Mara kwa mara katika hotuba zake Rais John Magufuli hukumbusha wajibu wa viongozi katika ngazi zote kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia wapiga kura. Amekumbusha tena kwenye hotuba yake hivi karibuni kwa watendaji wa kata aliyowaalika Ikulu.

Alisisitiza umuhimu wa watendaji kusimamia utekelezaji miradi ya maendeleo ya Serikali, akiwakumbusha jukumu lao muhimu sana la kudhibiti ubadhirifu na ukiukwaji wa maadili.

Alisema Serikali inahitaji udhibiti huo kwenye kata zao kwa sababu inapeleka mabilioni ya fedha kwenye miradi ya sekta mbalimbali kama afya, elimu, maji, umeme, na miundombinu. Alitumia fursa ya hotuba yake kuwajaza ujasiri watendaji, akiwaasa wawe mstari wa mbele na bila woga kufichua ubadhirifu na utekelezaji hafifu katika miradi hiyo.

Kwenye mfumo wa Serikali uliyopo mamlaka ya mtendaji wa kata yanazidi ya mtendaji wa kijiji tu kabla ya kumfikia mpiga kura. Juu yake kuna mkurugenzi wa halmashauri, mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa na wateule wengine kama mawaziri. Wote hawa, rais amesema, ni watumishi wa umma ambao wanapaswa kusimamiwa vyema na mtendaji ili watekeleze majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya utumishi bora.

Pamoja na nia njema iliyopo, Rais amewabebesha mzigo ambao wachache wataumudu. Wale watakaoubeba watakuwa na ujasiri mkubwa wa kuwa tayari kupambana na nguvu kubwa ya mfumo wowote wa utawala ambao, kwa kawaida, hulinda maslahi ya waliyomo – maslahi mazuri na maovu.

Ni binadamu wachache wanaokubali makosa. Wengi wetu hutumia kila mbinu kuficha maovu na ikiwezekana kuwaadhibu wale wanaotufichua. Nina taarifa za afisa mmoja wa halmashauri aliyefichua ubadhirifu kwenye mchakato wa uchaguzi wa marudio kwenye kata moja ambaye aliadhibiwa na wakubwa zake, akaondolewa kwenye kazi yake na kurudishwa kwenye ualimu. Hizi ndiyo dhahma zinazowakabili wajasiri.

Tatizo si kusema, tatizo ni kutaja maovu kwenye mfumo ambao unasimamiwa na wale wale ambao wanashiriki kwenye maovu na wana uwezo mkubwa na mtandao mpana wa kuhakikisha kuwa taarifa zozote zinazowaathiri hazivuki nje ya wilaya au mkoa husika.

Taarifa zitakazopenya ni ndogo sana kulinganishwa na zile ambazo zitazimwa. Inahitaji mfano mmoja wa ofisa aliyerudishwa kwenye ualimu kuwanyamazisha wengi.

Rais alisema kuwa watendaji ni watu walio karibu sana na wananchi kwa hiyo ni rahisi zaidi kwao kufahamu matatizo yaliyopo. Ni kweli, lakini sifa hiyo hiyo inaweza kuwa na sura mbili kutegemea na msimamo wa mtendaji na tafsiri yake ya wajibu aliyonao.

Sura ya kwanza ni kuwa mtendaji yule jasiri mfichua maovu ambaye Rais anamhitaji anaweza kuamua kuwa karibu na wapiga kura na kujitosa kulinda maslahi ya wapiga kura, akawa tayari kukabiliana na kila aina ya vikwazo na adhabu.

Sura ya pili inajitokeza akiamua kuegemea kwa wakubwa zake, si kwa woga, bali kwa kuchagua, akatetea kila kitu kinachofanywa na wakubwa hao – kiwe kwa maslahi ya wote au kwa maslahi binafsi. Haihitaji utaalamu mkubwa kuona kuwa wapo na watakuwapo watendaji ambao watashirikiana na wakubwa zao kwenye ubadhirifu na utendaji mbovu katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.

Kwa hiyo kuna vizingiti vikubwa viwili vya kukwamisha uwezekano wowote wa meno aliyotoa Rais kwa watendaji kuuma na kujeruhi: woga wa watendaji kuwasema wakubwa zao, na uamuzi wa watendaji kuwa karibu na wakubwa hao badala ya kuwa karibu na wapiga kura.

Ipo njia ya kuyaongezea nguvu yale meno: wapiga kura wenyewe. Mpiga kura akipewa uwezo na nafasi ya kutaja kero zinazomzunguka atafanya hivyo kwa uwazi zaidi. Sababu ni kuwa yuko karibu na anasumbuliwa zaidi na zile kero kuliko kiongozi wa ngazi yoyote.

Aidha, hana woga kuwa akifichua maovu atafukuzwa kazi au kuhamishwa kama yule afisa aliyerudishwa shuleni kufundisha.

Baadhi ya nchi zimeunda wadhifa wa aina ya kiranja ambaye anawachunga wakubwa kwa niaba ya wadogo. Kwa Kiingereza anaitwa ombudsman, au mchunguzi maalumu. Huyu kazi yake moja tu: kupokea malalamiko ya raia dhidi ya vitendo vya utawala mbovu na ukiukwaji wa haki za raia na kutafuta suluhu.

Mamlaka ya kisheria ya kiranja huyu yanatofautiana baina ya nchi na nchi. Atakayetufaa atakuwa yule mwenye nguvu inayolindwa kikatiba inayokaribiana na ile ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Atateuliwa na kuhudumia kwa muda uliopangwa na hataondolewa kwenye nafasi yake mpaka kipindi chake kitakapoisha, isipokuwa tu kwa ukiukwaji wa maadili ya utumishi.

Atakuwa na uwezo wa kutoa mapendekezo ya kutatua kero na uwezo wa kuagiza kuchukuliwa kwa hatua za kinidhamu na kisheria dhidi ya wale wanaokutwa na makosa ya kiutendaji au ukiukwaji wa maadili ya utumishi. Atakuwa na wawakilishi katika kila mkoa ili kufikisha huduma karibu na wapiga kura.

Vichwa vya habari wiki iliyopita vilisema kuwa Rais amewapa meno watendaji wa kata. Hoja yangu ni kuwa kama ni mfano wa meno ya binadamu, sidhani kama yanatosha. Inahitaji meno ya simba kufikia malengo. Huyu kiranja atawapa wananchi nguvu ya meno ya simba.

Maoni: [email protected]

By Jamhuri