Sengerema wamjaribu Rais Samia

SENGEREMA

Na Antony Sollo

Fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, zimeliwa.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa wizi wa fedha hizo umefanywa kwa ustadi mkubwa na maofisa kadhaa wa juu wa halmashauri ambao hadi wiki iliyopita walikuwa hawajaguswa wala kuhojiwa. 

Maofisa hao ni aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi, Ofisa Ugavi, Mhandisi wa Halmashauri, Mhandisi wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), Mkaguzi wa Ndani na Mhandisi Mshauri.

Fedha hizo zilitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kujenga jengo husika katika Kata ya Tabaruka.

Akizungumza na JAMHURI, mkazi mmoja wa Sengerema ambaye pia ni mbobezi katika masuala ya uchunguzi (jina tunalihifadhi), anasema inasikitisha kwamba wahusika katika ubadhirifu huo hawajafanywa lolote.

 “Huu ni mchoro uliochorwa kwa ustadi mkubwa sana. Inakuwaje watu hawa hawajakamatwa wakati wao ndio mshipa wa fahamu katika sakata hili?” anahoji.

Akichambua majukumu ya mtaalamu mmoja mmoja, mwananchi huyu anasema wajibu wa Mhandisi Mshauri ni kuishauri serikali ili taratibu zote zinazotakiwa katika ujenzi zifuatwe; Mkaguzi wa Ndani anapaswa kuthibitisha na kuona kama BOQ na masuala mengine yote yanakwenda sawa.

“Lakini mpaka fedha zinatolewa hawa walikuwa wapi?” anaendelea kuhoji.

Anasema jukumu jingine la Mkaguzi wa Ndani ni kuhakikisha mradi unakwenda vizuri lakini katika sakata la upotevu wa mamilioni ya fedha hizo, maofisa hawa hawakutimiza wajibu wao ingawa hadi sasa wapo ‘uraiani’.                                                                                      

Mbobezi huyo analitaja kundi jingine muhimu katika udhibiti wa fedha za umma kuwa ni Kamati ya Ujenzi yenye wajibu wa kufuatilia kanuni za matumizi ya fedha za miradi na kuzisimamia ili kuhakikisha mambo yote yanakwenda sawa.

 “Kamati hiyo inayojumuisha madiwani nayo ni kama imeamua kulifumbia macho suala hili ilhali lipo wazi na linafahamika bayana. 

“Watu tunajiuliza, kamati hii ilikuwa wapi mpaka upotevu mkubwa wa fedha za serikali unatokea? Hapa panahitajika tafakuri ya kina kuelewa juu ya namna mchoro huu ulivyoratibiwa na kuhalalisha upigaji wa fedha za serikali,” anasema mtoa taarifa huyo ambaye pia ni ofisa wa serikali. 

Anaendelea kusema kuwa iwapo wananchi wa Sengerema wamewachagua viongozi kwenda kusimamia mali za umma lakini fedha zinaibiwa mbele ya wasimamizi hao hao akiwamo Mwenyekiti wa Halmashauri na Kamati ya Fedha, basi ni wazi kuwa viongozi hao wameshindwa kutimiza wajibu wao na wanapaswa kujiuzulu mara moja.

Hata hivyo, Mtanzania huyo anatoa wito kwa vyombo vya uchunguzi kutumia jicho la tatu kuona namna gani wataalamu muhimu walioachwa katika sakata hili wakihojiwa, kwani kutochukua hatua za kisheria kutakwamisha juhudi za Rais Samia za kuwaletea maendeleo wananchi.

Mafundi, vibarua walilia mishahara, posho zao

JAMHURI limezungumza na mafundi wa ujenzi pamoja na vibarua waliokuwa wakifanya kazi katika mradi huo uliosimama, ambapo kwa ujumla wanasema mpaka sasa wanaidai Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Sh milioni 15.

Diwani wa Tabaruka, Sospeter Busumabu, anasema kitendo kilichofanywa na watumishi wa halmashauri ni ishara mbaya kwa Rais Samia aliyeipa heshima Halmashauri ya Sengerema kwa kutoa Sh milioni 749  kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya kisasa.

“Fedha zilizotolewa kwa ajili ya mradi huu zilitakiwa kukamilisha hatua ya ‘jamvi’, lakini zimeshatumika zote na mradi bado haujakamilika mpaka sasa. 

