Wiki hii ni ya majaribu ya aina yake kwa Bunge la Tanzania na dhana ya utengano wa madaraka, kwa maana ya kudurusu ukuu wa Katiba mbele ya sheria nyingine za nchi. Sidhani kama natakiwa kutumia muda mwingi kueleza kashfa ya IPTL kuhusiana na akaunti ya Escrow.

Hata hivyo, si sahihi sana nikaamini kuwa kila mtu anajua maana ya akaunti ya Escrow, hivyo ni vyema nikaieleza kidogo Escrow ni nini na ilifikaje IPTL. Escrow ni akaunti inayofunguliwa inapotokea wabia wawili wakawa na ugomvi kuhusiana na mapato yao.

Kwamba A anafanya biashara na B, kisha hawaelewani, basi hufungua akaunti ya kuweka fedha wanazopata kutokana na biashara wanayofanya, kwa maana kuwa wakati ugomvi unaendelea, biashara nayo inaendelea na wateja wanalipa, hivyo fedha zinazotokana na biashara zinatunzwa kwenye akaunti maalum hadi ugomvi uishe, ndipo wagawane.

Hilo ndilo lililotokea kwa Kampuni ya VIP Engineering inayomilikiwa na James Rugemalila na kampuni ya Mechmar. Hawa walikuwa wabia walioanzisha biashara pamoja kupitia kampuni ya IPTL. Mradi huu harufu yake ilianza mwaka 1994, ukawa na mgogoro mkubwa, ukachelewa kuanza rasmi hadi mwaka 2000.

Mwaka 2006 waliingia mgogoro, hivyo ikabidi wapelekane mahakamani na kadri siku zilivyokwenda wakalazimika kufungua akaunti ya kuhifadhi fedha zilizotoka TANESCO kutokana na kuzalisha umeme zijulikanazo kama capacity charge. Hizi ndizo zinatajwa kama dola milioni 250 zilizokuwa kwenye akaunti hii. Hata hivyo, gazeti JAMHURI katika toleo la leo repoti nzima ya CAG iliyovuja imechapishwa inaeleza kwa uwazi kila kitu, isome.

Sitanii, nafahamu wengi mmesoma mengi kuhusu suala hili la IPTL, lakini mimi nimeona heri nizungumzie eneo moja tu la kisheria, lililoanza kuleta mkoroganyo wa mawazo kati ya Serikali na Bunge. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amezungumza lugha ya kisheria. Akashauri Bunge lipime na kuangalia iwapo halitakuwa linaingilia muhimili mwingine wa dola kwa kujadili suala la IPTL ambalo lipo mahakamani.

Hapa, Pinda alikuwa anatumia dhana ya mwanasheria nguli, Mfaransa Charles Montesquieu, aliyeanzisha dhana ya utengano wa madaraka katika miaka ya 1800. Montesquieu, alijenga hoja kuwa kwa nia ya kuweka mipaka na kujenga misingi ya utawala Bora, basi kuwepo utengano wa madaraka, kwa maana ya kuanzisha mihimili mitatu ya dola.

Akapendekeza na ikakubaliwa kuwa dola (Serikali) igawanyike katika mihimili mitatu kwa maana ya Bunge (litunge sheria), Mahakama (itafsiri sheria) na Utawala (wasimamie sheria). Hakika mfumo huu umekubalika kwa kiasi kikubwa katika sehemu nyingi duniani na ndio unaochukuliwa kama utawala bora ikiwa mgawanyo huu unaheshimiwa.

Msimamo huu ndio jaribio kuu kwa Katiba ya Tanzania. Desemba 10, mwaka 1948 lilipita tamko la msingi la Haki za Binadamu. Kifungu cha 19 cha tamko hili, kikatoa uhuru wa kupokea na kutoa mawazo. Hii ikajumuisha vyombo vya habari, wananchi wa kawaida na viongozi kwa ujumla.

Sitanii, Tanganyika na hatimaye Tanzania, hatukuwahi kulikubali tamko hili tangu uhuru hadi mwaka 1984 yalipofanyika mabadiliko ya 5 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndipo haki za msingi za binadamu ikiwamo Ibara ya 18 inayoimbwa mno kuwa inatoa uhuru wa mawazo na vyombo vya habari zilipopata nafasi.

Watunga sheria wetu, kwa kuwaza zaidi vyombo vya habari wakatunga sheria mbaya. Wakaona wanahabari ni wadaku na wadukuzi. Kwa dhana kuwa wanadhibiti vyombo vya habari, wabunge wakatunga sheria inayozuia mtu yeyote au chombo chochote kujadili, kuchapisha, kuhoji au kutoa taarifa yoyote katika suala lililopo mahakamani.

Hapa, wabunge wakatunga Kanuni ya Adhabu (Penal Code) Sura ya 16, ambayo katika Kifungu cha 114 (1) (d) inaanzisha kosa la Kudharau Mahakama. Kosa hili lina adhabu ya mtu kwenda jela miezi sita au kupigwa faini ya Sh 400. Wakati wabunge wanatunga sheria hii, walikuwa wakiwaza vyombo vya habari, hawakujua kuwa nao ni watu.

Sitanii, sheria hii haikomei kwenye vyombo vya habari. Ama kwa upofu, au kwa kuburuzwa, wabunge wakaridhia Kanuni ya 64 (c) ya Kanuni za Kudumu za Bunge. Kanuni hii inamzuia Mbunge yeyote kujadili, kuhoji au kuzungumza suala lolote lililoko mahakamani, kwa dhana ya mihimili ya dola kuheshimiana na kutoingilia uhuru wa Mahakama.

