Walimwengu wanatambua wasanii wa muziki ni kundi ambalo linatoa mafunzo yenye maarifa mbalimbali kwa jamii. Tungo zao hutazamwa kwa shauku kubwa, kwa matarajio ya kuelimisha na kuburudisha jamii. Aidha, ndimi zao zinatawaliwa na adabu.

Katika fasihi hii namtazama mwana mama Siti bint Saad, aliyekuwa mwimbaji maarufu wa nyimbo za taarabu katika Kisiwa cha Unguja. Alitumia hekima na busara zipi kuvuta hadhira katika Afrika Mashariki na kukwepa mishale ya matusi, dharau na kashfa?

Katika kipindi cha miaka 70, dunia ilipata kushuhudia uhai, ufinyanzi na burudiko la sauti tamu na ya kuvutia ya binti Afrika, aliyetambulika na majina mawili: Mtumwa bint Saad ndani ya miaka 31 ya utotoni na ujanani: na Siti bint Saad ndani ya miaka 39 ya utu uzima wake.

Siti alikuwa binti wa wazazi Waafrika wa makabila mawili. Kiumeni alikuwa Mnyamwezi na kikeni alikuwa Mzigua. Wazazi wake walikuwa wazaliwa wa Kisiwa cha Unguja. Baba alikuwa mkulima na mama alikuwa mfinyanzi.

Siti ni mtoto wa kwanza katika uzawa. Alifuatiwa na ndugu watatu; Musa, Mbaruku na umbu Masika. Alipata kuolewa na Rajabu na walijaliwa kupata mtoto wa kike, aliyeitwa Mariamu.

Enzi ya utoto wake Siti hakubahatika kwenda madrasa wala skuli bali alifunzwa na mama yake ufinyanzi na uchuuzi wa vyungu mitaani, na ukubwani alifundishwa lugha ya Kiarabu na kuimba, na Muhsin Ali – mpiga udi katika Kijiji cha Unguja.

Siti alikuwa mwimbaji peke yake mwanamke wa kwanza katika Kisiwa cha Unguja. Mwaka 1911 alijiunga na jumuia ya taarabu akiwa na watribu watano; Subeti Ambari – mpiga udi, Buda Swedi – mpiga gambusi, Mwalimu Shaaban – mpiga tari, Muhsin All – mpiga udi na Mbaruku.

Uhai wa binti huyu ulianzia mwaka 1880 katika Kijiji cha Fumba na kukoma mwezi Juni, 1950 katika mji wa Unguja. Kazi zake zilimwezesha kufika vijiji vya Fumba, Mtoni na Unguja kuuza vyungu na kusafiri Afrika Mashariki na Bara Hindi kuburudisha na kurekodi santuri.

Siti alikuwa mwanamke mcha Mungu wa sala na saumu. Alisali vipindi vitano kila siku, akafanya faradhi na suna, katika maisha yake yote. Aliweza kutimiza ibada zake na kazi zake za sanaa bila kuleta migongano. Je, leo wapo wasanii wangapi wenye mwenendo kama huu?

Siti bint Saad alichunga sana ulimi wake katika kutamka maneno. Mashairi yake yalibeba hadhari, heshima na unyenyekevu kwa hadhira na jitihada kubwa ilifanywa kukwepa vijembe, mipasho, dharau, wivu na fitina kwa sababu hakuviridhia. Je, waimbaji wangapi leo wanafuata adabu kama hii?

Inaelezwa katika simulizi mbalimbali, wakati fulani Siti aliimbwa na kusemwa na jumuia moja ya taarabu ya mjini Unguja. Inasema:

Siti bint Saad, Ulikuwa mtu lini, 

Ulitoka shamba, Na kaniki mbili chini,

Kama si sauti, Ungekula nini? 

Maneno haya dhahiri ni ya shari, kedi na masimango. Busara inahitajika katika kujibu tungo hii kwa njia mbili, ama kujibu kwa fahamu au kuwa kimya. Lakini si wasanii tu wanaopata mashaka kama haya, hata viongozi, wanasiasa au watu wa kawaida wanakumbwa na joto kama hili.

Siti alitambua shari hii na busara zilimwelekeza kujibu ifuatavyo akiwa na lengo la kufunza watu adabu. Alisema:

Si hoja uzuri, Na sura jamali, 

Kuwa mtukufu, Na jadi kubeli, 

Hasara ya mtu – Kukosa akili. 

Majibu haya ni mwiba uliokwama kooni. Siti hakupenda wala hakutaka malumbano yasiyo na afya au neema. Yeye alitambua uzuri si mali, bali akili ndiyo mali. Je, msanii wewe unatambua vijembe si mali au si adabu?

Please follow and like us:
Pin Share