“Wananchi wa Tabaruka waliokuwa wakifanya kazi kama vibarua na mafundi wanaidai halmashauri Sh milioni 15 na sasa wanalalamika sana. Wanampigia simu mbunge; wananipigia simu mimi diwani wao; mkuu wa wilaya na hata mkurugenzi, lakini hakuna mafanikio yoyote,” anasema Busumabu.

Anasema wananchi hao wametumia mbinu mbalimbali kudai haki yao, ikiwamo kuandamana hadi kwa mkuu wa wilaya, lakini hawajafanikiwa na sasa wanaiomba serikali kuwasaidia.

“Mimi kama diwani niiombe serikali ituangalie sisi wananchi maana vibarua hawa ambao ni wapiga kura wetu wanateseka bure.

“Wamefanya kazi kwenye jengo hili mpaka hatua hii iliyofikia. Wametumia nguvu zao nyingi, na wengine wametoka maeneo ya mbali kabisa, wapo hapa. Walipanga vyumba na wanadaiwa kodi, kila kukicha wanalia hawaoni msaada. Badala ya sherehe sasa kazi hii kwao imegeuka kuwa karaha kubwa. Tunaomba mamlaka zitusaidie,” anasema Busumabu. 

Diwani huyo anahoji ni kwa nini mpaka sasa wahusika hawajarejesha fedha hizo licha ya agizo lililowahi kutolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa, aliyeita Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwahoji wahusika hao.

Wahusika wazungumza

Mwandishi wa habari hii imewatafuta wahusika wanaotuhumiwa kushiriki kwa namna moja au nyingine katika sakata hilo na kwa nyakati tofauti wamedai kutohusika.

Mmoja, huku akiomba kutoandikwa jina lake gazetini, amesema: “Ni tuhuma zinazonisumbua sana lakini kwa hakika mimi sihusiki hata kidogo.”

Kwa upande mwingine, pamoja na lawama za wananchi kwamba hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi yao, JAMHURI linafahamu kwamba maofisa hao wamekuwa wakiripoti TAKUKURU kila wiki.

Juhudi zinaendelea kufahamu uchunguzi wa TAKUKURU umefikia katika hatua gani na lini watafikishwa mahakamani. 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Binuru Shekidele, anakiri kwamba kesi hiyo ipo TAKUKURU ambako uchunguzi unaendelea. 

Alipoombwa kuzungumzia kwa undani kuhusu sakata hilo, Shekidele anasema: “Kwa kuwa suala hili liko katika hatua za uchunguzi ni vizuri kusubiri vyombo hivyo vifanye kazi yake na vikimaliza taarifa zitawekwa wazi.

“Kutoa taarifa kwa haraka si sahihi kwani unaweza kukuta mtuhumiwa huyu au yule hahusiki na matokeo yake unaweza kujikuta matatani kwa kumdhalilisha mtu. Nikuahidi tu ndugu yangu kuwa baada ya uchunguzi, tutaweka wazi taarifa hizo.”

Kuhusu kundi la wataalamu linalodaiwa kutoguswa na uchunguzi licha ya kuwapo kwa dalili zote za kuhusika, Shekidele anasema kwa kuwa suala hili liko kwenye mamlaka za uchunguzi, ikionekana kuna haja ya kuwaita wataitwa. 

“Mara ya kwanza hao unaowasema, mhandisi alikuwamo akaambiwa naye ana husika. Wote hao waliingizwa ila ninasisitiza kwa kuwa suala hili liko kwenye vyombo vya kisheria, tuviachie vyombo vifanye kazi yake,” anasema Shekidele.

Kwa upande wake, Mbunge wa Sengerema, Khamis Tabasamu, anasema amesikitishwa na namna watumishi hao walivyokosa uadilifu na kukwapua fedha zilizotolewa kuleta maendeleo kwa wananchi ambao ni wapiga kura wake pamoja na wa Rais pia.

“Hii wilaya ina watendaji wa ajabu. Inakuwaje watumishi hawa wa umma wamekosa uadilifu kiasi hiki mpaka wameamua kukwapua fedha zilizoletwa na Rais Samia kwa ajili ya maendeleo ya wananchi?” anahoji Tabasamu.