Na Charles Ndagulla, Moshi

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Aishiel Sumari, ameandamwa tena na wananchi wanaokataa asisikilize mashauri yaliyo mbele yake kwa madai kuwa hawana imani naye.
Hatua hii inakuja huku kukiwa na taarifa kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Moshi kuwa jaji huyo yuko katika maandalizi ya kustaafu utumishi wa umma kwa mujibu wa sheria.
Ally Hussein Mitta, ambaye ni mdaawa katika shauri Na. 41/2017 amemwandikia barua Jaji Sumari akimtaka ajitoe kusikiza shauri hilo lililopangwa kusikilizwa keshokutwa.
Akizungumza na JAMHURI mjini hapa, Mitta amesema msingi wa kumkataa Jaji Sumari kusikiliza shauri hilo ni kutokana na kuwepo kwa mazingira yanayowatia shaka.
Shauri hilo lilifunguliwa mahakamani hapo na Ramadhan Mohamed Mitti, anayepinga uamuzi wa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Moshi, uliompa ushindi Ally kuwa ndiye mmiliki halali wa nyumba iliyopo kwenye kiwanja namba 40, kitalu E, Section III, iliyopo Mtaa wa Selous, Manispaa ya Moshi.

Uamuzi huo ulitolewa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza, Mussa Mahelela, Oktoba 31, 2013 na tangu wakati huo Ramadhan hakuwahi kuomba kukata rufaa kwa zaidi ya miaka mitatu hadi alipoomba kufanya hivyo mwaka jana.
Kwa mujibu wa barua aliyomwandikia Jaji Mkuu wa Tanzania ya Agosti 20, mwaka huu, Ally anadai kuwa shauri hilo linasikilizwa kinyume cha sheria za nchi na taratibu za mahakama.
“Mheshimiwa Jaji Mkuu, baada ya shauri kuanza kusikilizwa na Mahakama Kuu Kanda ya Moshi mbele ya Mheshimiwa Jaji Sumari, tuna ushahidi kuwa kuna mazingira ya ukandamizaji [yanayoendelea],” inasema barua hiyo ambayo nakala yake tunayo.

Ally anadai katika barua hiyo kuwa tangu shauri hilo litolewe uamuzi na Baraza la Ardhi la Wilaya mwaka 2013, Ramadhan hajawahi kuomba mapitio ya hukumu hiyo ili aweze kukata rufaa, huku akisisitiza shauri lililopo mbele ya Jaji Sumari linakosa uhalali wa kisheria wa kuendelea kusikilizwa.
Katika shauri hilo, Ramadhan ambaye ni ndugu yake Ally, anaiomba mahakama kubatilisha uamuzi wa Baraza la Ardhi na kumtambua yeye kama mmiliki halali wa nyumba hiyo.
Kwa mantiki hiyo, Ally anamwomba Jaji Mkuu kutumia mamlaka yake kuwachukulia hatua wote wanaoendelea kusikiliza shauri hilo akidai kuwa lilitolewa uamuzi na mhusika hakuwahi kuomba mapitio ndani ya muda wa siku 90 kama sheria inavyotaka.

Mapema mwaka jana, Ramadhan aliwasilisha maombi Mahakama Kuu ya kukata rufaa nje ya muda unaokubalika kisheria na maombi hayo yalikubaliwa, hivyo kufunguliwa shauri hilo namba 41/2017.
Awali shauri hilo lilikuwa mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Patricia Fikirini, kabla ya Ally kumkataa kwa kile alichodai jaji huyo alikataa kuidhinisha malipo ya wakili wake ya Sh milioni tatu na kuidhinisha kiasi cha Sh 1,040,000.
Mbali na barua hiyo, Ally pia amemwandikia barua Jaji Sumari mwenyewe ya Agosti 31, mwaka huu ambayo Gazeti la JAMAHURI linayo nakala yake, akimtaka ajitoe kusikiliza shauri hilo kwa kile anachodai hana imani naye.
Nakala ya barua hiyo imesambazwa kwenye taasisi 11, ikiwamo Ofisi ya Rais, Jaji Kiongozi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Waziri wa Sheria na Katiba, Tume ya Haki za Binadamu, Mkurugenzi wa Takukuru na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Frank Mahimbali, hakupatikana kuzungumzia barua hizo zinazomtaka Jaji Sumari kujitoa kusikiliza shauri hilo.
Tukio hili ni la pili kwa Jaji Sumari kuingia majaribuni ambapo hivi karibuni alipokwa jalada la kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Scolastica, Humphrey Makundi (16).
Hatua hiyo ilitokana na familia ya mwanafunzi huyo kumwandikia barua Jaji Kiongozi kulalamika kuwa haki isingetendeka katika shauri hilo baada ya Jaji Sumari kudaiwa kujipangia shauri hilo licha ya katazo la Jaji Kiongozi.
Kwa sasa jalada hilo liko chini ya Jaji Huruma Songoro, ambaye amewahi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, huku Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula, akiwa chini ya Wakili Mkuu wa Serikali, Joseph Pande.
Shauri hilo la jinai namba 48/2018 linawakabili washtakiwa watatu akiwamo Mkurugenzi wa Shule hiyo, Edward Shayo, aliyekuwa mlinzi wa shule hiyo, Hamis Chacha, ambaye ni mshtakiwa wa kwanza na Laban Nabiswa, aliyekuwa Mwalimu wa Nidhamu ambaye ni mshtakiwa wa tatu.

Kutokana na malalamiko hayo, Jaji Kiongozi, Eliezer Feleshi, alimtaka Jaji Sumari amjulishe mara tu kesi hiyo itakapofikia hatua ya ‘plea taking’ na ‘PH’ ili ateue jaji wa kuisikiliza, lakini kinyume cha maelekezo ya Jaji Kiongozi, Sumari alijipangia kuisikiliza kesi hiyo Agosti 27, mwaka huu lakini Jaji Kiongozi akampoka jalada hilo.
Barua hiyo ya Jaji Kiongozi ya Julai 31, mwaka huu yenye Kumb. Na. HA. 59/190/02 ‘C’/3, iliandikwa na kusainiwa na D. B. Ndunguru, ambaye ni Katibu wa Jaji Kiongozi na nakala ya barua hiyo kunakiliwa kwa Jackson Makundi ambaye ni baba mzazi wa marehemu Humphrey Makundi.

1775 Total Views 5 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!