ARUSHA

NA MWANDISHI WETU

Idadi ya wazee nchini Tanzania inakadiriwa kuwa
asilimia 11 ya watu wote ifikapo mwaka 2050.
Hali hiyo inasababishwa na ongezeko la idadi ya
watu na kuboreshwa kwa huduma za afya nchini.
Mratibu wa Huduma za Afya kwa Wazee kutoka
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Dk. Edward Mung’ong’o, ametoa taarifa
hiyo alipowasilisha mada kwenye kongamano jijini
Arusha.
Kongamano hilo ni maandalizi ya kuelekea
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee.
Amesema mwaka 2002 idadi ya wazee ilikuwa
milioni 1.4, ambao ni sawa na asilimia 4 ya watu
wote kwa wakati huo (milioni 33.5).
Dk. Mung’ong’o amesema idadi ya wazee kwa
sasa inakisiwa kuwa milioni tatu, ambao ni sawa na
asilimia 5.6 ya watu wote. Inakisiwa kuwa sasa
Tanzania ina watu milioni 55.

Kwa upande wa huduma za afya, amesema serikali
kwa kushirikiana na Shirika la HelpAge International
imepitia na kuboresha mtaala wa kufundishia
wauguzi ngazi ya kata ili wapate mafunzo
yatakayowawezesha kuhudumia wazee vizuri.
Amesema kwa kushirikiana na HelpAge
International, serikali imeandaa mwongozo kwa
watoa huduma wa namna ya kutibu magonjwa ya
kawaida yanayowasibu wazee.
Kamishna wa Ustawi wa Jamii nchini, Dk. Naftali
Ng’ondi, akifungua kongamano hilo kwa niaba ya
Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, amesema wazee watatumia fursa hiyo
kujadiliana kuhusu utekelezaji wa sera na miongozo
ya kuboresha hali na maisha ya wazee nchini.
Sera na miongozo hiyo inazingatia utambuzi wa
wazee katika halmashauri, upatikanaji wa huduma
za afya na ushirikishwaji wa wazee.
Maeneo mengine ni huduma za afya kwa wazee na
utekelezaji wa mpango wa huduma rafiki wa afya
kwa wazee na mabadiliko ya utaratibu wa
uchangiaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii na azima ya
serikali kufikia pensheni ya jamii kwa wazee wote.
Kongamano la wazee pia litaangalia sera na mfumo
wa kodi unavyozingatia mahitaji ya makundi
maalumu, msamaha kwa wazee, mauaji ya wazee
nchini na jitihada za kukabiliana nayo.
Kamishna Ng’ondi amesema wazee wana haki ya
kuheshimiwa utu wao na kupata stahiki kama
binadamu wengine, ikiwa ni pamoja na haki ya
kuishi, kupata matunzo katika familia na kulindwa
dhidi ya madhara yanayoweza kuwaathiri kimwili,

kiakili, kihisia na kisaikolojia.
Wazee wameshiriki kongamano la wazee katika
kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya
Wazee yanayofanyika kitaifa Arusha kwa lengo la
kutoa fursa kwa wazee kujumuika na kujadili
changamoto na fursa katika kuboresha maisha yao.
Siku ya Kimataifa ya Wazee huadhimishwa
kutokana na Azimio la Umoja wa Mataifa Na.
45/106 la mwaka 1990, linalozitaka nchi
wanachama kutenga siku maalumu kutafakari
kuhusu mchango wa wazee katika maendeleo ya
jamii.

.tamati…

625 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!