Wanasema mnyonge mnyongeni lakini haki
yake mpeni. Ndivyo Mpita Njia (MN)
anavyoweza kusema baada ya kupata huduma
katika Hospitali ya Sinza (Sinza Palestina).
Tangu zama za Awamu ya Pili ya uongozi wa
taifa letu, Mpita Njia amekuwa mgumu
kuziamini huduma zinazotolewa kwenye
hospitali za umma.
Enzi zake, wakati wa Mzee Kifimbo, Mpita Njia
anakumbuka namna wagonjwa walivyodeka.
Walitibiwa bure. Waliolazwa walipewa chaguo
la chakula walichopenda kula kwa siku hiyo.
Kila huduma ilipatikana hospitalini – kuanzia
chakula, malazi, viburudisho na hata kauli
njema za madaktari, wauguzi na wafanyakazi.
Zama hizo za Ujamaa zilikuwa za ujamaa kweli.
Hata sindano tulishirikiana! Zilichemshwa
kwenye ‘stovu’ na zikatumiwa na wagonjwa
zaidi ya mmoja. Hayo yakafutwa na ujio wa
janga la ukimwi.

Awamu zilizofuata huu uhondo ukatoweka. Hali
ikawa mbaya tulipotakiwa ‘tuchangie’ huduma
za matibabu. Hapo mwanya wa rushwa
ukapenya. Kila kitu kikawa pesa – kuanzia
kupimwa malaria hadi kuhifadhi maiti.
Hadi wiki iliyopita MN kichwani mwake alijua
mambo ni mabaya kwa kiwango hicho. Kwa
shingo upande akajikuta anakwenda Sinza
Palestina ili walau, pamoja na uzee alionao,
ajue kiungo gani kinahitaji kufanyiwa sevisi.
Akapokewa kwa bashasha na wahudumu wa
hospitali hiyo. Akaelekezwa kwa daktari.
Akapokewa vizuri. Daktari akamweleza kuwa
hawezi kumhudumia hadi awe ameingizwa
kwenye ‘system’. MN akasindikizwa na kijana
aliyevaa kikoti chenye maandishi ‘Niulize mimi’
hadi kwenye dirisha la kujiandikisha na pia
malipo.
MN akarejea kwa daktari. Akaandikiwa vipimo
vya aina tatu. Akaenda maabara. Huko
akapokewa vizuri. Akachukuliwa vipimo na
kutakiwa asubiri kwa dakika kadhaa. Akafanya
hivyo.
Punde, akaitwa na kuambiwa aende akamwone
daktari. Huko akapokewa na kuandikiwa dawa
kwa uungwana usio kifani. Akaenda dirishani
kupata dawa. Kati ya dawa tatu alizoandikiwa,
akapata mbili. Hiyo moja aliyokosa hapo
hospitalini bei yake ni Sh 15,000; lakini
alipokwenda kuinunua kwenye duka binafsi nje,

akakung’utwa Sh 35,000. Hapo ni tofauti ya Sh
20,000. Mpita Njia akawa na maswali mengi,
lakini moja ni kwanini hakuna bei elekezi
kwenye dawa? Kwanini duka la serikali likose
dawa, lakini duka binafsi liwe nayo? Hayo
anawaachia wahusika.
Mpita Njia anasifu huduma zinazotolewa na
wafanyakazi wa Sinza Palestina. Jambo moja
anapenda kuushauri uongozi wa Sinza
Palestina. Nalo ni kuhakikisha madaktari,
wauguzi na wafanyakazi – kwa kadiri ya vitengo
vyao – wanavaa sare. Inapendeza kumwona
muuguzi akiwa amevalia nadhifu, juu kichwani
akiwa na kale ka-kitambaa kalikokunjwa kwa
majonjo.
Inapendeza kumwona daktari akiwa amevalia
joho jeupe na ‘Stethoscope’ shingoni.
Inapendeza kuwaona wale vijana kwenye
madawati ya maulizo wakiwa kwenye sare
maridhawa ili kuwatofautisha na wagonjwa na
hata matapeli.
Kwa hilo Mpita Njia ameona aushauri uongozi
wa Hospitali ya Sinza Palestina, waangalie
uvaaji wa sare kwa wafanyakazi wao, kwa kada
zote. Kwa kufanya hivyo watakuwa
wameongeza ladha kwenye huduma zao nzuri
wanazotoa. Hongereni Hospitali ya Sinza
Palestina.

.tamati….

3824 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Tags :
Show Buttons
Hide Buttons