Hofu yatanda Katiba mpya

*Ananilea: Rais akipenda ataokoa jahazi

 

Wingu zito limetanda juu ya mchakato wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya viongozi wa dini na wanaharakati kutabiri kifo chake.

Baadhi wamekosoa mfumo wa Bunge Maalum la Katiba, na wengine wametahadharisha kuwa chombo hicho badala ya kuwezesha upatikanaji wa Katiba inayotakiwa na Watanzania, kinaweza kuzusha vurugu nchini.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki, viongozi wa kiroho na wanaharakati mbalimbali wametaka mamlaka husika zichukue hatua haraka kumaliza msuguano mkubwa wa kisiasa unaoendelea kushika hatamu baina ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.

Wamesema taswira ya mwenendo usioridhisha katika uendeshaji vikao vya wajumbe wa Bunge hilo mjini Dodoma, unaashiria kuua matarajio ya kupata Katiba yenye tija kwa Watanzania.

Ananilea aelekeza lawama kwa Rais

Mkurugenzi mstaafu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Ananilea Nkya, amesema Rais Jakaya Kikwete hawezi kukwepa lawama kutokana na kuyumba kwa mchakato wa Katiba mpya.

“Mimi binafsi kama Mtanzania, naiona changamoto kubwa, wanaomshauri Rais wanamshauri vibaya, kinachoendelea bungeni hakitawezesha upatikanaji wa Katiba itakayokidhi mahitaji ya Watanzania,” amesema.

Hata hivyo, Nkya, ambaye ni mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu na maendeleo ya wanawake na watoto, anaamini kwamba Rais Kikwete anaweza kunusuru hali ya hewa isiendelee kuchafuka katika Bunge Maalum la Katiba.

“Sauti ya Rais ni kubwa, nina imani bado ana nafasi ya kuelekeza na kutoa kauli itakayosaidia mchakato wa Katiba kwenda vizuri,” amesema Nkya.

Kwa upande mwingine, Nkya ameelezea kutoridhishwa kwake na michango ya viongozi wa Serikali na wanasiasa wengi katika mchakato wa Katiba mpya, lakini pia katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo lukuki yanayoendelea kuwanyima Watanzania maendeleo ya kweli.

“Katika suala hili la Katiba, viongozi walipaswa kuwa wawezeshaji kama vile kuwaeleza wananchi faida na hasara za Serikali mbili na Serikali tatu, lakini badala yake wanatoa uamuzi. Mimi nasema viongozi wakubali kubadilika.

“Lakini pia, kuendelea na mawazo mgando siamini Nyerere [Mwalimu Julius Nyerere] na Karume [Abeid Amani Karume] wangekuwa hai wangeendelea kusimamia kile kile,” ameongeza.

Nkya pia ni miongoni mwa wananchi waliotangaza kutounga mkono uamuzi wa kuwashirikisha wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge Maalum la Katiba.

“Wajumbe wa Bunge la kawaida [Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania] hawakupaswa kuwa kwenye Bunge la Katiba, kilichotakiwa hapo ni Bunge la Muungano kupeleka wawakilishi wao wachache kwenye Bunge la Katiba kama ilivyofanyika katika taasisi nyingine,” amesema Nkya, huku akidai hali hiyo imechangia kuvuruga vikao vya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.

Akizungumzia misimamo ya vyama vya siasa kuhusu muundo wa Serikali, Nkya alisema hilo ni kosa linaloweka mwanya wa mgawanyiko wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.

Kitima: Wajumbe wamesahau mambo muhimu

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania (SAUTI), Padre Charles Kitima, ameelezea kushangazwa kwake na hatua ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kujikita zaidi katika suala la muundo wa Serikali na kuweka kando mambo mengine mengi yenye maslahi kwa wananchi.

