Na Deodatus Balile

Leo zimepita wiki mbili bila kuandika katika
safu hii. Makala yangu ya mwisho niliahidi
kuandika yaliyojiri katika safari ya mwisho
niliyokwenda Mwiruruma, Bunda kumzika
Comrade Shadrack Sagati (Mungu ailaze
mahala pema peponi roho yake). Sentensi
ya mwisho katika makala yangu ilisema:
“Olwo mumywanyi wawe kufa afelwa.” Hii
ina maana, kuliko rafiki yako kufariki dunia,
ni bora afiwe.
Sitanii, nilifika Mwiruruma kijijini kwa kina
Sagati majira ya saa 09:00 alfajiri. Ni
mwambao wa Ziwa Victoria. Tuliwakuta
wanakijiji wakitusubiri. Nilimkuta mzee
Sagati mwenyewe. Vilio vya wanakijiji
vilikuwa vingi. Sagati inaonyesha alikuwa
mtu wa watu. Wanawake kwa wanaume
wakati tunashusha mwili wa Sagati

walikuwa wanaangua vilio. Nami nilirejea
kulia upya.
Jumamosi iliyofuata tuliendesha ibada pale
nyumbani. Walikuwapo watu wengi mno.
Tulimzika Sagati. Kimsingi sitaki kuendelea
na simulizi hii. Maana kila ninapoandika
majonzi yanarejea, machozi yananitoka.
Nenda Sagati. Kamsalimie Nyerere.
Msalimie Mandela. Naamini huko uliko
unatuona na unaona tunavyosononeka.
Raha ya milele umpe ee-Bwana, na
mwanga wa milele umwangazie. Apumzike
kwa amani.
Sitanii, wiki iliyofuata siku ya Alhamisi jioni
nikapata simu kuwa shemeji yangu
Desmond Deogratias amefariki dunia.
Sikuwa na namna, zaidi ya kuanza safari ya
kwenda mazikoni Bukoba. Niliendesha gari
usiku kucha. Wapo ndugu zangu wengi
walionipigia simu kunipa pole na wakati
mwingine kuniuliza masuala ya kikazi nikiwa
njiani, sikupokea. Mniwie radhi. Kuendesha
kilomita 1,430 Dar es Salaam – Bukoba si
mchezo.
Nilifika Bukoba, bahati nzuri mke wangu
Dafrosa alitangulia akawahi maziko, ila mimi
nilifika usiku saa 04:00 na maziko
yalifanyika saa 10:00 jioni. Nimeshiriki

msiba. Ni majonzi. Desmond ameacha
watoto. Mtoto wake wa kwanza yuko
sekondari. Ni bahati mbaya kuwa mke wa
Desmond naye alikwisha kufariki dunia
yapata miaka 15 iliyopita. Kwa kweli ni
majonzi.
Sitanii, nimerejea Dar es Salaam
Jumamosi, Jumapili nikasikia dada wa Rais
John Magufuli, Monica, naye amefariki
dunia. Kampuni ikamteua Mkinga Mkinga
kwenda Chato si tu kushiriki maziko, bali pia
kuchukua matukio na taarifa mbalimbali.
Tunamwombea dada Monica, Mungu ailaze
mahala pema peponi roho yake. Kwangu
mimi hizi siku zimekuwa za masikitiko.
Katika kuhitimisha wikiendi, nikaenda
Zanzibar.
Leo msomaji wangu utaniwia radhi.
Nimeanza makala yangu na masuala
yanayohusu misiba, ila maisha lazima
yaendelee. Tunafahamu kuwa sote ni njia
yetu na hakuna kila mwanadamu
aliyezaliwa atakayekiepuka kikombe hiki.
Uwe mfupi, mrefu, una madaraka au hauna,
ipo siku utakufa, la msingi ni kuishi maneno
ya mwisho ya Sagati: “Tukifa tunaacha
alama gani maishani?”
Sitanii, katika safari hizi za kwenda misibani

nimepata fursa ya kutumia barabara kwa
umbali mrefu wa karibu kilomita 6,000 hivi
ndani ya wiki mbili. Nimepata fursa ya
kupitia Malampaka, Maswa, Simiyu na
hatimaye Lamadi. Safari ya Bukoba
nimetokea Dar es Salaam, nikapita
Kahama, Kanazi, Lusaunga, Biharamulo,
Muleba hadi Bukoba na baadaye nikaenda
Kilimilile.
Kuna jambo kubwa nimelishuhudia katika
njia hizo, nalo ni ujenzi wa barabara.
Nimepita katika miji mbalimbali ya nchi hii
ikiwamo Dodoma katika mwaka huu na
naangalia Dar es Salaam ujenzi wa
barabara mbalimbali unaoendelea.
Watanzania inawezekana bado tumepigwa
butwaa kuhusu mabadiliko katika Uhuru wa
Kuzungumza (Freedom of Expression), ila
Rais Magufuli kuna jambo analifanya, nalo
si jingine bali ni ujenzi wa miundombinu.
Hakika Rais Magufuli anajenga barabara.
Kasi inayoendelea ya ujenzi wa barabara
kufikia mwaka 2020 kuna kila dalili kuwa
sehemu kubwa ya nchi itakuwa inapitika
kwa mwendo wa kudumu. Mimi katika
maisha na uandishi wangu huwa nasifia
penye kustahili sifa na nasahihisha penye
kustahili marekebisho. Kwa hili la barabara
nasema kwa herufi kubwa HONGERA RAIS

