• Aeleza alivyohusishwa na uuzaji wa ‘unga’
• Ataka wasambazaji wahukumiwe kifo
• Afafanua utajiri wake, asema bila kazi huli
Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Idd Azzan, amezungumzia kwa mara ya kwanza tuhuma zinazotolewa dhidi yake kuwa yeye ni muuzaji mkubwa wa dawa za kulevya nchini. Yafuatayo ni mahojiano kati ya Mbunge huyo na JAMHURI yaliyofanyika mjini Dodoma hivi karibuni.

JAMHURI: Mheshimiwa Idd Azzan zipo tuhuma dhidi yako kuwa wewe ni muuzaji mkubwa wa dawa za kulevya hapa nchini. Je, wewe umepata kuzisikia tuhuma hizi, na unazizungumziaje?
Azzan: Nimezisikia tuhuma hizi na hapa ndipo nasema hii ni kampeni, watu wawe makini, vyombo vya usalama vifanye kazi kulinda wananchi na si kujihusisha na mambo hayo.
JAMHURI: Unaweza kufafanua kauli hii?
Azzan: Majibu ninayo. Nimelifuatilia kwa karibu mno suala hili lilipojitokeza. Suala hili halikuwapo kabla mimi sijaingia kwenye ubunge. Lakini nilipoingia kwenye ubunge, ndipo tuhuma hizi dhidi yangu zikaanza. Wanaoshiriki kusambaza tuhuma hizi ni wanasiasa wenzangu.
Mmoja ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM) aliyeshirikiana na watu wengine wenye kulitamani Jimbo la Kinondoni ndio walioshiriki kutengeneza hiyo barua iliyowekwa kwenye mtandao kwa nia ya kuchafua jina langu.
Barua hiyo ilipelekwa China, ikatumwa tena Tanzania kwa njia ya barua pepe. Ikadai kuwa ni mfungwa aliyeko China. Nilifuatilia huko China mfungwa akiwa ndani haruhusiwi kuwa na karatasi wala kalamu. Lazima apate ruhusa ya Mkuu wa Gereza. Lakini barua hii inaonyesha kuwa huyu aliweza kuandika akiwa gerezani akasema wananchi nao wasome ameandika nini. Mamlaka za magereza China niliuliza zikasema hazijaona kitu cha aina hiyo.
JAMHURI: Wanaokutuhumu wanasema kuwa wewe ni wakala, unawaagiza vijana wanaleta ‘unga’. Tuhuma hizi umezisikia mara ngapi?
Azzan: Nilipoingia kwenye siasa nikaanza kusikia hivi vitu. Nikasikia kuna orodha kuwa Amina Chifupa alitaja watu. Kabla ya hapo sijawahi kuhojiwa au kufikiri kufanya. Mimi niliona nimeonewa, nikajipeleka mwenyewe (polisi) kushitaki kwania kuwa wanaonituhumu wapatikane wathibitishe maelezo hayo sheria ichukue mkondo wake… hawa watu wamenizushia kitu ambacho sifanyi. Nilienda polisi kushitaki.
JAMHURI: Ndani ya CCM kuna wabunge wengi. Je, kwa nini usingiziwe wewe?
Azzan: Wapo wanasiasa wanaodhani jina langu likichafuka, basi wao watapata ubunge katika Jimbo ninalolishikilia sasa.
JAMHURI: Kutokana na ushindani jimboni kwako, umepata kupeleleza kujua kina nani wanaolitamani jimbo lako?
Azzan: Wapo wengi. Alikuwa anatajwa [Abas] Tarimba, lakini ameacha siasa. Alianza kupiga jaramba mwaka 2009, lakini sasa amerejea pale Bahati Nasibu ya Taifa kuna hela nzuri kuliko ubunge hivyo alivyopata mkataba mpya akaacha.
Alafu yupo Mama [Zarina] Madabida, yupo kijana Mstafa Muro, huyu naye ana makeke kweli. Kuna mwingine anamtumia kijana mmoja wa usalama wa taifa. Mkuu wa Wilaya (moja ya Dar es Salaam hakumtaja jina) aliniambia kijana huyu anataka kuletea mgombea tumchukue.
Aliweka mkakati wa kuniwekea dawa za kulevya kuharibu jina langu. Vijana wa Usalama wa Taifa wanaocheza naye mpira wakaniambia kuwa amewashawishi wakagoma na nasikia akaahidi kuwa ataniwekea dawa za kuelvya. Baada ya muda nikapata taarifa kuwa kijana huyo [wa usalama wa taifa] kakutwa na kete 3.