“Kuna mambo mengi ya msingi kama vile haki za binadamu, tume ya uchaguzi, utawala bora na umilikaji ardhi, tulitegemea sana hiyo Katiba ije na suluhisho la hayo. Masuala hayo yote bado hayajaongelewa na kupewa nafasi bungeni. Lakini wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wamezama kwenye muundo wa Serikali,” amesema Padre Kitima na kuongeza:

“Bado Tume ya Uchaguzi imeendelea kuwa chombo cha dola [Serikali]. Tunataka kiwe chombo cha wananchi ili kuondoa mwanya wa kuchakachuliwa [kuhujumiwa]. Watanzania watajitawala kama Tume hiyo itakuwa yao.”

Kuhusu uamuzi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kususia vikao vya Bunge Maalum la Katiba, mtazamo wa kiongozi huyo wa kiroho ni kwamba hatua hiyo itawezesha marekebisho yatakayosaidia kupata Katiba mpya yenye maslahi kwa umma.

“Binafsi ninaunga mkono UKAWA kususia vikao. Katika nchi ya kidemokrasia na watu walio huru kutoa maoni yao; kuvutana, kutofautiana na kusuguana ni kupanuka kwa mawazo.

“Wakiendelea hivi wanavuta muda wa kuelewa na kujifunza ili kutengeneza Katiba ya nchi. Kususia kwao ni kuonesha kuwa hawapendi kuonewa. Tuwaache watoke, na walio ndani tuwaache, lakini mwisho wote watakaa pamoja. Wasipuuzwe kwa sababu ya uchache wao maana ni wawakilishi wa wananchi.”

Hata hivyo, Padre Kitima amewakumbusha wapinzani kufahamu kwamba siyo kila kitu wanachotaka lazima kikubaliwe na kila mtu.

Maghoba: Wapinzani wamesusia, CCM wanashangilia

Mbunge mstaafu wa Kigamboni, Dar es Salaam, Frank Maghoba, amekosoa kitendo cha UKAWA kususia vikao vya Bunge Maalum la Katiba akisema kitawapa wanachama wa Chama Cha  Mapinduzi (CCM) mwanya wa kuunda Katiba inayotetea maslahi yao.

“Nina hofu kwamba Bunge halitafanikisha upatikanaji wa Katiba mpya ya Watanzania. UKAWA wamesusia vikao, hivyo hawatapata fursa ya kutoa michango yao. CCM ndiyo itatengeneza Katiba.

“Ninaamini upinzani ungesaidia kupatikana kwa Katiba mpya. Hatuwezi kupata Katiba mpya kwa kususia vikao. Wapinzani walichopaswa kufanya ni kulalamika na kupigania haki zao wakiwa ndani ya Bunge,” amesema Maghoba.

Amehimiza dhana ya kuruhusu uhuru wa watu kutofautiana mawazo ndani ya vyama vya siasa, akisema hali hiyo itasaidia kufanya uamuzi wenye maslahi kwa umma.

Mwenyekiti wa wastaafishwa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rashid Mohamed, yeye amesema, “Mimi mambo ya siasa siyapendi, lakini nina wasiwasi kwamba huenda mchakato wa Katiba mpya ukakwamishwa na mvutano wa kisiasa unaoendelea kutawala Bunge Maalum la Katiba.”

Mchungaji Mwita: Mungu atasaidia kupata Katiba

Mchungaji wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Tarime mkoani Mara, Ezekiel Mwita, amesema kinachotakiwa sasa ni Watanzania wote kumwomba Mungu awajalie wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba uelewano utakaofanikisha upatikanaji wa Katiba bora.

“Kilichobaki ni kufanya maombi, tumwombe Mungu awajalie wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba hekima, upendo, umoja na uelewano ili waweze kutimiza matarajio ya Watanzania ya kupata Katiba itakayowafaa.

“Tumwombe Mungu awajalie wajumbe wa Bunge hilo waone na kutanguliza maslahi ya Taifa, wafikie mwafaka utakaoamua Katiba itakayokubalika kwa Watanzania,” amesema Mchungaji Mwita.

Naye Dk. Sayi Inundo wa mkoani Simiyu ameelezea kutoridhishwa kwake na mwenendo wa mchakato wa Katiba mpya, huku akitahadharisha kwamba kukwama kwa shughuli hiyo muhimu kunaweza kusababisha vurugu na kutowesha amani hapa nchini.