Wiki iliyopita makala hii inayomhusu Mtakatifu Valentino iliishia pale ambapo aliweza kuhamasisha upendo na taratibu watu walianza kujirekebisha na upendo ukaanza kurudi ndani ya ndoa.  Hata hivyo Mfalme Claudio alimchukia Valentino na kumfunga gerezani. Endelea…

Wachumba walifundishwa na Valentino kwamba upendo wa kweli wa wapendanao hujidhihirisha katika kufunga ndoa mbele ya Mwenyezi Mungu.  Hivyo, aliwakemea bila woga vijana wengi waliokuwa wakiishi maisha ya unyumba.

Vijana wengi wakafunga ndoa, jambo hilo lilimkera sana mfalme kuona kwamba watu wengi wanaingia katika dini ya Kikristo.  Pia aliwatetea vijana waliokuwa jeshini ambao walikatazwa kwa sheria ya mfalme wasifunge ndoa.

Sheria hiyo iliwanyima wanajeshi maisha ya ndoa kwa imani kuwa askari hodari hawatakiwi kuishi maisha ya ndoa.  Mtakatifu Valentino alipigania haki ya hao askari na kuwataka watawala waibatirishe sheria hiyo potofu.

 

Katika kuwasaidia watu watambue utakatifu wa ndoa, Mtakatifu Valentino alifanikiwa kuwafungisha ndoa wachumba wawili (mmoja Mkristo na mwingine alikuwa mpagani), ambao wazazi wao walikuwa wamewawekea vikwazo.

Mchumba wa kike ambaye ni Mkristo alikuwa mgonjwa na yule wa kiume ambaye ni mpagani alikuwa ni askari.  Askari aliambiwa eti si vizuri aoe kwani maisha yake yamo daima hatarini, hasa wakati wa vita, hivyo atamwacha mkewe kuwa mjane.

Na yule binti pia aliambiwa asiolewe eti kwa kuwa yeye ni mdhaifu, hivyo anaugua mara nyingi itakuwa ni vigumu kutimiza wajibu wake wa nyumbani. Mtakatifu Valentino aliingilia kati na kuwafundisha wazazi wa vijana hao kuwa upendo hauna mipaka wala ubaguzi.

Pia wale wachumba akawafundisha kuwa katika ndoa ni lazima kupendana katika taabu na raha, afya na magonjwa, na kuheshimiana daima. Mtakatifu Valentino alifanikiwa kumbatiza askari na kumfungisha ndoa kwa yule binti ambaye alikuwa taabani mgonjwa kitandani.

 

Mwaka 269 Mfalme Aureliano alimkataza rasmi Valentino kuhubiri na kuwafungisha watu ndoa takatifu. Mtakatifu Valentino aliendelea kumshuhudia Kristo bila woga na akawa tayari kwa lolote ila tu upendo wa Kristo uhubiriwe.

Mwaka 270 mfalme alimhukumu Valentino adhabu ya kufungwa gerezani kwa miaka mitatu. Februari 14, 273 kwa amri ya mfalme, Mtakatifu Valentino aliuawa kwa kukatwa kichwa.

Hukumu hiyo ilitolewa kwa sababu Mtakatifu Valentino alikuwa amewabatiza watu wengi na kuwafungisha ndoa takatifu ya mume na mke mmoja, wanaotakiwa kudumu katika uaminifu, upendo na umoja.

Katika miaka mitatu aliyofungwa gerezani kabla ya kukatwa kichwa, Mtakatifu Valentino alifaulu kumhubiria mkuu wa gereza na kumwongoa.

Vilevile binti mmoja wa mkuu wa gereza ambaye alikuwa kipofu alifanyiwa muujiza na Mtakatifu Valentino akapata kuona. Mkuu wa gereza alibatizwa yeye na familia yake na akafunga ndoa takatifu.

Tarehe 14 mwezi Februari, mwaka 273 ambayo ndiyo siku ya kuuawa kwake, Mtakatifu Valentino aliwaandikia barua watu wengi aliowafungisha ndoa akawasihi wadumu katika upendo, uaminifu na umoja.

Kila barua aliyoandika mwishoni iliandikwa: “Ndimi Valentino wako.” Maneno hayo yakawa ni kielelezo cha upendo wa Mtakatifu Valentino kwa watu wote kuwa yeye aliishi na kufa kwa ajili ya kuwapenda watu wote kama Kristo alivyosema: “Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama nilivyowapenda ninyi.”

By Jamhuri