Naanza kwa kusema chereko chereko na hongera, pia kwa kutamka ‘Congratulations and Celebrations’ kwa gazeti Jamhuri kutimiza mwaka tangu kuingia sokoni mnamo Disemba 6, 2011 hadi leo. Vilevile natoa heko kwa waandishi wa habari kuliendesha gazeti hili hadi sasa, kwa umakini na utulivu, ndani ya soko la usambazaji wa habari kwa jamii.

Kwa mujibu wa kalenda yoyote, mwaka mmoja ni hatua ya kwanza kuelekea miaka mingi ya mafanikio au ya hasara. Ni muda mfupi sana. Lakini katika mawanda ya makuzi au ya kutenda jambo; mwaka mmoja ni kipindi kirefu. Ni kipindi cha kuonesha uwezo, ubora au udhaifu wa umri wa mtu au mafanikio ya maendeleo yaliyopatikana ndani ya jamii fulani.

 

Katika kipindi hicho gazeti Jamhuri limefanikiwa kuelimisha jamii ya Watanzania kwa kuzingatia misingi na kanuni za uandishhi wa habari. Mafanikio chanya na hasi yamepatikana na changamoto mbalimbali wakati wa utekelezaji wa maadili ya taaluma hiyo.


Natarajia katika kipindi hiki kipya cha mwaka wa pili changamoto za zamani na mpya zitapatiwa ufumbuzi wa kitaaluma, hivyo kutoa mvuto kwa wadau wengi zaidi hasa wasomaji wa gazeti hili kuingia sokoni mara dufu.


Changamoto maalum itawavaa wamiliki wa gazeti na wadau wanaochangia kuandika makala mbalimbali kubuni na kutumia mbinu mpya za taaluma ya uandishi wa habari, kwa lengo la kuliwezesha gazeti Jamhuri kuhimili vishindo vya soko, liweze kusonga mbele. Mungu libariki gazeti Jamhuri.


Kwa mtazamo wa juju, gazeti Jamhuri ni karatasi zilizopangwa kwa ustadi na kujazwa maneno matamu ya kufurahisha na machungu ya kukera nafsi ya mtu yeyote atakayebahatika kusoma toleo la gazeti hili.


Gazeti hili linajinasibu kwa kaulimbiu yake, ‘Tunaanzia wanapoishia wengine’. Kauli mbiu hii mimi inanipa tafsiri ya kweli sifa ya sura mbili. Sura ya kwanza ni ya nje yenye kutambua kuwa magazeti yaliyolitangulia na yaliyopo yameandika mengi kuhusu habari, elimu na burudani ikiwa ndilo jukumu hasa la vyombo vya habari. Ama kwa hilo wote wanastahili heko na hongera.


Sura ya pili ni ile ya ndani yenye nguzo tatu kuu. Nguzo ya kwanza Jamhuri halifungamani na chama chochote cha siasa, wala mwanasiasa yeyote, achilia mbali mfanyabiashara kwani wote hao ni bure aghali.


Nguzo ya pili ni gazeti linalosimama katika kweli na haki, kwa kutoa makala zenye habari sahihi, sanifu na kamilifu kutoka kwenye vyanzo vya habari kwa kuzingatia kanuni za uandishi wa habari.


Ama kwa nguzo yake ya tatu ni kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha babu yake; wajina wake Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inadumu, kwa kuhimiza mijadala ya kuuboresha Muungano wetu kwa maslahi ya Watanzania wote.


Nathubutu kulinganisha umri wa gazeti Jamhuri na baadhi ya magazeti mengine nchini kama ni kilembwe kwa gazeti la Kiongozi (tangu 1905). Ni mjukuu kwa magazeti ya Uhuru na Daily News kwenye mika ya ‘60 yalipoanzishwa.


Si hivyo tu, Jamhuri ni mtoto mbele ya  gazeti la An-Nur. Kaka zake ni Nipashe, Raia mwema. Na mdogo wake ni gazeti la Kisiwa. Nimetaja magazeti hayo kwa uchache kati ya mengi yaliyopo na wala si kwa ubora la hasha. Bali ni kuweka msisitizo wa kuwepo kwa vyombo vya habari nchini.


Pamoja na kuwa umri wake ni mdogo, Jamhuri limeweza kuonesha umahiri wake katika makala za habari na uchambuzi kuhusu uchumi, siasa, afya, elimu na utamaduni. Limesifu palipostahili sifa. Limekemea palipokuwa na kasoro na limekosoa palikuwa na makosa.