Wakati huo nikaambiwa kuwa kijana huyo yupo kwenye geti la Bunge la kukagua wabunge wanaoingia ndani ndiye anayeshika mbwa wa kunusa dawa za kuelvya. Nilivyosikia tukio la kukamatwa kwake na kete 3, nikaandika barua kwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, nikatoa nakala kwa Spika wa Bunge, Mkuu wa Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai.
Kijana huyo kweli alihamishwa pale bungeni, lakini ilinipa shida kidogo. Huyu amepewa hadi mbwa wa kunusa dawa za kulevya, lakini ndiye ikawa wanataka kumtumia aniwekee dawa za kulevya. Iliniogopesha mno. Niliacha kuingiza gari langu bungeni, maana angeweza kunirushia hata kete moja ndani ya gari langu akasema nimekamatwa na dawa hizo na ikawa shida kwangu.
Polisi na Usalama wa Taifa hadi leo hawajajibu barua yangu, ila walichofanya ni kumhamisha kijana huyo. Hii iliniuma sana kuona siasa zinatufikisha hapo na vyombo nyeti vya ulinzi na usalama vinakubali kutumiwa kwa kiwango hicho.
JAMHURI: Unasema umeonewa, je wanaouza ‘unga’ unawafahamu?
Azzan: Rumours (uvumi) zinasema kuwa wapo wauzaji kwa Manyanya (Kinondoni). Kwa uhakika nani anauza au ni nyumba ipi siwezi kufahamu.
JAMHURI: Tatizo lipo, kuna wauzaji na waathirika wa dawa za kulevya. Je, ‘mateja’ unawasaidiaje maana jimbo lako linaongoza hapa nchini?
Azzan: Tumeitaka Serikali kuweka utaratibu wa kuwasaidia waathirika wa dawa za kulevya. Nashukuru Mwananyamala Serikali imejenga kituo cha tiba ya dawa za kulevya kinasaidia. Ninachohangaika ni kujaribu kuwatafutia ajira zinazoweza kuwasaidia wawe na shughuli ya kufanya baada ya tiba iweze kumsaidia kujikimu wasirudi huko. Wapo pia waliosoma wanapata kazi nzuri za ofisini na kampuni binafsi wanakuwa makarani.
Tulianzisha kundi la usafi na sanaa Kinondoni, ila baada ya mafuriko wengi wamehama. Lilikuwa linasaidiwa na halmashauri ambapo halmashauri iliwapa kazi kwa ajili ya kusafirisha barabara. Kukiwa na ujenzi wanatakiwa mafundi, vibarua hawa wanafanya vizuri. Nilikutana na baadhi yao mwaka jana na kuwashauri waache.
JAMHURI: Kwa maoni yako, unadhani kwa nini vijana wanajiingiza kwenye janga hili la dawa za kulevya?
Azzan: Vijana wa ‘dotcom’ (kizazi cha kisasa) wakiangalia maisha ya kwenye mitandao jinsi watu wanavyoishi Ulaya, wanajiingiza kwenye tamaa. Wengine wanafanya hata ushoga kwa sababu ya tamaa. Tuache tamaa zisizo na tija. Hakuna mafanikio ya haraka haraka. Lazima tufanye kazi.
Mwabudu Mwenyezi Mungu, ukitaka kwenda kwenye vitu tofauti, kwamba ukiuza unga unapata hela unakwenda huko mwisho utakuwa mbaya. Biashara haramu unayofanya unawaangamiza wengine kitu ambacho si kizuri.
JAMHURI: Wewe ni mtunga sheria. Unadhani sheria ya sasa ya kudhibiti dawa za kulevya ina upungufu wowote?
Azzan: Sheria ya sasa inamtaka Kamishna wa Tume ya Dawa za Kulevya pekee ndiye atie saini katika hati ya kuthamanisha dawa za kulevya. Huu ni upungufu mkubwa. Mtu mmoja akiwa ndiye mtia saini, hii inaweza ikakwamisha kasi ya kesi kufikishwa mahakamani kama ni hitaji la kisheria. Serikali iangalie upya eneo hili. Huyu akiugua au akifa, kesi zote zinasimama. Kuna haja ya kurekebisha hilo.
Esther Bulaya [Mbunge wa Viti Maalumu CCM] aliwahi kutoa hoja binafsi bungeni kutaka sheria zibadilishwe. Nikubaliane na wazo lake kuwa sheria ziwe kali. Kumpiga faini mtu anayejihusisha na biashara hii haramu ni wazi unampatia mwanya wa kutomfunga kwa sababu atalipa. Lakini wakifungwa muda mrefu, wakitoka watakuwa hawana hamu.