MAGUFULI.
Ninaposema miundombinu, siishii kwenye
barabara tu. Mtaona gazeti letu siku zote
limekuwa na msimamo wa kupinga dhana
yoyote inayopinga ununuzi na umiliki wa
ndege. Msimamo huu tumeufikia kwa
kutambua faida za taifa letu kumiliki ndege.
Ukiwa katika mji kama Guangzhou, China
au London, Uingereza ndipo utaona faida
ya kumiliki ndege.
Sitanii, nchi kama Ethiopia ambayo ilikuwa
inaomba msaada wa chakula hivi
ninavyozungumza inatutimulia vumbi.
Shirika la Ndege la Ethiopia Airline lilipata
faida ya dola milioni 220 mwaka 2017,
karibu Sh bilioni 600. Hiyo ni faida
waliyoipata kwa kurusha ndege, bado ipo
faida ya watalii walioingia nchini humo na
mauzo ya maua nje ya nchi, ambapo sasa
Ethiopia inashika nafasi ya kwanza Afrika
kwa kuuza maua Ulaya.
Rais Magufuli pia anajenga Standard
Gauge, reli itakayorahisisha usafirishaji wa
mizigo na kuepusha barabara kuharibika
haraka. Barabara zetu zinapaswa kukaa
miaka 30 hadi 50. Isipokuwa barabara zetu
hizi zinaharibiwa na malori yanayojaza
mizigo kupita kiasi na matokeo yake

yanaharibu barabara. Nasisitiza hili la ujenzi
wa miundombinu analofanya Rais Magufuli
ni ukombozi kwa taifa letu. Mataifa yote
yaliyoendelea yamepata maendeleo kwa
kuwa na miundombinu imara.
Sitanii, wakati ujenzi ukiwa tamu ya Rais
Magufuli, anao upande wa pili wa shilingi.
Rais Magufuli anashughulikia yaliyokuwa
yakilalamikiwa miaka yote. Anaondoa kero
zilizokuwa zinatukwaza Watanzania na
kuona hakuna sababu ya kuendelea kuwa
na serikali. Nchi yetu hastahili kuwa taifa
maskini.
Rais Magufuli kazi anayoifanya ilipaswa
kufanywa na upinzani. Ndiyo maana mwaka
wa kwanza wa Rais Magufuli madarakani,
tumeshuhudia kila mtu akishangilia utendaji
wa Rais Magufuli. Kila awaye ameona
anaondoa kero. Bahati mbaya moja tu, na
nieleweke vizuri, bahati mbaya moja
iliyopata serikali ya Rais Magufuli ni ushauri
aliopewa (sijui na nani) wa kuzuia watu
wasiseme.
Kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali anapofanya uchunguzi
na kubaini wizi au matumizi mabaya ya
fedha za umma, njia kuu ya kuzuia
yaliyobainika yasitokee tena ni kuwapa watu

fursa ya kuzungumza wakakemea. Rais
hawezi kuona kila kitu. Waandishi wa
habari, vyama vya siasa na watu wengine
wametandaa sehemu nyingi nchini.
Sitanii, hawa wanatembea macho yakiwa
wazi. Mikutano ya hadhara kwa mfano
imekuwa ikitumika kuonyesha wizi uko
wapi. Kwa kufanya hivyo, rais angepata
fursa ya kubana wakwapuaji. Lakini ni
bahati mbaya sasa hakuna mikutano ya
hadhara ya vyama vya siasa. Hawa kama
hawatumii mikutano kukejeli, wanasaidia
kuonyesha “panya amekimbilia wapi”.
Suala jingine linaloleta shida ni ‘mchezo’ wa
wabunge kuhama vyama kila mwezi tukawa
na uchaguzi. Nafahamu serikali inataka
kudhibiti mpango huu, ila nasema hizi siasa
za wabunge kuhama kutoka upinzani au
chama tawala na watu wale wale
wakateuliwa na kupitishwa kugombea
ubunge si siasa safi. Hili nakushauri Rais
Magufuli uliangalie kwa kina linaweza
kuchafua taswira yako mbele ya jamii na
wapiga kura.
Sitanii, waruhusu wananchi waseme kero
zao nawe uwasikilize, kwa kufanya hivyo
utabaini wapi kuna tundu kwenye neti na
kuliziba mara moja. Nakuhakikishia kwa

mwenendo wa sasa unaweza kuishia
kusikitika mbele ya safari ukibaini kuwa
kuna wasaidizi wako wametumia fursa ya
serikali ‘kuogopwa’ wakaandaa mikakati
yenye manufaa binafsi kwako na si kwa
taifa.
Naomba kuhitimisha makala hii kwa
kusema kuwa uongozi wa Rais Magufuli
una utamu wake, lakini sehemu hii
niliyohitimisha nayo yenye uchungu kwa
kuwanyima watu fursa ya kukutana na
kusema wazi wanachodhani sicho,
irekebishwe.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share