Safu za Nyundo ya Wiki, Sitanii, Jamhuri ya Waungwana, Fikra ya Hekima, Anga za Biashara na Uchumi, habari mabalimbali, matangazo na michezo ni lishe bora zilizojenga siha yake. Siha ambayo imetoa mvuto na kusuuza nyoyo za wasomaji mbalimbali hata kuamua kumlea Jamhuri.


Waanzilishi wa gazeti hilo, katika tahariri yao ya kwanza Disemba sita, 2011 wamesema, “Disemba 6, 2011 itabaki kuwa siku muhimu mno kwetu waanzilishi wa Kampuni ya Jamhuri  Media Limited (JML), watangazaji na wasomaji wa gazeti Jamhuri.”


Wameendelea na kusema, “Tunasema ni siku muhimu kwa sababu tumetimiza ndoto ya matamanio yetu ya muda mrefu ya kuanzisha  na kuendesha chombo cha habari kinachomilikiwa na wanahari wenyewe. Kwa wataalamu wenzetu, tunawakaribisha tuunganishe nguvu na maarifa yetu.”


Kauli hiyo inaelekezwa kwenye ukombozi wa fikra na changamoto ya kuondoa umaskini kwa wanahabari. Inatukumbusha kwamba saa ya ukombozi imefika, kwa maana ya kuwa wakati ni huu. Hili linawezekana kwa kutoa mifano hai minne.


Kuanzishwa na kuendeshwa kwa Raia Mwema Company Limited, Authentic Broadcasting Media (ABM) Fm Radio, Jamhuri Media Limited na Veterans’ Electronic Media Association kuendeshwa na wanahabri wenyewe.


Nimezungumza Gazeti Jamhuri kama chombo cha mawasiliano na umma. Chombo ambacho kinaendeshwa na watu wenye taaluma ya uandishi wa habari na mawasiliano na umma. Hivyo, gazeti Jamhuri si maneno tu yaliyoandikwa ndani ya kurasa zake. Gazeti hili ni watu, ndio maana nilitoa kongole kwa wabunifu hao.


Wakati napongeza nakusifu Gazeti Jamhuri ukweli nawapongeza na kuwasifu waendeshaji na wasimamizi wa gazeti hili.


Kitendo cha kutimiza dhamira yao ya kuwa na chombo hicho ni ukombozi mkubwa sana. Ni ukombozi wa mawazo ya kukataa kuuza taaluma yao, nguvu zao na ujuzi kutumika kama chombo cha kuwapunja haki zao.


Ukombozi wa mawazo humtoa mtu yeyote ndani ya dimbwi la umaskini, uonevu, unyanyaswaji na unyonywaji. Humpeleka na kumzamisha ndani ya ziwa la haki, furaha na neema. Nalisema hili kwa sababu waandishi wa habari na watangazaji wengi tunashindwa kujikomboa kimawazo!


Sisi wanahabari ni mahodari mno kuwasema  wasiyo wanahabari kuwa hawajikomboi kimawazo, wanakumbatia umaskini. Ni kweli ni kazi yetu kuelimisha, kushawishi, kukemea na kukosoa. Lakini tunapohubiri ukombozi wa fikra au mawazo, sisi tunajikomboa ili tuwe mfano?


Tumeshauri, tumeelekeza na hata kutoa mbinu za uganguzi katika kuanzisha na kuendesha vikundi vya uchumi, umoja wa vikoba, vyama vya nguvu kazi na ujasiriamali na kadha wa kadha. Lakini sisi wenyewe hapana!


Ndiyo kwanza tunajigubika wimbo wa msanii mkongwe katika Afrika Mashariki katika muziki wa taarabu, Juma Bhalo. Katika wimbo wake mmoja una maneno, “Nalia mwenzenu nalia, natengeneza kwa wenzegu kwangu kuna poromoko.”


Maneno hayo ya msanii Bhalo wa Mombasa katika Jamhuri ya Kenya, nchi jirani na Tanzania, yanaonesha binadamu ana kasoro au upungufu katika utendaji wake wa kila siku. Binadamu huyo halazimishwi bali anafanya mambo kwa hiari yake. Pamoja na kuona kwake kunaporomoka lakini bado analia nakulalama kwa watu, ukweli binadamu huyo bado hajajikomboa kimawazo na kifikra.


Kwa hiyo, wanahabari tutambue kukiri upungufu huu si kitendo cha kujidhoofisha bali ni kitendo cha kujiamini na kujiimarisha. Tutoke huko kwani tunachekwa kwa kutengeneza kwa wenzetu.