Hata hao waliobaki wakiona mwenzao ameadhibiwa vile, watakosa hamu ya kufanya biashara hii. Kesi ikisikilizwa watakaotiwa hatiani adhabu iwe ni kunyongwa au kufungwa maisha. Mfano ni kosa la mauaji ambapo hukumu yake ni kuuliwa. Kutokana na ukali wa sheria hii, hata ikitokea ugomvi unaoweza kusababisha mauaji, mtu anajitenga. Anajua akihusishwa na mauaji, hatimaye naye atauawa.
Adhabu ikiwa kali watu wataogopa hii biashara, ikiwa ndogo kama za askari wa barabarani, watu wataendelea kuvunja sheria wanajua adhabu ni ndogo.
JAMHURI: Je, unaridhishwa na uendeshaji wa kesi za dawa za kulevya hapa nchini?
Azzan: Utaratibu si mzuri. Mtu amekamatwa anatoa pipi kwa njia ya haja kubwa, inaonekana zimetokea tumboni mwake, lakini kesi inachukua muda mwingi sana. [Mbunge wa Temeke Zuberi] Mtemvu alisema yule mtu [aliyekamatwa na dawa za kulevya] yupo jela, wakati alitaka ahukumiwe mara moja kwani kidhibiti kipo kesi imalizike katika kipindi kifupi ila hii haitokei.
Kama unakosa (ukikamatwa na dawa za kulevya) ufungwe, kama huna kosa uachiwe kuliko kesi kukaa muda mrefu. Kuwe na uharakishaji wa kesi hizi ambazo tayari vidhibiti, ushahidi vipo.
JAMHURI: Kuna wazo la kuanzishwa kwa mahakama maalum ya dawa za kulevya kwa nia ya kuharakisha kesi. Je, unalizungumziaje wazo hili?
Azzan: Sikubaliani na wazo la mahakama maalum. Tutakuwa na mahakama nyingi sana. Wengine watadai mahakama ya rushwa, mwizi wa kuku, mauaji, naamini mahakama zilizopo zinaweza kushughulikia suala hili. Majaji ni wengi, mawakili ni wengi. Ni jukumu la mahakama kuendesha kesi bila kuzichelewesha. Hata ukianzisha Mahakama ya Dawa za Kulevya, tatizo linaweza kuwa lilelile kinachotakiwa ni uharakishaji wa kesi.
Mtu anashuka uwanja wa ndege, kazitoa dawa za kulevya kwa njia ya haja kubwa, zimeonekana, kitu gani kinachelewesha hukumu kuchukuliwa? Kama anahitajika Mlinzi wa Amani awepo na baadae atoe ushahidi mbele ya Mahakama, hukumu inatoke mara moja mchezo unakwisha.
Hali ilivyo sasa, kuna wengine wako ndani, wengine ujanja ujanja wanapata dhamana wako nje. Kasi ya hukumu itaongeza woga. Ikitokea akakamatwa mtu leo, kesho akahukumiwa, mtaani wataogopa. 
JAMHURI: Je, unaridhishwa na kiwango cha madaraka aliyonayo DPP na jinsi anavyoyatumia?
Azzan: Sheria inayompa mamlaka DPP kuwa akiamua kuondoa kesi mahakamani inakuwa na ndo basi hatoi sababu, ni tatizo. Ni lazima aeleze kwa nini ameifuta hiyo kesi au kutoipeleka mahakamani. Kuwepo na mahali anapoweza kuulizwa kwa nini amefuta hiyo kesi, lakini iangaliwe jinsi hata kama anateuliwa na Rais isije ikatokea akatumia vibaya madaraka yake.
JAMHURI: Wewe unatajwa kuwa tajiri, unayo maelezo yasiyotiliwa shaka jinsi ulivyopata utajiri wako?
Azzan: Katika maisha yangu sikupata kufikiria kwamba ipo siku nitamiliki gari. Mwaka 1982, Kaka yangu alininunulia gari ndogo aina ya 504 kutoka Uarabuni. Gari lile niliisajili kama teksi, ila nimesimama barabarani kama wiki moja nafanya biashara ya teksi nikapata rafiki yangu akaniambia hutapata hela kwenye teksi peleka gari lako tours.
