheo cha sajenti meja,” anasema na kuongeza:

“Cheo hicho ni cha askari wa field na wenzao wengine katika miachano hiyo hiyo wanaweza kupanda kutoka konstebo japo kwa juhudi kubwa mno na wengine wanaweza kupanda hadi kuwa IGP au ICJ.

“Kwa hiyo tunapotangaza matangazo hayo kwa mfano kidato cha nne awe na daraja la nne na pointi 27 huyo ana njia ya kuendelea mbele ila mwenye pointi 28 hakuna chuo kinaweza kumchukua.

“Sisi tunawataka hao waende kuwa askari, wabebe bunduki, waende lindo na kukamata watu, sasa ukimchukua mtu wa division one ukampeleka hawezi kubeba silaha na kulinda benki, hawezi kubeba silaha akawalinda wafungwa, ndiyo maana tunawataka hawa na wataishia cheo cha sajenti meja ndiyo mwisho wao.

“Kwa mfano, zile ajira za Zimamoto 180 tunataka askari watakaoshika na kuzima moto na huwezi kumchukua mwenye digrii ukatarajia atazima moto, lakini kati ya hizo, 50 zimetangazwa kwa watu wa kidato cha sita na digrii na wenye ujuzi zaidi ya ule wa kidato cha nne ambao nao tunaamini wamefaulu.”

Katika hatua nyingine, anakanusha si kweli kwamba majeshi hayo yanataka watu wasiosoma, bali wanatakiwa kwa sifa hizo kwa shughuli maalumu na wale wenye ufaulu wa daraja la kwanza au diploma wakichukuliwa wana njia za kuendelea na vyuo vikuu.

Anasema tofauti yao ni kwamba maofisa hawawezi kubeba silaha na kwenda lindo kwa kuwa wana ufaulu mzuri wa daraja la kwanza, pili na la tatu, kwa hiyo badala ya kufanya kazi watakuwa wanang’ang’ania kwenda kusoma chuo kikuu wakati wao wanawataka wakalinde benki na kufanya doria usiku.

“Wenye diploma au daraja la kwanza hawezi kwenda katika lindo usiku, tuna upungufu wa askari, nenda hata Marekani au Uingereza nao wanatumia utaratibu na mfumo kama tunaoutumia sisi kwa miaka yote,” anasema na kuongeza:

“Ukiwa na maofisa peke yake watakuwa wanaamka asubuhi na kwenda kazini, lakini hawawezi kufanya kazi za usiku wakati sisi tumelala na askari hadi wapande vyeo ni vigumu kwa kufuata mfumo wa ndani.

“Sisi tunawataka waliofeli na waliofaulu pia, ila lazima wawe na sifa za kupita mafunzo ya JKT na kadhalika, mchakato wa ajira uko wazi kwa kushirikisha vyombo vyenyewe na hakuna upendeleo wowote kwa sababu walioomba ni wengi wakati nafasi zilizotangazwa ni chache, kwa hiyo kuna wenye sifa watakosa hizo nafasi na haina maana kuna upendeleo.”

By Jamhuri