Wanahari tukumbuke sisi ndiyo askari wa mstari wa mbele wa mapambano ya kujenga uchumi, kupiga vita ufisadi, kuondoa rushwa na kuboresha huduma za maendeleo ya jamii. Kwa mfano, afya, elimu, miundombinu ya barabara, kilimo na nishati kwa kutumia mawasiliano na umma.


Wananchi wanyonge na maskini watapata elimu bora zaidi na madhubuti kutokana na kalamu zetu zitakapokuwa hazina dosari za upendeleo, woga, vitisho wala kurubuniwa na kuzuiwa kuandika yale ambayo tunatambua ndiyo kweli.


Habari zenye ukweli na sahihi zitamkomboa mwananchi kutoka kwenye mzizima alionao wa kujinasua kiuchumi na kuwa katika joto la kumchangamsha kufanya mambo yake ya maendeleo kwa mipango.


Sitakuwa mkweli kama sitasema dukuduku langu la moyoni linalonisibu juu ya taaluma yetu ya uandishi wa habari na taaluma za wenzetu katika fani mbalimbali zinavyolindwa, kunyenyekewa na kuenziwa.


Vipi wanataaluma wengine mathalani, wahandisi, madaktari, wanasheria, wachumi na wafanyabiashara wanatumia taaluma zao kuanzisha, kumiliki na kuendesha kampuni za ujenzi, hospitali, benki, uwakili, viwanda vya uzalishaji mali na kadhalika; na wanawaajiri wanataaluma wenzao kufanyakazi nao.


Inakuwaje sisi wanahabari tuendelee kuwa watumishi wa taaluma nyingine kwa asilimia kubwa? Tatizo ni nini? Uwezo hatuna au hatuna umoja, mshikamano au ujinga? Wengi wetu tumekwishaonja dhuluma, udhalilishaji, uonevu hata kupewa mikataba ya ujanja ujanja na mengineyo mengi katika vituo vya kazi vya magazeti, redio na runinga.


Wengi wetu tunazijua kampuni chache za habari nchini zinazoendekeza kasumba ya kudhulumu na kupunja haki za wanahabari wao na hata zenyewe zinajijua kuwa zinafanya dhambi hiyo kwa makusudi kabisa!


Wanahabari tunatumika kufanya kazi katika mazingira magumu ya ajira kwa kulipwa ujira mdogo, kutolipwa ujira hadi kipindi fulani, ‘cheap labour, free labor/slaves labour na pia taaluma yetu kutothaminiwa na baadhi ya waajiri.


Wanahabari wenzetu wamekwisha kutuonesha njia kwa vitendo na kutuambia, “wanahabari kumiliki na kuendesha vyombo vya habari inawezekana.” Sasa tunasubiri nini? Lazima tujikomboe na tubadilike. Tukumbuke kuwa ‘ajizi nyumba ya njaa’.


Machache nimeyasema, Mwanahabari sikia.

Nakuhimiza mapema, La mgambo limelia

Anzisha choma mapema, Chenye asilia media.

Nakamilisha makala yangu kwa kusema, binafsi nina furaha na bashasha kupongeza na kutoa hongera kwa Raia Mwema Company Limited kutimiza umri wa miaka mitano tangu kuwa sokoni (31/10/ 2007-31/10/2012) katika mambo ya habari na mawasilano na umma.


Aidha, hongera kituo cha radio cha Authentic Broadcasting Media (ABM) Fm Dodoma kutimiza umri wa miaka miwili tangu kuwa hewani (01/08/2010-01/ 08/2012), pia hongera Veterans Electronic Media Association (VEMA) kupata usajili serikalini, Oktoba 05, 2012.


Mwisho, ndugu zangu wapenzi wangu na wamiliki wa Gazeti Jamhuri, ingawa mmefaulu na kumudu kuendesha  chombo hicho, ni vema mdumishe umoja wenu asilia. Muimarishe mshikamano wenu na mwepukane na urafiki na mapenzi kwani hizo ni kambi mbili zenye tabia ya kuzaa unafiki na ushenzi daima.


Mhariri Mtendaji, Balile usibweteke,

Ufunge wako mkwiji, Gazeti hili lineemeke,

Vibaka wanahitaji, Walizamishe Temeke.

Manyerere Mtendaji, Kamanda pasi makeke,

Usiruhusu walaji, Vikosi kula mateke,

Kumbuka chanzo mtaji, Siri yenu isitoke.

 

1046 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!