Nikaingiza gari tours na mtu wa kwanza kuwa mteja wangu mkubwa alikuwa Nsaka Kaisi. Mwaka 1984, alikuwa akija Dar es Salaam anaichukua gari yangu. Nilipata hela nikanunua ‘costa’ nikaipangia njia ya Pugu Kariakoo. Baada ya mwezi mmoja nikaona kama hela haikai, nikaipeleka tours.
Nikiwa tours nikaingia jeshini kwa msaada wa Luteni Jenerali Charles Makakala, huyu alikuwa mkuu wa Chuo cha Kunduchi. Wakati ule alikuwa Kapteni, ila alikuwa anafanya kazi ‘Court Marshall’. Ikawa namsafirisha kila siku. Huyu ilikuwa unaweza ukakaa miezi mitatu bila kulipwa, ila ukilipwa unapewa hela nzuri. Nilifanya kazi hii kati ya 1985 hadi 1989.
Baada ya hapo nikapata mkataba na kiwanda cha saruji cha ‘Wazo Hill’ kati ya mwaka 1988 mwaka 1992 kusafirisha saruji yao. Mwaka 1992 walinunua magari yao wenyewe, ila baada ya mwaka mmoja ikawashinda hivyo mwaka 1993 wakatangaza zabuni. Nilishinda zabuni ya kusafirisha saruji yao kazi ninayoifanya hadi leo.
Nimesafirisha saruji yao kupeleka Burundi tangu mwaka 1994, hadi leo nasafirisha saruji kwa malori. Nina malori kila gari ikipeleka saruji na mengine nakodisha. Kila gari ikipakia tani 32 napata hela. Baada ya kupata zabuni ya Wazo Hill, jeshini niliacha walinunua magari yao.
Nasafirisha saruji kwenda DRC, Rwanda, Burundi, na si kwa gari moja. Kuna wakati nasafirisha tani 3,000 na zaidi. Wakati inajengwa barabara ya Iringa Dar es Salaam, mimi ndiye niliyesafirisha saruji yote kutoka Wazo Hill kwenda kwenye ujenzi wa barabara hii. Hivi kweli kwa muda wote niliofanya biashara hii bado mtu anapata shaka nimepataje hela kweli? Tumwogope Mungu.
JAMHURI: Je, unashauri nini kuhusiana na tatizo hili la dawa za kulevya?
Azzan: Sheria zibadilishwe kudhibiti uingizwaji wa dawa za kulevya. Ni vyema sheria iwabane wanaotumia dawa waseme mimi nanunua kwa fulani. Uchunguzi wa kina ufanyike na wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Kwenye hili tuache kusingizia watu. Usione mtu kapata mafanikio ukadhani ameuza unga. Watu wamepata mafaniko kwa kazi halali. Tusione kila kijana akipata hela ni unga. Wapo watu Mwanza, mikoani, wameanza kwa kuuza mazao gunia 10 leo wanauza mazao kwa matani na ni matajiri wakubwa sana, akaunti zao zina mabilioni. Mwenzangu na mimi ukiona kijana ana gari nzuri, nyumba unasema kauzi dawa. Tusikurupuke.
Tunaenda kwenye uchaguzi, niwaombe wanasiasa uchwara waache tabia ya kuchafua wenzao. Wananchi ndio wataamua kuwa huyu anafaa au vinginevyo. Kumzushia mwenzako ili upate nafasi hiyo, si jambo zuri. Tuangalie kauli zetu, tuombe kura kwa ustaarabu wananchi wenyewe wataamua.
Kwa vijana, ninawashauri kuwa ajira za halali zipo nyingi sana. Vijana wawe wabunifu kuangalia kitu gani kinaweza kuwapatia kipato halali. Dawa za kulevya, ujangiri, kuiba, mwisho wake ni mbaya tu. Tunayo ardhi kubwa na ya kutosha. Kijana anapaswa kuchukua ardhi akaanza kulima.
Ulimaji wa kisasa ekari moja, mbili unapata mapato makubwa. Kina Masanja, ‘wa the original comedy,’ wanazalisha mpunga Mbarali. Wamewekeza kwenye kilimo, wana maeneo makubwa. Wanapata hela nzuri sana. Wamewezaje wao? Watu wakikaa vijiweni wanaweza kuwa wanasema labda wanauza unga wale, kumbe sio.
Kijana akiwa mbunifu ataachana na hayo mawazo. Tanzania tuna ardhi ya kutosha, ukienda Dar es Salaam, Mkuranga, Rufiji, maeneo yapo kibao. Watu wakalime tu.

By Jamhuri