Hata hivyo, Ibara ya 100 ya Sheria Mama, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inamruhusu mbunge kusema au kufanya jambo lolote akiwa bungeni. Ibara hii inatafsiriwa na Sheria ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge ya Mwaka 1988, ambayo inaendeleza uhuru wa mbunge kutoa mawazo bungeni.

Leo, inawezekana kuna kikundi cha watu serikalini, ambacho kinaona masilahi yao yako hatarini. Kikundi hiki sasa kinaikumbuka Sheria ya Kudharau Mahakama. Wabunge wamesema wala wao hawatajadili kesi iliyoko mahakamani, bali ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), leo tunapata kigugumizi.

Sitanii, nafurahi kuwa wabunge wemefikishwa kwenye kona mbaya katika suala hili la IPTL. Ni Tanzania pekee ambapo Sheria inayotungwa na Bunge inaweza kuwa na nguvu kuliko Katiba. Kwamba Katiba inawaruhusu wabunge kujadili jambo lolote, likiwamo hili la IPTL, lakini sheria inayotokana na Katiba inawakataza, wanaufyata. Ajabu kweli.

Kazi yetu hii inahitaji roho ngumu. Najua kuna majina ya wakubwa yanatafutwa katika kashfa hii. Watanzania pia naomba tujiandae kisaikolojia. Tusizoee kudhani wezi ni wanasiasa pekee. Kuna watendaji ambao ni hatari. Kuna majaji, mawakili na watu wamezoa fedha za IPTL kama njugu.

Wapo watendaji walioaminiwa kuwa watoza ushuru kwa niaba ya Serikali, lakini wamefika mahala sasa wanawaelekeza watoa ushuru jinsi ya kukwepa ushuru. Hawa si mawaziri, si makatibu wakuu na wala si wabunge. Nasema, nieleweke vizuri hapa. Ndio, wapo wabunge na mawaziri waliochota fedha hizi, lakini watendaji ndio usiseme.

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai hadi tunakwenda mitamboni alikiri kuwa uzalendo umewashinda Kamati ya Uongozi ya Bunge. Wameamua kusimamia ukuu wa Katiba. Ibara ya 100 ya Katiba imechukua mkondo na hivyo Bunge litaijadili ripoti hii kwa siku mbili kati ya Novemba 26 na 27.

Binafsi sitaki kuingia katika kilichomo undani wa ripoti hii. Kwa kuwa imevuja na tumeipata na gazeti hili la JAMHURI limeichapisha kwa hoja kuwa tayari taarifa ikiishafika mikononi mwa Bunge inakuwa waraka wa wazi. Someni muone Benki Kuu ya Tanzania ilichofanya Novemba 28, 2013. Inatisha.

Sitanii, makala yangu ni juu ya ubaya wa sheria zinazozuia haki ya kupata habari. Kama si shinikizo la kisiasa, ripoti hii ya CAG wala jamii isingeiona. Ipo pia ripoti ya TAKUKURU. Kwa Serikali zinazojiendesha kwa uwazi, hii nayo ingewekwa hadharani. Imekabidhiwa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Kwa ripoti hizi kutowekwa wazi nchi inaendelea kuishi kwa umbea tu. Mara tunaambiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi ndiye mtuhumiwa namba moja, mara tunaambiwa waziri wake Profesa Sospeter Muhongo ndiye kinara, wengine wanamtaja Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na wengine.

Binafsi jicho langu halikuanini. Nilipoziona ripoti hizi mbili wala sikukuta wakitajwa hao. Hata ushahidi wa mazingira, hauonyeshi hivyo. Wapo watendaji kama Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu wanayo maswali mengi ya kujibu. Yupo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ana maswali mengi ya kujibu.

Wapo watendaji ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao walijua kuwa hisa za IPTL zimeuzwa kwa Piper Link kwa dola milioni 6, sawa na Sh bilioni 10.2, lakini wakawatoza kodi ya Ongezeko la Mtaji kwenye Sh milioni 6 za Tanzania. Piper Link iliuza hisa asilimia 70 za IPTL kwa PAP kwa dola milioni 20 karibu Sh bilioni 37, lakini watoza ushuru wa TRA wakawatoza kodi kwenye dola 300,000 (sawa na Sh milioni 480 wakati huo).

Sitanii, hapo ndipo kilipolala kilio change. Haki ya kupata habari ni ya kila Mtanzania. Utaratibu wa kuficha taarifa na kuwafanya baadhi ya watendaji ndani ya Serikali kuwa binadamu daraja la kwanza, kwa maana ya wao tu kuziona na kuzishikilia taarifa kisha wakaamua kuipotosha jamii haufai.

Nasema sakata la mjadala wa taarifa hii ya IPTL/Escrow uwe fundisho. Wabunge sasa wakubali sheria ya haki ya kupata habari, na wasikubali kamwe kutunga sheria inayopingana na Katiba. Wasingetumia ubabe, ripoti hii isingejadiliwa. Tujifunze kutokana na makosa.

Mwisho, nahitimisha kwa ombi kuwa ikiwezekana hawa waliotajwa kwenye ripoti ya TAKUKURU kwa kupokea hizi fedha wahojiwe kwa nini walipewa hizi fedha na majibu yao yasiporidhisha, basi wawajibishwe kwa kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria. Tukiwajibika, maendeleo hayatatupita. Tusioneane, ila tutendeane haki kwa uwazi katika hili.

By Jamhuri