Mawazo ni mtihani. “Mawazo yana nguvu kuliko bunduki,” alisema Joseph Stalin. Mawazo yakisongana yanaleta msongo wa mawazo. Msongo wa mawazo unadhoofisha mwili. Mawazo ni mtihani. Chunga mawazo yako yanazaa maneno.

Chunga maneno yako yanazaa matendo. Chunga matendo yako yanazaa tabia. Chunga tabia yako inazaa desturi. Chunga desturi yako inazaa hatima yako. Yote yanatokana na mawazo. Kuna upande mzuri wa mawazo. Mawazo yanaleta mabadiliko chanya.

“Kwanza inakuja fikra, halafu mpangilio wa fikra kuwa mawazo na mipango; halafu mipango hiyo inabadilishwa na kuwa ukweli. Utakavyogundua mwanzoni vipo kwenye kupiga picha kwako ya kiakili,” alisema Napoleon Hill.

Wazo lolote mbadala wa kitu usiliache lipae kama moshi wa ubani. Wazo ambalo limeiva na wakati wake umefika si la kuahirisha.

“Hakuna jeshi ambalo linaweza kukabili nguvu ya wazo ambalo muda wake umefika,” alisema Victor Hugo. Kila mara kuwa na wazo mbadala au fikiria kiuwezekano.

Dk. Robert H. Schuler wa Marekani alipendekeza kanuni kumi juu ya kufikiria kiuwezekano. Kanuni chache naweza kuziweka katika maneno yangu kama ifuatavyo:

Kanuni ya kwanza, usikatae wazo linalowezekana kwa vile kuna jambo ambalo si sahihi na wazo hilo. Kila wazo zuri linazungukwa na mambo hasi.

Kila fursa inazungukwa na mambo hasi. Tenganisha hasi na uwezekano. Usiliue wazo. “Mawazo ni magumu kuyaua zaidi ya watu, lakini mwishowe mawazo yanaweza kuuawa,” alisema Neil Gaiman wa Marekani.

Kanuni ya pili usikatae wazo kwa vile hautapata sifa. Uamuzi wako usijikite kwenye kusifiwa na  kujipendelea bali kujipenda na kuipenda jamii. Inawezekana usipate sifa kutokana na wazo lakini ukapata riziki.

Kipi bora, sifa au riziki? “Wewe ni mvumbuzi na unaiwakilisha jamii ya binadamu, na jambo zuri sana unaloweza kulifanya ni kuleta tena mawazo mapya, kwa sababu dunia yetu inahatarishwa na kutokuwepo mawazo mazuri,” alisema Terence McKenna.

Kanuni ya tatu, usikatae wazo kwa vile haliwezekani.  Mwanzo mgumu, kila wazo zuri mwanzoni linaonekana haliwezekani. Wazo la kuwa na ndege ya kuruka angani lilionekana haliwezekani. “Ukitaka jambo jipya, uache kufanya jambo la zamani,” alisema Peter Drucker.

Kanuni ya nne, usikatae wazo kwa sababu umekwisha kufanya uamuzi au kujiwekea msimamo.  Watu wasiobadili mawazo yao ni wakamilifu au wasumbufu. John Cage alisema: “Sielewi kwa nini watu wanaogopa mawazo mapya. Ninaogopa mawazo ya zamani.”

Kanuni ya tano, usikatae wazo kwa vile hauna nguvu ya pesa au nguvu watu. Tumia rasilimali  kidogo ulizonazo kutekeleza wazo lako. Bwana wetu Yesu Kristo hakuwa na nguvu ya pesa au nguvu ya watu.

Aliazima mtumbwi wa Simoni Petro. Aliazima mwanapunda.  Alianza kazi na mitume kumi na wawili na wafuasi sabini na wawili. Alifanya mawazo yake na mafundisho yake yawepo.

Kanuni ya sita, usikatae wazo kwa vile si namna yako ya kufanya mambo. Jambo ambalo linafanya iwe vigumu vijijini kuleta mambo mapya ya maendeleo ni baadhi ya watu kukataa mawazo mapya kwa vile si namna yao ya kufanya mambo.

Kanuni ya saba, usikatae wazo kwa sababu linaweza kushindwa. Waliokwenda mwezini hawakukataa wazo, kwa sababu lingeweza kushindwa. Wazo la kwenda mwezini walilifanyia kazi. Mawazo ni mtihani, mawazo mazuri yafanyie kazi.

Please follow and like us:
Pin Share